Kwa ufupi
Wakati mchakato wa kumfungulia mashtaka ukiwa 
unaendelea ofisa huyo alitoroka usiku wa Desemba 17 kuamkia 18 mwaka 
jana, hivyo ofisa huyu ni mtoro kwa kipindi cha ziadi ya miezi minane.
Dar es Salaam. Jeshi la Wananchi wa Tanzania 
(JWTZ), linamtafuta ofisa wa jeshi hilo, Luteni Kanali, Colestine 
Seromba, baada ya kutoroka na kuelekea kusikojulikana.
Ofisa huyo aliyekuwa Mkufunzi katika Chuo cha 
Mafunzo ya Kijeshi cha Kompyuta kilichopo Dar es Salaam, anasadikiwa 
kutoroka na nyaraka muhimu za jeshi hilo tangu Desemba 18, mwaka jana.
Msemaji wa jeshi hilo, Meja Erick Komba 
akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi jijini humo jana
 alisema, Seromba alikuwa na tuhuma za makosa ya kijeshi na ndiyo sababu
 ya kutoroka kwake.
“Wakati mchakato wa kumfungulia mashtaka ukiwa 
unaendelea ofisa huyo alitoroka usiku wa Desemba 17 kuamkia 18 mwaka 
jana, hivyo ofisa huyu ni mtoro kwa kipindi cha ziadi ya miezi minane,” 
alisema Meja Komba na kuongeza:
“Kijeshi kosa la utoro halifutiki, yaani halina 
‘Time Bar’. Kwa maana hiyo bado ofisa huyu anaendelea kutafutwa na 
akipatikana hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.”Meja Komba 
alisema ofisa huyo ni Mtanzania mzaliwa wa Kijiji cha Rukira mkoani 
Kagera na si Mnywaranda kama ambavyo baadhi ya taarifa zinavyoenezwa.
Akijibu swali aliloulizwa kuhusu ofisa huyo kuwa 
Mkuu wa Chuo hicho, Meja Komba alisema alikuwa mkufunzi wa masomo ya 
kompyuta na taarifa nyingi alizokuwa nazo ni zile zilizowahusu wanafunzi
 yaani mahudhurio na matokeo yaliyowahusu wanafunzi.
“Mkuu wa chuo hicho hakuwa yeye alikuwa Kanali 
Obeid ambaye naye amestaafu miezi sita sasa, lakini jeshi lilipoanza 
uchunguzi dhidi yake alikabidhi vitendea kazi vyake vyote,” alisema Meja
 Komba.
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper