Posted Jumatano,Agosti28 2013 saa 21:28 PM
Kwa ufupi
- Asema msimamo wa Mansour ndiyo alionao hata mwenyewe na kwamba, haki haikutendaka kutompa nafasi ya kujitetea.
 
Zanzibar. Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya 
Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, akisema uamuzi wa CCM kumfukuza
 uanachama Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid, 
siyo sahihi, Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Wilaya ya Dimani, 
Unguja umesema chama hicho kiwatazame vigogo wengine wanaokwenda kinyume
 cha maadili yake.
Halmashauri Kuu ya CCM ilimvua uanachama Mansour 
kwa kile kilichoelezwa kukisaliti chama, kwa kushindwa kusimamia malengo
 ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama, kushindwa kutekeleza wajibu
 wa mwanachama na kukiuka maadili ya viongozi wa CCM na kuikana ilani ya
 CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2010-2015 na kuisaliti CCM.
UVCCM ilidai kuwa hatua hiyo isimkumbe peke yake, 
badala yake iwatizame wabunge, wawakilishi na viongozi wengine 
wanaokwenda kinyume na sera za chama hicho.
Taarifa ya umoja huo kwa vyombo vya habari 
iliyosainiwa na Katibu wa UVCCM Wilaya ya Dimani, Yussuf Suleiman, 
inadai umoja huo umepata faraja na imani kuona chama chao kinatetea 
nidhamu ili kukabiliana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na mwakilishi 
huyo.
Pia, inadai umefika wakati wa uongozi wa chama 
hicho kuchukua hatua za maadili dhidi ya wawakilishi na wabunge ambao 
mchana ni CCM na usiku hugeuka maadui na wasaliti.
Moyo apinga
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema jana mjini hapa 
kwa simu kuwa Mansour ameonewa, kwa sababu hakupewa nafasi ya kujitetea 
kabla ya kuchukuliwa hatua ya kufukuzwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.
Moyo (pichani kulia) aliyewahi kushika nyadhifa 
mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa miaka mingi, 
alisema hata yeye, moyo wake upo kwenye muundo wa Serikali ya Muungano 
wa Mkataba.
Watu waonaotaka Muungano wa Mkataba katika 
mapendekezo ya Katiba Mpya inayojadiliwa sasa wanataka ziwepo Serikali 
mbili za Tanganyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili, baadaye kuwapo na 
Muungano wa mkataba baina ya Serikali hizo.
“Utashi wangu ulikuwa kwenye mkataba, lakini 
Kamati ya Katiba haikutupa kwa hiyo sasa kete yangu naitupa kwenye 
Serikali tatu,” alisema Moyo.
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa atajivua uanachama 
wa CCM ikiwa Mansour atafukuzwa, Moyo alisema hakuwahi kusema hivyo bali
 alieleza ikiwa Mansour anafukuzwa na yeye anaweza kufikwa na hatua kama
 hiyo, kwani ana fikra sawa na Mansour.
“Sijasema nitajivua uanachama, ila nilieleza kuwa 
nami nitakuwa na hali kama hiyo ya Mansour kwani msimamo wangu si 
tofauti,” alisema Mzee Moyo.
CCM kina msimamo wa kutaka mfumo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar uendelee.
Hata hivyo asilimia kubwa ya wananchi wa Zanzibar 
waliotoa maoni yao kwa Kamati ya Katiba wanataka Muungano wa Mkataba na 
Serikali mbili za Tanganyika na Zanzibar, zenye mamlaka kamili na Kamati
 ya Katiba imetoa rasimu yenye kupendekeza Serikali tatu; Shirikisho, 
Zanzibar na Tanzania Bara.
Mansour agoma
“Naomba uniache tafadhali, nasikitika kuwa sitakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa sasa,” alisema.
Jumamosi iliyopita Mansour alizungumza na gazeti 
na kusema anasubiri uamuzi wa Halmashauri Kuu kujua hatma yake na 
kuahidi kuwa, angezungumza baada ya uamuzi huo, jambo ambalo ameshindwa 
kutekeza kwa kuendelea kuwa kimya.
Mara ya kwanza, tuhuma za Mansour zilifikishwa 
katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 
16, mwaka huu Ofisi za CCM Kisiwandui na wajumbe wa kamati hiyo kwa 
kauli moja walitoka na azimio la kumvua uanachama. Uamuzi wa kumvua 
uanachama Mansour uliwasilishwa katika kikao hicho chini ya Makamu 
Mwenyekiti wake, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. 
Hatua hiyo inaliacha wazi Jimbo la Kiembesamaki kwa ajili ya uchaguzi wa
 mwakilishi.
source : Mwananchi
source : Mwananchi