Rais Jakaya Kikwete ambaye hivi karibuni alivitaka vyombo husika 
kuhakikisha kuwa vinawasaka na kuwarudisha kwao wahamiaji haramu 
            
Kwa ufupi
Kauli na matamko ya viongozi mbalimbali ambayo 
yamekuwa yakitolewa katika nyakati tofauti yanaonyesha pasipo kuacha 
shaka kwamba Serikali bado haijatambua ukubwa wa tatizo la wahamiaji 
haramu katika mkoa huo.
Serikali inaonekana kupatwa na kiwewe na 
kuridhishwa na mafanikio kiduchu katika suala la kuwarudisha makwao 
wahamiaji haramu katika Mkoa wa Kagera.
Kauli na matamko ya viongozi mbalimbali ambayo 
yamekuwa yakitolewa katika nyakati tofauti yanaonyesha pasipo kuacha 
shaka kwamba Serikali bado haijatambua ukubwa wa tatizo la wahamiaji 
haramu katika mkoa huo.
Inawezekana kwamba viongozi serikalini hawakuamini
 kwamba agizo la Rais Jakaya Kikwete kuhusu wahamiaji haramu mkoani 
Kagera kurudi makwao lingepata mafanikio angalao kidogo. Yafaa tukumbuke
 hapa kwamba Rais alipofanya ziara katika Mkoa wa Kagera mwishoni mwa 
mwezi uliopita aliwapa wiki mbili wahamiaji haramu wawe wamerudi makwao 
kwa hiari yao, vinginevyo wangekamatwa katika operesheni maalumu ya 
kijeshi baada ya muda huo kuisha.
Takwimu zilizotolewa baada ya muda huo kuisha 
ziliwapa viongozi wa Serikali matumaini makubwa kupita kiasi, hivyo 
kutoa matamshi na kauli zilizoibua hisia miongoni mwa wananchi kwamba 
sasa tatizo la wahamiaji haramu katika mikoa hiyo limekwisha. Bahati 
mbaya ni kwamba wananchi hawakuweza kutambua kwamba tatizo la wahamiaji 
haramu bado ni kubwa mno kuliko Serikali inavyofikiria, mbali na takwimu
 zilizotolewa na viongozi mbalimbali serikalini katika wakati tofauti 
kutofautiana, hivyo kuibua maswali mengi kuhusu usahihi na uhalisia wa 
takwimu hizo.
Juzi katika nyakati tofauti viongozi wa Serikali 
walitoa takwimu zilizoonyesha mkanganyiko huo. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, 
Fabian Massawe alisema kati ya Julai 29 mpaka juzi wahamiaji haramu 
8,262 walikuwa wameondoka mkoani humo kuelekea Rwanda, Burundi, Uganda 
na DRC. Alisema kati ya hao, wahamiaji 5,200 walikwenda Rwanda, 2,800 
walikwenda Burundi, 220 Uganda na 42 walielekea DRC, huku wakisalimisha 
silaha 42, zikiwamo za kivita aina ya AK47.
Lakini siku hiyohiyo, Wizara inayohusika na 
masuala ya kigeni, ilitoa taarifa kwamba idadi ya wahamiaji haramu 
walioondoka kwenda makwao ni 8,509. Alisema waliokwenda Rwanda ni 5,521 
na kwamba Burundi walikwenda 2,744 wakati Uganda walirejea wahamiaji 
244. Kuhusu silaha, wizara hiyo ilisema bunduki 60 zilizotengenezwa 
kienyeji ndizo zilizosalimishwa.
Hata hivyo, takwimu ambazo hazikuwa na utata ni za
 mifugo. Taarifa ya Wizara na ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera zote zinataja 
1,996 kama idadi ya mifugo iliyosafirishwa na wahamiaji hao wakati 
wakirudi makwao.
Tumechapisha takwimu hizo ili kuonyesha kutokuwapo
 kwa umakini katika mamlaka zinazohusika na jambo nyeti kama hilo na pia
 kuonyesha kwamba tatizo la wahamiaji haramu bado ni kubwa mkoani 
Kagera. Inakadiriwa kwamba wapo wahamiaji haramu mkoani humo zaidi ya 
50,000.
Sensa ya watu hao ya mwaka 2006 ilionyesha 
walikuwa 32,000 na iliongezeka kwa kasi ya ajabu baadaye kutokana na 
kuongezeka kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi katika mamlaka 
za kiserikali, zikiwamo Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, 
Takukuru na Serikali za Mitaa.
Tunachotaka kusema hapa ni kwamba Serikali 
isibweteke kwa kuondoka wahamiaji haramu 8,000 tu wala kusalimishwa kwa 
bunduki 42. Wamebakia wahamiaji haramu na silaha lukuki. Lazima 
operesheni aliyoitangaza Rais Kikwete ianze sasa kuwanasa wahamiaji 
haramu waliobaki na silaha wanazozitumia kuua na kuteka wananchi.
Tatizo pekee tunaloliona ni kukwamishwa kwa 
operesheni hiyo iwapo itahusisha pia watumishi wa mamlaka hizo hapo juu 
ambao ndio waliosababisha hali hiyo.