Na Patricia Kimelemeta
Posted Jumatano,Septemba18 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Septemba18 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Tunamwomba Rais Kikwete kuingilia kati
operesheni hii kwa sababu inasababisha wananchi wazawa kuingizwa kwenye
mkumbo usiowahusu, jambo ambalo linaweza kusababisha migongano ya hapa
na pale.
Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuwachagua watu wenye utaalamu wa
kuwabaini wahamiaji haramu ili waweze kuwabaini bila ya kunyanyasa
wananchi wazawa.
Akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Wananchi wa
Mkoa wa Kigoma uliofanyika Dar es Salaam jana, Kafulila alisema,
kitendo cha kuwakamata ovyo wananchi wa mkoa huo ambao ni wazawa ni cha
udhalilishaji na kwamba kinapaswa kupingwa kwa nguvu zote.
“Tunamwomba Rais Kikwete kuingilia kati operesheni
hii kwa sababu inasababisha wananchi wazawa kuingizwa kwenye mkumbo
usiowahusu, jambo ambalo linaweza kusababisha migongano ya hapa na
pale,” alisema Kafulila. Aliongeza, utaratibu unaotumika siyo mzuri,
unasababisha malalamiko na mvutano, hivyo aliitaka Serikali kuwatumia
wataalamu wenye ujuzi na mbinu zinazofaa zaidi.
“Zoezi hili mkoani Kigoma linahusisha hadi wazawa,
huku wanaoendesha operesheni hiyo wakiwa hawana utaalamu, jambo
linalosababisha usumbufu, Serikali inapaswa kuangalia utaratibu mpya.”
Mratibu wa umoja huo, Raymond Kulikiza alisema,
hawapingi operesheni hiyo, lakini kitendo cha unyanyasaji kwa wananchi
wa mkoa huo ndicho kinachowafanya walalamikie.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI