Na Rachel Chibwete na Masoud Masasi, Mwananchi
Posted Septemba7 2013 saa 11:38 AM
Posted Septemba7 2013 saa 11:38 AM
Kwa ufupi
Dodoma. Moto mkubwa umezuka jana kwenye Msikiti
wa Manyema uliopo Barabara ya Saba katika Manispaa ya Dodoma na
kusababisha uharibifu mkubwa wa mali pamoja na jengo hilo.
Moto huo ulianza saa 8 mchana baada ya swala ya
Ijumaa hatua ambayo ilileta taharuki kwa waumini waliokuwapo ndani ya
msikiti huo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Juma Mohamed
alisema walianza kuona moshi mzito ukitoka ndani ya jengo la ghorofa ya
pili ya msikiti huo na baadaye moto mkubwa ulizuka.
“Baada ya kuona moto huo, tuliwasiliana na Kikosi
cha Zimamoto ambao walifika katika eneo la tukio na kuuthibiti moto huo
japo kuna uharibifu wa mali uliotokea,” alisema Mohamed.
Shuhuda mwingine Sauda Ally alisema, alikuwa nje
ya duka lake lililopo karibu na msikiti huo na kushuhudia moto mkubwa
ukiwa unawake kwenye ghorofa ya pili ya jengo hilo hali iliyowafanya
kufunga maduka yao.
Mmoja wa maofisa wa polisi aliyefika katika tukio
hilo alisema, bado hawajua chanzo halisi cha moto huo japo kwa taarifa
za awali zinaonyesha kuwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
“Sisi baada ya kupata taarifa hizo tuliwasiliana
na wenzetu wa Kikosi cha Zimamoto na Tanesco kwa ajili ya kuuzima moto
huu,” alisema ofisa huyo. Kaimu Kamanda wa Polisi Suzan Kaganda,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
source: Mwananchi
source: Mwananchi