Na Mwinyi Sadallah
Posted Jumatatu,Septemba9 2013 saa 22:34 PM
Posted Jumatatu,Septemba9 2013 saa 22:34 PM
Kwa ufupi
NI kauli ya Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar, Juma Duni Haji, kuhusu ugonjwa unaomsumbua kiongozi wa Uamsho
Zanzibar. Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni
Haji, amesema hakuna tatizo kwa kiongozi mwandamizi wa Uamsho, Sheikh
Azzan Khalid Hamdan, kutibiwa nje ya nchi kama jopo la madaktari
litapitisha uamuzi huo.
Akizungumza na Mwananchi Ofisini kwake Vuga mjini
Zanzibar juzi, Duni alisema kwa mujibu wa katiba, mwananchi yeyote ana
haki ya kutibiwa nje ya nchi kwa maradhi ambayo tiba yake haipatikani
nchini.
Alisema hata hivyo hatua hiyo itategemea uwezo wa Serikali kifedha na ukubwa wa ugonjwa.
“Bado sijapokea ripoti kuhusu Sheikh Azzan, wajibu
wangu ninapopokea nalazimika kupeleka Hazina, hakuna ombi hata moja
nililowahi kulitupa,”alisema waziri.
Alisema daktari anayemtibu sheikh huyo, anapaswa
kuwasilisha ripoti ya mgonjwa katika Bodi ya Matibabu ya Nje ambayo
ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kulingana na ukubwa wa ugonjwa.
Alisema ingawa Sheikh Azzan ni mshtakiwa, hicho hakiwezi kuwa kigezo cha kukosa kutibiwa nje.
Kiongozi huyo amelazwa katika Hospitali ya Mnazi
Mmmoja mjini Zanzibar akisumbuliwa na maradhi ya figo kuwa na vijiwe na
anapaswa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
Katibu wa hospitali hiyo, Omar Abdallah Ali
alisema kwa utaratibu Bodi ya Matibabu ya Nje inakutana kila baada ya
miezi miwili kufanya uamuzi kuhusu wagonjwa wanaotakiwa kutibiwa nje ya
nchi.
Alipia pia inaweza kukutana kwa dharura pale panapokuwa na mgonjwa anayehitaji uharaka wa matibabu.
Kiongozi huyo wa uamsho anakabiliwa na mashtaka ya kufanya uchochezi na kusababisha uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha.
source: Mwananchi
source: Mwananchi