Kwa ufupi
La Nairobi ni shambulizi la kigaidi la kulaaniwa
vikali na wapenda amani wote ulimwenguni. Hata hivyo, moja ya tafsiri ya
vitendo vya kigaidi tunavyovishuhudia Nairobi ni kuwepo kwa hali ya
vita vya kigaidi vyenye kuendeshwa kwenye maeneo ya mijini (Urban
terrorism).
Ulimwengu umepatwa na mshtuko mkubwa kwa kuona
picha za tukio kubwa la kigaidi kwenye moja ya maduka makubwa jijini
Nairobi. Hili ni shambulio kubwa la kigaidi kupata kutokea Afrika
Mashariki tangu lile la mwaka 1998. Na ajabu ya kihistoria ni kuwa
matukio mengi ya kigaidi yametokea Septemba.
La Nairobi ni shambulizi la kigaidi la kulaaniwa
vikali na wapenda amani wote ulimwenguni. Hata hivyo, moja ya tafsiri ya
vitendo vya kigaidi tunavyovishuhudia Nairobi ni kuwepo kwa hali ya
vita vya kigaidi vyenye kuendeshwa kwenye maeneo ya mijini (Urban
terrorism).
Ni shambulizi lenye athari mbaya kiuchumi si tu
kwa nchi ya Kenya, bali hata majirani zake ikiwemo Tanzania. Ni
shambulizi lililowaogopesha wageni wengi wakiwamo wawekezaji. Kwamba Al
Shabaab inalenga pia nchi za Magharibi. Hivyo basi, hata raia wake.
Kunahitajika jitihada za pamoja kuwaondoa hofu watu wa mataifa ya nje,
kuwa kilichotokea Nairobi kitadhibitiwa kwa njia zote, kisitokee tena.
Na hakika, aina hii ya ugaidi ni ngumu sana
kudhibitika hata kama nchi ina jeshi kubwa na lenye vifaa vya kisasa.
Inahitaji ushiriki wa raia wema katika kutoa taarifa za wahalifu hata
kabla hawajafanya matendo yao maovu. Inahitaji pia maandalizi makini, ya
kuwa na vikosi vilivyo tayari wakati wote kukabiliana na matukio kama
haya.
Jina la kikundi cha kigaidi cha Harakat Al Shaabab
Mujahideen, si jina la Kisomali, bali Kiarabu, na maana hasa ya jina
hilo ni vijana wenye kupigana vita vitakatifu. Hakika Al Shabaab ni moja
ya changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Al Shaabab iliundwa mwaka 2006. Kinasemekana kuwa
na wapiganaji wenye silaha wapatao 10,000. Al Shabaab katika miaka ya
karibuni wamepoteza maeneo mengi ya mijini waliyokuwa wakiyadhibiti,
ikiwamo mji wa Kismayu ambao majeshi ya Kenya yaliudhibiti baada ya
kuwasambaratisha Al Shabaab. Kwa sasa Al Shabaab bado wana nguvu maeneo
ya vijijini katika Somalia.
Kufuatia Kenya kujiingisha kijeshi kupanbana na Al
Shaabab, kikundi hicho kimeifanya Kenya kuwa adui na kutangaza wazi
azma yake ya kuishambulia Kenya. Mwezi Aprili mwaka huu watu watano
walipoteza maisha nchini Kenya baada ya wapiganaji wa Al Shabaab kuingia
kwa nguvu wakiwa na silaha kwenye mgahawa mmoja kwenye mji wa Garissa
nchini Kenya.
Mwaka 2012 ndipo Al Shabaab walipojiunga rasmi na
mtandao wa kigaidi wa Al qaida chini ya kiongozi wa Al qiada, Ayman al-
Zawahiri.
Hakika, hapa duniani matukio ya kigaidi yameongezeka.
Kwa faida ya wasomaji, nitaanza kwa kuangalia
chimbuko la ugaidi kihistoria. Ni rahisi kusema kwamba ulimwengu
umebadilika baada ya ugaidi wa Septemba 11 mwaka 2001 kule Marekani.
Kwamba ugaidi umesogea karibu zaidi katika fikra zetu. Watanzania bado
tunakumbuka tukio la shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Ubalozi wa
Marekani jijini Dar es Salaam, Agosti 7, 1998.
Sura ya ugaidi imeonekana vema zaidi miongoni mwa
walimwengu. Bila shaka, picha ya filamu ya televisheni yenye kuonesha
majengo mawili ya World Trade Centre kule Marekani yakitunguliwa na
kuanguka, zimeonwa na takribani asilimia 75 ya watu wa ulimwengu huu.
Katika hili la kuchambua ugaidi, hebu basi tuanze na kujiuliza;
Ugaidi ni nini?
Itakumbukwa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano walipokutana
Dodoma mwaka 2002 walipitisha Muswada wa Ugaidi. Wabunge wetu walitumia
muda mwingi sana kujadili tafsiri ya neno “ugaidi”.
Kwa kifupi, ugaidi ukitafsiri kutoka neno la
Kiingereza “Terrorism” tunapata maana ya “hofu”. Neno la Kiingereza
“Terror” lina maana ya hali ya “kutisha”.
Vitendo vya kigaidi hutumiwa na mtu au makundi ya
watu ili kuwaingizia watu hofu ndani ya mioyo yao na pengine hata
kuchukua madaraka ya kisiasa. Ugaidi ni njia ya mnyonge na hata mwenye
nguvu kutimiza malengo yake. Hili litafafanulika zaidi kadri
utakapofuatilia maandiko haya.
Kihistoria tunaona kuwa, vitendo vingi vya kigaidi
humu duniani vimefanywa pia na dola zilizo madarakani kwa minajili ya
kuendelea kushika hatamu za dola. Mathalan, msemo wa “ Utawala dhalimu”
kwa tafsiri ya Kiingereza “Terror regime” hutumika tunapoielezea dola
yenye kutumia mabavu na nguvu nyingi kupita kiasi. Dola au mtawala
asiyezingatia sheria wala haki za kibinadamu.
Msamiati huu wa utawala dhalimu unatokana na lugha
ya Kifaransa na una chimbuko la Mapinduzi ya Wananchi kule Ufaransa
kati ya mwaka 1789 hadi 1799. Utawala dhalimu wenye kutisha” la terreur”
ulikuwepo kule Ufaransa kunako miaka ya kati ya 1792 hadi 1794. Katika
kipindi hicho watu takribani 40,000, wengi wao wakiwa wakulima na
wahunzi waliuawa.
Mifano ya tawala dhalimu na za kutisha katika
sehemu nyingine za dunia ni kama Urusi ya zamani chini ya dikteta
Stalin, utawala wa Kinazi wa Ujerumani kati ya mwaka 1933-1945 chini ya
Fashisti Hittler.
Katika Afrika, tuna pia mifano kadhaa ya tawala
dhalimu na za kutisha ambazo kimsingi ni tawala za kigaidi. Uganda ya
Idd Amin, Afrika ya Kati ya Bokassa, Zaire ya Mobutu, na nchi nyingine
nyingi. Hizi zilikuwa tawala dhalimu.
Ugaidi kimsingi ni ile hali ya mtu, kikundi au
dola, kwa maana ya taifa, kutumia nguvu nje ya wigo wa sheria ili
kufikia malengo yao.
Mwenye kuendesha vitendo vya kigaidi huchagua watu wake watakaoathirika na vitendo hivyo.
Si lazima mtu au watu hao watakaoathirika wawe ni
wahusika wa moja kwa moja wa mgogoro husika, isipokuwa, waathirika mara
nyingi huchaguliwa na huonekana kama wawakilishi wa malengo ambayo
magaidi wanataka kuyafikia.
Malengo au sababu za ugaidi zaweza kuwa ni za kidini, kijamii na kisiasa.
Ugaidi huwa wa kimataifa pale tukio la kigaidi
linapofanywa nje ya mipaka ya yule anayatenda tendo la kigaidi, au raia
wa nchi moja wanapokuwa walengwa na kuathirika na tendo la kigaidi
katika nchi ya tatu, mathalan, magaidi kutoka Colombia wanapofanya tendo
la kigaidi dhidi ya raia wa Uingereza katika nchi ya Zambia.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI