Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 21:57 PM
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 21:57 PM
Kwa ufupi
Kauli hiyo ilitolewa jana na kaka wa marehemu, Dk Aziz Mlima
Dar es Salaam. Askari wa Jeshi la Ulinzi la 
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwenye mpango 
wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya 
Congo, DRC, (Monusco), Luteni Rajab Ahmed Mlima, alikuwa katika hatua za
 mwisho za kufunga ndoa.
Askari huyo aliuawa katika uwanja wa mapambano na 
vikosi vya wapiganaji wa Kundi la Waasi la M23, katika Milima ya Gavana,
 karibu na Goma, DRC- Congo wakati akitekeleza jukumu la ulinzi wa amani
Akizungumza na gazeti hili, kaka wa marehemu Dk 
Aziz Mlima, alisema kuwa ndugu yake alikuwa tayari amekamilisha mipango 
yote na kilichokuwa kikisubiriwa ni siku ya kufunga ndoa hiyo.
“ Alikuwa yuko mbioni kufunga ndoa, lakini kwa 
sasa sitapenda kutaja jina la mchumba wake kwa kuwahayupo hapa lakini 
naye ni askari,” alisema Dk Mlima.
Alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili 
nchini leo ukitokea Entebbe, nchini Uganda, ulikopelekwa kwa ajili ya 
uchunguzi wa kitabibu.
“ Utakapowasili utaendelea kuwa nchini ya jeshi na
 baadaye kupewa heshima za mwisho kesho na siku inayofuata yaani 
Alhamisi, tutakuwa na mazishi ya kifamilia” alisema Dk Mlima.
JWTZ yatoa tamko
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Makao Makuu ya 
JWTZ, ilisema askari huyo alipigwa risasi wakati akiwalinda wananchi 
wasidhurike na mapigano kati ya Jeshi la Serikali ya DRC na wapiganaji 
wa Kundi la M23.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema Monusco inajipanga 
kuuleta mwili wa marehemu na wananchi watajulishwa taratibu za mapokezi,
 kuaga mwili na mazishi.
Ofisa huyo anakuwa wa pili wa JWTZ kuuawa katika 
mapigano nchini humo, baada ya hivi karibuni Meja Khatib Shaaban 
Mshindo, kuuawa kwa bomu katika mapigano makali yaliyotokea katika mji 
wa Goma, Agosti 28, mwaka huu.
Julai 13, askari saba wa Tanzania waliokuwa 
wakilinda amani katika mji wa Darfur nchini Sudan, waliokuwa katika 
mpango wa kulinda amani, waliuawa na kikundi cha Janjaweed.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI