Tido Mhando 
            
Posted Jumatatu,Septemba30 2013 saa 10:20 AM
Kwa ufupi
Kwenye makala zake hizi za kila Jumapili, anasimulia
 baadhi tu ya mambo hayo. Wiki jana alianza kuielezea safari yake ya 
kurejea nyumbani Tanzania kutoka Christchurch, New Zealand, alikokuwa 
ameenda kutangaza mashindano ya Michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola ya 
1974, ambapo mwanariadha Mtanzania, Filbert Bayi, aliweka rekodi mpya ya
 dunia. SASA ENDELEA…
Kwa miaka mingi sana Tido Mhando alifanya kazi 
ya utangazaji, hususan wa redio. Kazi iliyokuwa chaguo lake tangu 
utotoni…Katika kipindi hicho kirefu, alishuhudia mengi mno ya kusisimua.
Kwenye makala zake hizi za kila Jumapili, 
anasimulia baadhi tu ya mambo hayo.
Wiki jana alianza kuielezea safari yake ya kurejea nyumbani Tanzania kutoka Christchurch, New Zealand, alikokuwa ameenda kutangaza mashindano ya Michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola ya 1974, ambapo mwanariadha Mtanzania, Filbert Bayi, aliweka rekodi mpya ya dunia. SASA ENDELEA…
Wiki jana alianza kuielezea safari yake ya kurejea nyumbani Tanzania kutoka Christchurch, New Zealand, alikokuwa ameenda kutangaza mashindano ya Michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola ya 1974, ambapo mwanariadha Mtanzania, Filbert Bayi, aliweka rekodi mpya ya dunia. SASA ENDELEA…
Safari ya mkondo wa kwanza ya kutoka Christchurch 
hadi Melbourne, Australia, ilikuwa ya muda wa kama saa tatu hivi. 
Kikundi chote cha Watanzania, wote tukiwa kwenye sare zetu, kilikuwa cha
 watu wenye furaha kubwa mno. Nina hakika kila mmoja wetu alikuwa 
akiwaza kivyake kuhusu itakavyokuwa tutakapowasili kwetu nyumbani.
Tulikuwa tumepangiwa kulala hapo mjini Melbourne 
kwa muda wa saa chache hadi mapema siku ya pili, kwa hiyo safari ilikuwa
 bado ndefu. Hata hivyo, kwa upande wangu nilikuwa nikiwaza kuhusu mambo
 niliyokuwa nimeelezwa na maofisa wa Shirika la Ndege la Qantas juu ya 
fidia ya sanduku langu lililopotea.
Nikiwa ndani ya ndege hiyo kutokea Chrischurch 
nilikuwa nikiwaza: “Je, endapo hawa jamaa watanipiga chenga nitafanya 
nini?” Hii ilikuwa safari yangu ya kwanza ndefu ya kimataifa, kwa hiyo 
sikuwa na uzoefu wa mambo haya. Lakini nikaamua kupiga moyo konde na 
kujisemea kuwa ingebidi tu kuwaamini.
Naam, muda mchache baadaye, rubani wetu 
alitutangazia kujiweka tayari kwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa 
Melbourne, mahali ambapo nilikuwa nimepangiwa kukamilisha hizo taratibu 
za fidia ya sanduku langu ama niseme kwa kweli, kijisanduku changu.
Lazima niwe mkweli maana hadi wakati huo bado 
mambo ya ujana-ujana ndiyo yaliyokuwa yamenitawala. Ingawaje nilikuwa 
mpenzi sana wa kuvaa mavazi ya vijana ya siku zile kama walivyokuwa 
wengine wa rika langu, sikuwa na nguo za kutisha hivyo.
Kwanza, nyingi ya nguo hizo zilikuwa za 
kushonesha, kuanzia suruali hadi mashati ya kubana. Nilikuwa na fundi 
cherahani wangu maalumu pale kwenye Mtaa wa Uhindini maeneo ya Mnazi 
Mmoja ambaye alikuwa ananishonea mavazi yoyote niliyohitaji. Alikuwa 
fundi maarufu wa vijana wa mjini, lakini alikuwa maalumu sana kwangu na 
baadhi ya marafiki zangu wa karibu hasa Robert Mwaimu.
Sasa kwa kweli kwenye kisanduku kile nadhani 
kulikuwa na suruali zisizozidi tano na kama mashati sita hivi, kwisha! 
Sasa kwa vile hawa jamaa wa shirika la ndege walikuwa tayari 
wameshanipatia fedha za kujikimu, niliona kama watakuwa wamenilipa zaidi
 ya kile ninachostahili, lakini ndiyo hivyo - huo ndiyo uliokuwa 
utaratibu na wajibu wao.
Nilikuwa miongoni mwa wasafiri wa mwisho-mwisho 
kushuka pale Melbourne na ghafla chini ya ndege hiyo nikamwona mtu 
aliyekuwa ameshika bango lenye jina langu. Nilimwendea na kujitambulisha
 ya kwamba mimi ndiye Dunstan Mhando (ambalo ndiyo jina langu rasmi).
Alikuwa jamaa mtanashati na mchangamfu sana 
ambaye, mbali na kunisalimia na kunitaka nifuatane naye, alikuwa mcheshi
 wa kutosha, kwani njiani alikuwa akinizungumzisha ingawaje kile 
Kiingereza chake cha Kiaustralia kilinisumbua kiasi.
Hata hivyo, yote kwa yote, alitaka kufahamu zaidi 
kuhusu safari yangu na hasa akapenda kufahamu mengi juu ya Filbert Bayi.
 Ndipo nilipotambua ya kwamba kumbe na yeye alikuwa tayari amezipata 
habari za ushindi wetu.
Hapana shaka, nilijisemea moyoni, huyu jamaa alikuwa amefuatilia
 taarifa za michezo ile iliyomalizika hapo jirani tu na kwao, yaani New 
Zealand na hasa kwa kuwa timu ya Australia ndiyo iliyokuwa imefanya 
vyema zaidi kwenye michezo mingi. Kwa hiyo, bila shaka raia wake 
walikuwa wamefurahia michezo hiyo.
Naam, punde kijana huyo alinielezea hayo kwamba 
raia wa Australia walikuwa kwa siku zote hizo za michezo wakifuatilia 
kwa karibu sana yale yote yaliyokuwa yakifanyika viwanjani na 
wamefurahia ushindi mkubwa na mnono walioupata.
Ndipo nikafahamu ya kwamba kwa kweli michezo ni 
nguzo kubwa ya mshikamano wa kitaifa. Nikawaza wingi wa medali walizozoa
 hawa jamaa wa Australia, ukilinganisha na medali zetu mbili. Lakini 
bado na sisi tulikuwa tukienda kifua mbele na hata wakati huo nilipokuwa
 na ndugu huyu wa Australia nilikuwa bado namtambia.
Mara tukaingia kwenye ofisi moja ndogo kiwanjani 
hapo. Ilikuwa ofisi nadhifu iliyokuwa na maofisa watatu tu, mmoja wao 
ambaye alionekana kama ndiye kiongozi humo, alikuwa ni mwanamama, mkubwa
 kidogo kiumri kuliko wale wengine wawili ikiwa ni pamoja na yule 
mwenyeji wangu.
Huyu ndiye aliyenikaribisha, pia akanipongeza sana
 kwa ushindi wa Filbert Bayi na zaidi, akaniambia kuwa kwa muda mrefu 
yeye na mumewe wamekuwa wakifikiria kwenda Tanzania kupanda Mlima 
Kilimanjaro.
Nilishtuka sana, kwani sikuwa nimefikiri kwamba 
kuna watu ambao wapo maili elfu nyingi namna hii ambao walikuwa wanawaza
 kuja Tanzania kupanda mlima ambao wengi miongoni mwetu wenyewe tulikuwa
 wala hatuujali kiasi hicho. Nilijisikia vibaya!
Kwa hakika, mama huyu alitaka kufahamu mengi zaidi
 kuhusu Tanzania na mlima wake wa Kilimanjaro, nami nilijitahidi kwa 
kiasi changu kumwelewesha na kumwelimisha zaidi na nikamwona kuridhika 
sana na kufurahia kukutana na mimi.
Hatimaye, akanitaka radhi kutokana na upoteaji wa 
‘kasanduku kangu’. Akasema wamejitahidi kila walivyoweza kulitafuta 
lakini wameshindwa. Kwa hiyo, kwa kuzingatia taratibu na sheria za 
safari za ndege tulitakiwa ‘kumalizana’. Kwa hali hii wangenipatia kiasi
 cha Dola 430 kama fidia yao ya mwisho kwangu.
Tayari walikuwa wameandaa nyaraka zote husika kwa 
kukamilisha utaratibu huo, kwa hiyo kile ambacho mimi nilitakiwa kufanya
 kikawa ni kutia sahihi tu. Nilifanya hivyo harakaharaka, maana kwa 
kweli sikuwa nimetegemea hata kidogo kupata kiasi kama hicho cha malipo.
Baada ya kuweka sahihi kwenye karatasi husika, 
wakanipatia kiasi hicho cha fedha na kunitakia kila la heri huku bado 
wakiendelea kuniomba msamaha. Kwa kweli niliwaona kuwa watu wastaarabu 
na waungwana kwelikweli. Baadaye yule kijana alinichukua tena na 
kunipeleka mahali walikokuwa wenzangu.
Walikuwa tayari wamo kwenye basi la kutupeleka 
kwenye hoteli ambayo tungelala hadi mapema siku ya pili tutakapoanza 
safari ya kurejea nyumbani kwa kupitia tena Mauritius. Nilifurahi kwamba
 hoteli tuliyokuwa tumepangiwa ilikuwa katikati ya mji huo wa Melbourne 
maana baada ya kukamata kitita kile cha fedha sasa nilikuwa tayari 
kufanya ‘shopping’ ya nguvu ya nguo na vifaa vingine vya harusi. Nikajua
 kwamba kweli, Mungu ni mkubwa.
Kwa kuwa katika eneo lile la dunia, ule ulikuwa 
wakati wa msimu wa kiangazi basi maduka ya pale nayo yalikuwa yamejaa 
nguo nzuri mno hasa za wanawake zinazoendana na hali ya hewa ya jua la 
nyumbani Tanzania. Nikaamua kuyavamia kikweli kweli.
linunua magauni kadhaa ya mvuto ambayo nilijua yangeweza kumpendeza mchumba wangu wakati wa harusi ambayo kwa wakati huo haikuwa mbali. Siku zilibaki chache sana. Zaidi nilihakikisha kwamba zilikuwa nguo za kupendeza za kipekee kabisa maana hata mchumba mwenyewe alikuwa mtu aliyejali sana mitindo.
SOURCE: MWANACHI linunua magauni kadhaa ya mvuto ambayo nilijua yangeweza kumpendeza mchumba wangu wakati wa harusi ambayo kwa wakati huo haikuwa mbali. Siku zilibaki chache sana. Zaidi nilihakikisha kwamba zilikuwa nguo za kupendeza za kipekee kabisa maana hata mchumba mwenyewe alikuwa mtu aliyejali sana mitindo.
Pamoja na nguo hizo, mimi pia nilijinunulia nguo 
kiasi. Halikadhalika nikanunua vitu vingine muhimu hasa kwa harusi ikiwa
 ni pamoja na viatu na makorokoro mengine ya kutishia tu. Kwa kweli 
mwisho wa yote nilikuwa nimeridhika mno na ununuzi huo.
Sasa kazi kubwa ikawa ni jinsi ya kuvifungasha. 
Kwa kuwa masanduku yetu yote yalikuwa yamehifadhiwa kwa pamoja, 
hatukuruhusiwa kuyachukua wakati tulipoteremka pale Melbourne. Kwa maana
 hiyo, tulikuwa pia haturuhusiwi kuingia na mizigo mingine mikubwa na 
mizito. Sasa mimi ikawa kama vile ndiyo naanza safari nikiwa 
nimefungasha kupindukia.
Nilichokifanya ilikuwa ni kuwakabidhi wachezaji 
mbalimbali baadhi ya vifurushi na wao wakawa wameridhia kabisa. Tulikuwa
 tukisafiri kama familia moja kubwa. Hasa kwa kuwa wote walikuwa 
wanafahamu ya kwamba mara tu nirejeapo nilikuwa nafunga pingu za maisha.
Tuliondoka Melbourne nikiwa mtu mwenye furaha 
kupindukia. Mambo yote yalikuwa yamekwenda vizuri kupita kiasi. Tulikuwa
 tunarejea nyumbani tukiwa washindi; nilikuwa nimefanikiwa kununua vitu 
vizuri na vya thamani kwa ajili ya harusi yangu na nilikuwa 
nimekamilisha kazi yangu vizuri mno. Ilikuwa ni fahari kubwa kwangu. 
Tuliwasili Mji Mkuu wa Mauritius, Port Luis, ikiwa nako ni wakati wa 
mchana kulingana na tofauti ya saa. Baada ya muda si mrefu tuliunganisha
 moja kwa moja na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA) 
kuelekea Dar es Salaam.
Mkondo huu ulikuwa umejaa shauku kubwa na nina 
uhakika siyo kwangu tu bali kwa sisi sote. Mimi nilikuwa nawaza na 
kuwazua jinsi tutavyopokewa tutakapowasili. Kuna nyakati ile hali ya 
hoihoi tuliyokuwa nayo ndani ya ndege ilikuwa inageuka ya utulivu mkubwa
 mno.
Naam, baada ya kama saa nne hivi, ikasikika sauti 
ya rubani ikisema tunakaribia kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es 
Salaam kwa hiyo tujiandae kwa kufunga mikanda. Kiza kilikuwa kimeanza 
kuingia.
Niliketi kimya kwa muda hivi, nikifurahi kurejea 
salama nyumbani lakini nikiwa bado na mawazo mengi. Nilifahamu kwamba 
nikirejea kazini nitakuwa na kazi kubwa ya kujibu maswali mengi ya 
wenzangu na wasikilizaji wangu.
Wakati nikiwaza hivyo, nikaamua kuangalia 
dirishani na kwa mastaajabu makubwa, nikaona nje kulikuwa na halaiki 
kubwa ya watu waliofika uwanjani pale kutupokea. Nikafahamu kwamba 
Watanzania walikuwa wamefurahia ushujaa wetu na hasa wa bingwa wetu mpya
 wa dunia, Filbert Bayi. Machozi yakanilengalenga.