Na Raymond Kaminyoge
Posted Jumanne,Oktoba8 2013 saa 17:45 PM
Posted Jumanne,Oktoba8 2013 saa 17:45 PM
Kwa ufupi
Profesa Lipumba alisema baada ya kuzungumza na Rais kuhusu muswada huo, ndipo watakapotoa uamuzi.
Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimeahirisha maandamano ambayo yalitakiwa kufanyika keshokutwa (Alhamisi).
Vyama hivyo vilipanga kuandamana nchi nzima ili 
kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asisaini muswada wa Sheria ya 
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa una kasoro nyingi
 ikiwamo Zanzibar kutoshirikishwa katika mchakato.
Viongozi wa vyama hivyo wamesitisha uamuzi huo 
baada ya Rais Kikwete kusema yuko tayari kufanya nao mazungumzo kujadili
 suala hilo.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
 hayo Jumanne mara baada ya kukutana na viongozi wenzake katika Ofisi za
 NCCR-Mageuzi, Ilala Dar es Salaam.
Mbele ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na 
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Profesa Lipumba alisema 
viongozi wa vyama hivyo wametafakari na kuona ni busara kumsikiliza Rais
 Kikwete kwanza kabla ya kuamua kuendelea na uamuzi wao au la.
“Lengo la kuandaa maandamano ni kuhakikisha kwamba
 tunapata Katiba bora isiyo na kasoro, ndiyo maana tunaona kwa kuwa Rais
 ameonyesha nia ya kuzungumza na sisi tumeona ni bora tukakutana naye 
kwanza,” alisema.
Profesa Lipumba alisema baada ya kuzungumza na Rais kuhusu muswada huo, ndipo watakapotoa uamuzi.
Alisema bado hawajapata taarifa rasmi kutoka Ikulu
 kuhusu lini watakutana na Rais na kwamba taarifa hizo wamezipata 
kupitia vyombo vya habari.
Jana, vyombo vya habari vilikariri taarifa kutoka 
ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ikisema Rais Kikweta anatarajia 
kukutana na viongozi wa vyama hivyo kati ya Oktoba 13 na 15 mwaka huu.
Rais Kikwete katika hotuba yake ya kila mwezi 
Ijumaa iliyopita, alisema hoja na kauli za wanaopinga muswada huo 
zinazungumzika ili kutafuta mwafaka badala ya kufanya maandamano.
Katika kikao cha Bunge kilichopita, wabunge wa 
vyama hivyo walitoka nje ya ukumbi wakipinga Muswada usijadiliwe kwa 
kuwa una kasoro nyingi.
Miongoni mwa kasoro hizo ni kutoshirikishwa kwa 
Serikali ya Zanzibar, madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge 
maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya 
kuwasilisha rasimu ya pili kwenye Bunge la Muungano badala ya kuwepo 
hadi katika kura ya maoni.
SOURCE: MWANANCHI