Na Mwinyi Sadallah,Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba31 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Oktoba31 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Waziri huyo aliongeza kuwa, mashambulizi haya 
yameleta taswira mbaya kwa Wazanzibari wenyewe na Tanzania kama nchi 
kwani yanailenga jamii moja ambayo siku jamii hiyo ikiishiwa uvumilivu 
taifa linaweza kuingia katika machafuko na kuathiri kwa kiasi kikubwa 
amani, mshikamano wa kitaifa na utulivu visiwani hapa.
Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi
 ya Zanzibar(SMZ), imesema mashambulizi ya kutumia tindikali dhidi ya 
viongozi wa dini na Serikali visiwani hapa ni utekelezaji wa mipango ya 
kisiasa na si sehemu ya chuki za kidini.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya 
Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed wakati wa mahojiano 
maalumu na gazeti hili ofisini kwake eneo la Vugha, Zanzibar jana.
“Mashambulizi haya ya kutumia tindikali yanatokana
 na chuki za kisiasa na kamwe siyo dini kwani Wazanzibar kwa muda mrefu 
wamekuwa na tofauti za kidini lakini hapakuwahi kutokea choko choko na 
mashambulizi kama haya,” alisema waziri huyo.
Akizungumza kwa uchungu amesema, wanaotekeleza 
mashambulizi haya ni watu waovu wenye nia ya kuleta vurugu na kuivunja 
nchi katika vipande na tayari katika hii wanaelekea kufanikiwa kwa 
kuitia doa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Waziri huyo aliongeza kuwa, mashambulizi haya 
yameleta taswira mbaya kwa Wazanzibari wenyewe na Tanzania kama nchi 
kwani yanailenga jamii moja ambayo siku jamii hiyo ikiishiwa uvumilivu 
taifa linaweza kuingia katika machafuko na kuathiri kwa kiasi kikubwa 
amani, mshikamano wa kitaifa na utulivu visiwani hapa.
Amesisitiza hadi sasa tathmini ya awali inaonyesha
 chanzo kikuu ni kuibuka kwa vikundi vya dini vilivyojikita katika mambo
 ya siasa hali inayosambaratisha amani na umoja wa kitaifa uliokuwa 
umeanza kuimarika tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Umoja wa 
Kitaifa Zanzibar Novemba, 2010.
Alisema baadhi ya viongozi wa dini wanaofanya 
kampeni za Zanzibar kujitenga katika Muungano bila ya kuangalia athari 
zake kwa pande zote mbili.
Waziri huyo alionya iwapo Muungano wa Tanzania 
Bara na Zanzibar utavunjika basi wanaotoka visiwani hawatabaki salama 
kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyowahi kuonya siku za 
nyuma. Waziri huyo alibainisha kuwa,faida za Muungano wa Tanganyika na 
Zanzibar ni nyingi kuliko kero zinazolalamikiwa. Alizitaja faida hizo 
kuwa ni pamoja na fursa ya kumiliki ardhi, soko la watu milioni 40 la 
bara, kuishi na kufanya kazi upande wowote.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI