Na Habel Chidawali, Mwananchi
Posted Novemba2 2013 saa 1:12 AM
Posted Novemba2 2013 saa 1:12 AM
Kwa ufupi
Pinda pamoja na mawaziri hao wanatakiwa kuachia
ngazi kama hatua ya kuwajibika kutokana na matukio ya vifo na baadhi ya
watu kujeruhiwa, katika matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa
upande mmoja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa upande
mwingine.
Dodoma. Waziri Mkuu Mizengo
Pinda pamoja na mawaziri wake wawili; Khamisi Kagasheki (Maliasili na
Utalii) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David wameingia
matatani kutokana na shinikizo linalowataka wang’oke katika nafasi zao.
Pinda pamoja na mawaziri hao wanatakiwa kuachia
ngazi kama hatua ya kuwajibika kutokana na matukio ya vifo na baadhi ya
watu kujeruhiwa, katika matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa
upande mmoja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa upande
mwingine.
Jana wabunge walicharuka na kuwataka mawaziri
waliohusika katika Operesheni Tokomeza Ujangili wawajibishwe wakieleza
kutoridhishwa na maelezo waliyoyatoa mapema jana, baada ya kipindi cha
maswali na majibu.
Kelele za wabunge zilizuka baada ya wabunge kuanza
kuchangia maelezo ya Serikali kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima,
hifadhi za wawekezaji na maelezo ya Serikali kuhusu Operesheni Tokomeza
Ujangili.
Aliyekuwa wa kwanza kuchangia mjadala huo ni
Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola (CCM) ambaye katika hitimisho lake
alitoa hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kile
ambacho alikiita kuwa ni unyanyasaji wa wafugaji na uporaji wa mifugo
yao.
Profesa Msola alielekeza shutuma zake kwa Serikali
kuwa ilifanya operesheni zake kwa pupa bila kufanya maandalizi hivyo
kuwaathiri wananchi wasiokuwa na hatia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda kabla ya kuahirisha
kikao cha Bunge jana mchana aliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge
kwa ajili ya kuchunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji, wakati
‘madudu’ ya Operesheni Tokomeza Majangili yatachunguzwa kupitia Kamati
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Chimbuko la hoja
Jana asubuhi kabla ya Bunge kuanza kikao chake,
Spika Makinda alitoa taarifa kwamba Kikao cha Kamati ya Uongozi
kingekutana wakati kipindi cha maswali na majibu kikiendelea, kwa lengo
la kutoa mwelekeo wa mjadala wa hoja za dharura.
Hoja hizo ni zile zilizotolewa na wabunge wawili
kwa nyakati tofauti; Alphaxard Kangi Lugora wa Mwibara (CCM) kuhusu
Operesheni Tokomeza Majangili na Saidi Nkumba wa Sikonge (CCM), kuhusu
vita baina ya wakulima na wafugaji.
Kamati hiyo ilikutana baada ya kipindi cha maswali
na majibu na Spika Makinda alitoa taarifa za kusitisha shughuli
nyingine, ili wabunge waweze kujadili masuala hayo ambako kabla ya
kuanza mjadala aliwaita mawaziri kutoa taarifa zao.'
Alianza Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi
Kagasheki ambaye katika maelezo yake alihitimisha kwa kutangaza
kusitisha Operesheni Tokomeza ili kupitia mpango huo na kufanya
maboresho ili kuondoa upungufu uliopo.
SOURCE: MWANANCHI
Licha ya kueleza sababu nyingi zilizofanya Serikali kuendesha
operesheni hiyo, alisema ina manufaa makubwa katika kuokoa wanyama aina
ya tembo, lakini waziri alihitimisha kwa kusema itakuwa ni busara
kuifanyia tathmini wakati ikiendelea, hivyo kutangaza kuisitisha mara
moja.
Kwa upande wake Dk Mathayo alitoa maneno ya kuomba
radhi na kuwapa pole watu waliopatwa na usumbufu ikiwa ni pamoja na
kupoteza mali zao na mifugo.
Mathayo aliwaeleza wabunge kuwa Serikali imepanga
kujenga malambo katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia
wafugaji kupata maji ili kupunguza safari za kuhamahama kutoka eneo moja
kwenda jingine.
Shinikizo kwa Pinda
Baada ya kumaliza hotuba zao, wabunge kadhaa
walipata nafasi ya kuchangia maelezo hayo huku wengi wakielekeza shutuma
zao kwa mawaziri hao na wenzao wa Mambo ya Ndani ya Nchi na yule wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Wabunge wawili wa Chadema, Paulina Gekul (Viti
Maalumu) na John Shibuda (Maswa Mashariki) walitaka Waziri Mkuu Pinda
ajiuzulu kutokana kushindwa kwake kudhibiti mauaji na mateso kwa
wananchi.
Gekul alisema kinachotokea sasa ni utekelezaji wa
kauli ya Pinda aliyoitoa bungeni akisema wahalifu wapigwe tu pamoja na
ile ya Kagasheki aliyoitoa mjini Arusha akisema majangili watakaokamatwa
wamalizwe hukohuko kwenye hifadhi.
Mbunge huyo alieleza operesheni hiyo kwamba
imesababisha mauaji ya watu wasio na hatia ikiwemo mama Emiliana ambaye
alifuatwa akiuza nyanya, lakini akateswa hadi kufa na hadi sasa mwili
wake bado uko katika Hospitali ya Babati baada ya wananchi kugoma
kuuzika.
Shibuda kwa upande wake alisema Pinda anapaswa
kufungua milango kwa mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu haraka, kutokana na
kulea uzembe ambao umesababisha madhara makubwa kwa wafugaji.
Shibuda alisema kuwa Wizara ya Mifugo imekuwa na
mtazamo hasi lakini akasisitiza kuwa uzembe wa viongozi wa ngazi za
mikoa, wilaya hadi vijiji unatokana na ukimya wa Pinda ambaye anashindwa
kuchukua hatua yoyote dhidi yao.
Wabunge wengine
Kwa upande wake Nkumba aliunga mkono kuundwa kwa
kamati teule, lakini akasisitiza kuwa mawaziri hao wanne wana hoja za
kujibu ndani ya chama tawala CCM na kwa Rais, vinginevyo Serikali
haipaswi kuendeshwa na viongozi wazembe wa aina hiyo.
“Mawaziri mnaosimamia jambo hilo mnayo hoja ya kujibu kwa chama
chenu tena bahati nzuri wote mnatoka CCM, ambao ni Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ninyi wa
Mifugo na Uvuvi pamoja na Maliasili na Utalii, nasema hatuko pamoja na
watu wazembe hata siku moja,” alisema Nkumba.
Mbunge huyo alionya kuwa umefika wakati ambao
Serikali inatakiwa iache tabia ya kuwadanganya wabunge kuwa itapeleka
taarifa bungeni, lakini mambo yakishapoa basi inakaa kimya na akataka
maelezo ya kina majangili wakubwa wako wapi, na kwa nini wasikamatwe na
badala yake kinachofanyika ni kuendelea kuwatesa wasiokuwa na hatia,
kisha akashawishi wabunge wote wazikatae taarifa za mawaziri hao.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alizikataa
taarifa za mawaziri wote wawili kwa madai ya kupikwa na kujaa giliba za
kuwahadaa wananchi.
“Mawaziri hawa wataponea wapi katika mkono huu,
watu wamekufa, wameteswa, mifugo imeporwa na mingine kupigwa risasi wao
wapo tu, nasema wataponea wapi ikiwa ushahidi wote uko hapa,” alisema
Lugola na kuongeza:
“Mawaziri hawa wataponea wapi kama damu ya Dasu
Lutaligula (Kilombero), Madirisha Luchagula (Mulele), Baya Tambi
(Ulanga) wafugaji watano waliokufa huko (Mtimbira- Ulanga ), vilema vya
kudumu Luhende, Ofisa Tarafa (Mpimwe) Diwani wa Maji Moto, wafugaji
watano wa Mtimbira waliopata vilema kutokana na waliyotendewa na
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, hivi wataponea wapi kwa damu za hao?”
Alisema zaidi ya ng’ombe 500 walipigwa risasi
katika mpango wa mradi wa watu wachache wa kutaka kujinufaisha wenyewe
ama kwa kushirikiana na viongozi wa juu.
Aliwatuhumu askari wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), polisi na askari wa wanyamapori, kuwa wamekuwa wakiua
watu ovyo na wengine kubakwa, lakini Serikali inawakingia kifua hali
inayoonyesha kuwa kuna udhaifu ndani ya Serikali.
Katika michango yao, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester
Bulaya (CCM) alisema maelezo yaliyowasilishwa na mawaziri ni mzaha,
huku akiwaonya mawaziri kuacha tabia ya kupuuza hoja za wabunge, kwani
wanapozungumza huwa tayari wamefanya utafiti.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya
(CUF) na Mbunge wa Kuteuliwa James Mbatia (NCCR-Mageuzi), walisema yote
yametokea kutokana na uzembe wa viongozi ikiwemo mawaziri kushindwa
kutimiza wajibu wao.
Hadidu za rejea
Jana jioni Spika wa Bunge, Anne Makinda alimpa
nafasi Profesa Msola, ili aelezee malengo ya kamati teule itakayoundwa
ambapo alisema itakuwa na jukumu la kuchunguza na kuchambua sera
mbalimbali zinazohusu ardhi, kilimo, mifugo, maji, wanyamapori na
uwekezaji ili kubaini kasoro za ardhi, hatimaye kuleta mapendekezo
bungeni yatakayoondoa migogoro ya ardhi inayoendelea kati ya wakulima,
wafugaji, hifadhi, uwekezaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Alizitaja hadidu za rejea za kamati teule kuwa ni
kuchambua sera mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi kubainisha
kasoro zilizopo katika sera hizo, kuchunguza mikakati iliyowekwa na
Serikali, kuchambua mikakati yote ya Serikali ya kusuluhisha migogoro ya
wakulima na wafugaji.
Nyingine ni kuchambua mikakati ya kulinda vyanzo vya maji,
uharibifu wa mazingira na kutoa mapendekezo yatakayoondoa migogoro yote
kudumisha uhusiano mzuri na utengamano na mambo mengine ambayo kamati
itaona yanafaa.
Akiboresha hadidu za rejea Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika (Chadema), alisema ni vyema kamati teule hiyo ikapitia ripoti
mbalimbali tume na kamati zilizoundwa kuchunguza suala ya matumizi ya
ardhi ikiwemo ya Profesa Shivji.
Alisema kuwa kumekuwa na kawaida ya kuunda tume ambazo zimekuwa ni siri na utekelezaji wake hakuna.
Mnyika alisema kuwa ni vyema katika kuongeza hadidu za rejea ya kushughulikia uwajibikaji pale ambapo kuna kasoro za utendaji.
Mbunge wa Tunduru Abdallah Mtutura (CCM), alisema
wapo watu ambao wameuawa kwa kisingizio kuwa ni majangili huku wengine
wakijificha maporini kuogopa operesheni hiyo.
Aliunga mkono kuongezwa kwa hadidu ya kuchunguza mauaji na watu walioteswa katika operesheni hiyo.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM), alitaka
kuwepo kwa muda maalumu wa kamati teule kufanya kazi kwa kuwa jambo
hilo ni zito.
Alisema kumekuwa na tume nyingi ambazo
hazijaonyesha matokeo yake na kutaka kamati hiyo itakayoundwa iwe ya
mwisho katika utekelezaji.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali (NCCR-
Mageuzi), alisema operesheni hiyo imefanya zaidi ya ugaidi na unyama na
kuomba waliohusika na mauaji na utesaji wa watu kupimwa akili.
Kwa upande wake Mbunge wa Mkanyageni, Habib
Mohamed Mnyaa, (CUF), alitaka kuwepo kwa fidia kwa watu walioathirika na
operesheni hiyo.
Akihitimisha hoja hiyo, Profesa Msola alisema
mapendekezo yote yataingizwa katika hadidu za rejea ili yasaidie katika
utendaji wa kamati hiyo teule.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema majina ya wabunge watakaounda kamati hiyo, yatatajwa Jumatatu ijayo.
SOURCE: MWANANCHI