Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba31 2013 saa 12:51 PM
Posted Alhamisi,Oktoba31 2013 saa 12:51 PM
Kwa ufupi
Siku ya kuoana na hata kabla, kuna ahadi ambazo watu
hao hupeana;hasa zinahusiana na kuheshimiana na kufanya mambo yenye
lengo la kuonyesha upendo wa dhati na kuimarisha ndoa yao na familia kwa
ujumla.
Japo wengine wanaweza kuwa na maana tofauti,
ndoa inafahamika kuwa ni muungano baina ya watu wa jinsi tofauti yaani
mwanaume na mwanamke.Kwa Wakristo ndoa inapaswa kuwa ya mke mmoja na
mume mmoja, wakati kwa Waislamu, mume anaruhusiwa kuoa zaidi ya mke
mmoja.
Siku ya kuoana na hata kabla, kuna ahadi ambazo
watu hao hupeana;hasa zinahusiana na kuheshimiana na kufanya mambo yenye
lengo la kuonyesha upendo wa dhati na kuimarisha ndoa yao na familia
kwa ujumla.
Hata hivyo hapa nchini kama ilivyo katika nchi
mbalimbali za nje, kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wanandoa
kutoheshimu viapo walivyopeana siku wanafunga ndoa.
Baadhi ya wasomi maarufu katika masuala ya ndoa,
Kertzer, David I na Marzio Barbagli (2001) wanasema katika utafiti wao
walioupa jina la the history of the European family yaani historia ya
familia Ulaya, uliochapishwa na Chuo Kikuu Yale, Marekani kuwa ndoa
njema ni ile ambayo watu wake wanajali kwa vitendo ahadi walizopeana za
kuishi vizuri. Kwa bahati mbaya kuna watu wanaingia kwenye ndoa wakiwa
wanaelewa vizuri, baada ya kuanza kuwa umaarufu au kuwa na fedha, ndoa
zao hugeuka na kuanza kuwa mbaya.
Badala ya fedha kuwa sehemu ya kusaidia maisha yaweze kuwa bora,zinaonekana kuchangia kuwa na ndoa zilizokithiri migogoro.
Wengi huanza kurudi usiku wa manani au hata kulala nje kwa visingizio vya wingi wa kazi au hata safari feki za kazi.
Watafiti Evans, Tanya (2005) katika chapisho
walilolipa jina la Women, Marriage and the Family yaani wanawake ndoa na
familia wanasema kutoheshimu ndoa kunasababisha baadhi ya watu
kushindwa kuwa na maisha bora kwa sababu ya kutumia fedha nyingi bila
sababu za maana.
“Wengine nje ya ndoa wana zaidi ya wanaume au
wanawake mmoja, hii yote ni kuonyesha namna gani si bora, kwani walio
bora hujua namna ya kuvifanya hata visivyo vizuri view vizuri” inasema
sehemu ya utafiti wa wasomi hao ikizingumzia tabia za baadhi ya watu wa
kada mbalimbali.
Hivi karibuni, Rais Robert Mugabe aliwaonya
mawaziri wake dhidi ya `nyumba ndogo’ akisema baadhi ya mawaziri
wanatumia mali zao nyingi kuwa katika uhusiano wa kimapenzi wa wanawake
wasio wake zao.
Kuna viongozi wameoa wake wengine na kuachana na
wale wa awali bila sababu za maana, huku watoto wao wakiwa na maisha
duni. Kinachoonekana ni kama wake wengi wa viongozi na watu wenye fedha,
wanaishi kwenye ndoa kwa kuvumilia, siyo kwa furaha; wengi kwa nje
wanaonekana wana furaha, ndani ni shida.
Wengine hawajawahi kupanda gari pamoja na waume
zao kwenda kwenye matembezi, na hata wanapotaka ukaribu huambiwa kwani
shida ni nini kama kula si unakula…watu hawaingii kwenye ndoa kufuata
kula, bali uhusiano mzuri wenye amani, wanasema watafiti Berstein na
Nina (2007) katika utafiti wao walioupa jina la “Polygamy, Practiced in
Secrecy” yaani katika maana isiyo rasmi ndoa za wake wengi
zinavyoendesha kwa kificho.
Maoni ya watafiti
Watafiti hawa wanasema wengi wanasema wameoa mke mmoja, ingawa
katika uhalisia wana zaidi, kwa kuwa wengine huko nje hutoa huduma zote
kama mke. Wengine ambao pia ndoa zao zinawaka moto ni viongozi wa dini,
ni mojawapo ya dalili za kujua hilo ni kuangalia kama ni watu wanaoweza
kutembea pamoja au la.
Mara nyingi ukiona wanandoa hawatembei pamoja hasa
nyakati za mwisho wa wiki au sikukuu, kama hakuna sababu labda za
ugonjwa, mwingiliano wa kazi au zinazofanana na hizo, yaweza kuwa ni
ishara kuwa ndoa yao ni mbaya, tayari mmoja ana mwingine nje, hivyo
hajali tena kuwa karibu na mwenza wake wa ndoa.
Kauli ya Mugabe huenda ikawa ni muhimu kujadiliwa
na jamii zote duniani kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na hisia
zinazofanana na Mugabe katika nchi nyingi.
Mugabe alitoa kauli hiyo kwenye harusi ya mpwa
wake.Huku akiwasihi wanandoa kuwa waaminifu katika ndoa zao, Mugabe
alionya dhidi ya kile alichokitaja kama tabia ya wanaume kuwa na `nyumba
ndogo’ akisema kuwa mawaziri wake aliowatarajia kuwa watu wenye maadili
mema, pia walikuwa na tabia ya uasherati.
Kwa mujibu wa jarida la New Zimbabwe, Mugabe
anasema kuwa, “mali ambayo baadhi ya mawaziri wanayo ndiyo chanzo cha
matatizo kwenye ndoa.
Anasema nyumba ndogo siyo jambo jema na
anasisitiza kuwa anajua kuwa mawaziri wake wote wana tabia ya uasherati
ambalo siyo jambo jema katika jamii.
“Nawasihi muachane na tabia hiyo. Mwammume mmoja
na mke mmoja bila shaka itafanikisha ndoa zenu,” anasema Mugabe
akimaanisha watu kuheshimu ndoa zao.
Hoja ya Mugabe
Rais huyo anasema “Wanawake lazima wapigane dhidi ya tabia hii”.
Anasisitiza kuwa usawa wa kijinsi haupaswi
kumaanisha kutupilia mbali tamaduni na maadili. Mugabe anasema tabia
hiyo ya ngono ndiyo inayochangia kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi kwani
anawafahamu mawaziri wengi wanaougua ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, neno ndoa ni makubaliano rasmi ya
mwanamke na mwanamume ya kuishi pamoja kama mke na mume. Ingawa neno
`nyumba ndogo’ bado halijawekwa rasmi kwenye Kamusi za Kiswahili lakini
likitumiwa linaeleweka vizuri katika jamii.
Linaeleweka vizuri kwa sababu suala la mwanamume
kuwa na nyumba ndogo ni la kawaida sana hapa nchini ndiyo maana hata
msamiati huo unaeleweka vizuri.
SOURCE: MWANANCHI
Dini zote zinakataza watu kuwa mahusiano ya kimapenzi bila ya
kuwa na ndoa. Kwa Wakristo kuna amri ya sita ambayo inakataza kuzini
wakati Waislam dini hiyo inakataza hata kuikaribia zinaa.
Kwa hiyo mwanamume anapokuwa na nyumba ndogo ni dhahiri kuwa anavunja amri ya sita kwa kuzini ama kufanya zinaa.
Ingawa Mugabe ameweka wazi kwamba katika nchi yake
kuna mawaziri wenye nyumba ndogo kwa maana ya kwamba wanaozini ni
lazima tujiulize hali ikoje hapa nchini Tanzania? Kiongozi anapokosa
uaminifu kwenye ndoa itakuwa vigumu kuwa muaminifu kwenye taasisi
anayoiongoza. Viongozi ndiyo wanatakiwa kuwa waaminifu katika jamii ili
wananchi waweze kuiga matendo mema unayoyafanya, wanasema watafiti
Berdahl, J. L., & Anderson, C. (2005) katika utafiti wao walioupa
jina la Men, women, and leadership yaani wanaume, wanawake na uongozi.
Wasomi hao wanasema ingawa viongozi wa dini
wamekuwa mstari wa mbele kukemea watu wasijihusishe na nyumba ndogo kwa
sababu huathiri ndoa zao, watu wanajiita kwa majina ya dini mbalimbali
wamekuwa hawajali mafundisho ya dini zao.
Katibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wa
zamani, Blandina Nyoni aliwahi kusema watu wengi wamekuwa si waaminifu
katika ndoa zao na kwamba hilo ndilo tatizo la kuendelea kuenea kwa
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Wanakufa kwa Ukimwi ndani ya ndoa
Katika utafiti uliofanywa mwaka 2007 hadi 2008 na
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa
Kupambana na Ukimwi (NACP), unaonyesha asilimia 6.6 ya wanawake walio
katika ndoa wameathiriwa na virusi vya Ukimwi wakati wanaume ni asilimia
4.6.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania KKKT, Amin Sandewa ambaye anaishi na virusi vya Ukimwi, aliwahi
kusema kwamba baadhi viongozi wa Serikali na wale wa kidini walio
katika ndoa wanashiriki vitendo vya uasherati.
Mchungaji Sandewa anasema viongozi unawakuta
wanakemea vitendo vya uasherati wakati wenyewe wanashiriki vitendo
hivyo, tena baadhi ya viongozi hao wenye ndoa chafu ni wale ambao
ukiambiwa huwezi kuamini kwa namna walivyo na hadhi katika jamii.
“Viongozi wenye ndoa ni lazima tubadilike, nyumba ndogo hazitatusaidi,
zaidi ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kuwa katika hali
mbaya kiuchumi, maana kuwa na nyumba ndogo ni gharama,” alisema Sandewa.
Kama wewe uko kwenye ndoa, pata muda wa
kujitathimini…je, hali ya ndoa yako ikoje? Je, unafanya mambo ambayo
ungependa mwenza wako akufanyie? Jibu unalo. Wapo wengine wamekataa hata
kuwasomesha watoto wao kwa sababu wamegombana na wake zao, watoto wana
kosa gani? Inaendelea Kesho
SOURCE: MWANANCHI