Friday, 1 November 2013

wengine wagoma kutiwa nguvuni


Na Waandishi wetu, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Novemba1  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Baada ya kukamatwa kwa madiwani hao juzi, jana kikosi hicho kilikwenda kufanya upekuzi katika nyumba zao.


Serengeti na Arusha. Jitihada za Kikosi Maalumu cha Kuzuia Ujangili, kuwakamata polisi wa Loliondo, ili kuunganishwa na madiwani watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro akiwemo mwenyekiti wao, juzi zilikwama.
Kukwama huko kulitokana na kuibuka kwa malumbano katika Kituo cha Polisi cha Loliondo.
Katika tukio hilo, risasi kadhaa zilipigwa hewani .
Hata hivyo, baada ya kushindwa kukamatwa kwa polisi hao (majina yanahifadhiwa) na askari wa kikosi kurejea kambini, maofisa wa juu wa operesheni, waliagiza kuwa, polisi wanaotuhumiwa wawekwe rumande taratibu za kipolisi zitakapokamilika.
“Tuna orodha ya baadhi polisi kuhusika na mtandao wa ujangili, tutawafuata tena na kuwahoji,”alisema ofisa mmoja
Madiwani na mwenyekiti wa kijiji mbaroni.
Baada ya kukamatwa kwa madiwani hao juzi, jana kikosi hicho kilikwenda kufanya upekuzi katika nyumba zao.
Habari kutoka katika Wilaya za Ngorongoro zilisema madiwani hao walikamatwa wakiwa katika semina ya hali ya hewa iliyokuwa inafanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kwa mujibu wa habari hizo madiwani hao wote ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alipoombwa kuzungumzia kukamatwa kwa madiwani hao, Diwani wa Kata ya Enduleni, James Moringe, alisema huenda wanashikiliwa kwa mahojiano kwamba ana imani kuwa wataachiwa.
Wakati huohuo, Serikali imeshauriwa kuzifanyia marekebisho sheria ya ujangili.
Rai hiyo inatokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kukosekana kwa meno makali katika sheria hiyo hasa dhidi ya watu wanaokamatwa wakiwa na nyara za Serikali.


Imeelezwa kuwa hali hiyo inachangia katika ongezeko la matukio ya kuuawa kwa wanayamapori nchini.
Ushauri huo, ulitolewa juzi na Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori cha Kenya, Prof esa George Owiti, alipokuwa akitoa mada kwenye kongamano la kimataifa linalohusisha nchi zaidi ya 20 duniani.
Katika mkutano huo unaofanyika mkoani Kilimanjaro, Profesa Owiti alisema sheria hizo hazina makali kwa wahalifu.
“Ni vyema Tanzania ikaweka utaratibu wa kutumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa wahalifu wa wanyamapori katika hifadhi kwa kuchukuliwa sampuli za wahalifu,” alisema Owiti.
SOURCE: MWANANCHI