Sunday, 11 March 2007

ADA YA UANACHAMA




Napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha rasmi ,kuanza kuwakilisha fees za tasao ,kama tulivyokubaliana katika kikao cha tarehe 24/ 02 / 07 ,na zilikuwa kama ifuatavyo;


(i) Ada ya kuingilia uanachamaHii ni ada itakayokupa uhalali wa kuwa mwanachama wa TASAOKikao kilipitisha NOK 100/=(ii) Ada ya kila semisterKikao kiliona kuwa ili kuepusha michango ya mara kwa mara ni vema kuwa na mchango wa kila semester. Kwa pamoja walikubali kuchanga NOK 200 kwa kila semister.

Hivyo basi kila mwanachama ,anaombwa kuwasilisha kiasi cha 300NOK
Ingekuwa ni vyema tuharakishe michango hii ,kama mnavyofahamu Graduation ni mwisho wa mwezi ujao ,Tungependa kufahamu mapema ,kiasi che fedha ili tujue kama kuna haja ya kuchangia Graduation au la.

Naomba ada hizo ziwakilishwe ,anwani hii Block 10 ,H0106 napatikana kuanzia saa moja jioni na kuendelea jumatatu mpaka jumapili.

Au waweza wasiliana na kiongozi yeyote aliye karibu nawe kwa kurahisiha zoezi hili hakikisha unapata taarifa za mawasilisho ya mchango wako kwa mhazini.

Asante sana Kwa ushirikiano wenu ,

Beatrice Chinguwile,
Mweka Hazina .
TASAO - (PAMOJA DAIMA)

Friday, 2 March 2007

HONGERA TASAO KWA KUFANYA UCHAGUZI WA KWANZA 24. 02. 2007

Hawa ndio viongozi wetu jamani!!!!

Salamu na Hoja za Wana - TASAO kwa Mh. Rais J.M. Kikwete, 28.02.2007

Mheshimiwa Rais,

Hapa Norway na hususani Oslo, kuna wanafunzi watanzania wanaosoma katika vyuo mbalimbali. Wanafunzi hawa wanaunganishwa kwa pamoja katika Umoja wao unaojulikana kama TASAO – Tanzanian Students Association – Oslo. Umoja huu umeanzishwa january, 6 mwaka huu, kwa malengo ya kuwaunganisha, kusaidiana kwa hali na mali pia kuhamasishana katika kutimiza na kufikia malengo ya kishule yaliyotuleta huku kama wanafunzi.

Baada ya hayo mheshimiwa Rais, wanafunzi walikuwa na haya ya kusema kuhusu yanayojiri kwa ndugu zetu, wadogo zetu, kaka na dada zetu huko nyumbani Tanzania:


1. Suala la kuchangia elimu ya juu:
Kwa pamoja tunaungana na serikali katika suala hili. Tunaomba serikali iwe makini haswa katika suala la nani anastahili kupata mkopo.. Hata hivyo tuna mapendekezo yafuatayo;
i. Twaiomba serikali itoe mkopo kwa 100% kwa kila mwanafunzi aliyefaulu na ana sifa za kujiunga na chuo.
ii. Wazazi na wanafunzi waelimishwe juu ya suala hili ili kuepusha migongano
iii. Iwekwe mikakati thabiti ya kufuatilia urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa ili iweze kuwasaidia na wengine
iv. Kuna haja ya kupitia mara kwa mara viwango vya posho na mikopo ili kukidhi tatizo la viwango vidogo vya bei za soko.

2. Kuhusu mazingira ya kusomea:
Pamoja na nia nzuri ya serikali katika kuongeza idadi ya vyuo na wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu, serikali pia izingatie;
i. Uwiano wa miundombinu na idadi ya wanafunzi
ii. Ihamasishe wawekezaji kuwekeza kwa kujenga hosteli kwa ajili ya malazi ya wanafunzi ndani ya maeneno ya vyuo.
iii. Ukubwa wa darasa (number of student) iendane na idadi ya walimu kwa baadhi ya vitivo
iv. Uboreshaji wa usafiri kwa wanafunzi wanaoshi nje ya vyuo (kampasi)
v. Uwezo wa vyuo kumudu mahitaji ya ufundishaji yanayohusiana na programu zilizoongezwa

3. Elimu kazini
Sambamba na nia nzuri ya serikali kuendeleza viwango vya elimu kwa watumishi wake, yapo matatizo ambayo yanarudisha nyuma nia nzuri ya serikali yetu. Kama yafuatayo:
i. Baadhi ya watumishi kuzuiwa kwenda masomoni hata pale wanapokuwa na ufadhili binafsi
ii. Kutotambulika kazini pindi wamalizapo masomo yao na kutakiwa kuomba kazi hizo upya
iii. Kutokuinuliwa kwa vyeo ama kupandishwa kwa madaraja ya utumishi ya watumishi kulingana na viwango vyao vya elimu walivyojiendeleza


4. Utafiti
Ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia tunapendekeza serikali kuzingatia yafuatayo;
i. Iwekeze kwenye tafiti za msingi kwa maendeleo ya nchi
ii. Ithamini na kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali zilizokwisha fanyika kwa ajili ya nchi yetu

Mwisho twasema ahsante kwa kututembelea na twakuomba kama wanafunzi tufikishie salamu zetu kwa mfalme na serikali ya Norway kwa ufadhili wao kwetu katika masomo. Twawaomba wasichoke kutusaidia. Pia tusalimie wa-Tanzania wenzetu walioko huko nyumbani pindi utakapo rejea. Karibu tena - Norway.

Ni sisi wanafunzi wa Tanzania hapa Oslo - Norway

Imesomwa na Rais wa TASAO,

JOHN, Chalukulu

Taarifa ya kikao cha TASAO tarehe 24.02.07

1. Kikao kilifanyika

Tarehe: 24-02-07
Mahali: Chuo kikuu cha Sayansi ya michezo na elimu ya viungo-Norway (NIH) -Songsvann

2. Kufunguliwa kwa kikao
Kikao kilifunguliwa rasmi na aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa TASAO.


3. Kusomwa kwa taarifa ya kikao kilicho pita.
Katibu alisoma taarifa ya kikao kilicho tangulia cha tarehe 03-02-07.
Wanachama walikubaliana na taarifa hiyo.

4 Yatokanayo na kikao kilichopita.
Kikao kilichopita kilidhamiria pamoja na agenda nyigine, kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba. Hivyo kilipendeleza tarehe 24-02-07 kuwa ndiyo situ ya ya uchaguzi mkuu wa TASAO.

5. Zifuatazo ndiyo zilikuwa agenda za mkutano
(i) Mahafali ya kuwaaga wanaomaliza
(ii) Ada ya uanachama
(iii) Ujio wa Rais Kikwete
(iv) Uhusiano wa TASAO na vyama vingine Norway
(v)Uchaguzi wa viongozi
(vi) Mengineyo

6. Mahafali ya kuwaaga wanaomaliza

Kikao kwa pamoja kilikubali kuwepo na mahafali ya kuwaaga wanaomaliza. Ili kuweza kuwaaga wote wanaomaliza kwa pamoja, wajumbe walipendekeza kufanya sherehe mapema. Kwa kuwa wanafunzi wanapishana muda wa kumaliza, ilionekana ni vema tufanye sherehe mwezi wa nne(April) na iwe situ ya ijumaa ili kuruhusu wajumbe kushiriki. Tarehe rasmi itatangazwa baadae.

7. Ada ya uanachama
Kikao kilitangaza rasmi kuwa kutakuwa na ada za aina mbili
(i) Ada ya kuingilia uanachama
Hii ni ada itakayokupa uhalali wa kuwa mwanachama wa TASAO
Kikao kilipitisha NOK 100/=
(ii) Ada ya kila semister
Kikao kiliona kuwa ili kuepusha michango ya mara kwa mara ni vema kuwa na mchango wa kila semester. Kwa pamoja walikubali kuchanga NOK200 kwa kila semister.
ANGALIZO:
Wajumbe walipendekeza kuwa ni vema matumizi na mapato ya TASAO yawekwe wazi kwa kila mwanachama.



8. Ujio wa Rais wa Tanzania.
Wajumbe kwa pamoja walijadili kuhusu ujio wa Rais Kikwete nchini Norway. Wajumbe kwa pamoja waliona kuna haja ya kuwa na risala yao kama wanafunzi kwa mheshimiwa Rais. Waliona kuwa risala yao igusie masuala ya wanafunzi wakiwa masomoni nje ya nchi na ndugu zao walio kule nyumbani Tanzania. Kwa hali hiyo, waliona kuna haja ya kuunda kamati ili kuweza kuandika risala yao kwa kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wanafunzi. Kikao kilichagua wajumbe wawili. Wajumbe hao wataungana na Rais, Katibu na Makamu wa Rais watakaochaguliwa hapo baadae. Hivyo kamati ya kuandika risala ilikuwa na watu watano.

Wajumbe wafuatao walichaguliwa na mkutano
(i) Hafsa, Waziri
(ii) Robert, Ngukah

9. Uhusiano wa TASAO na vyama vingine vya Kitanzania hapa Norway
Mkutano uliona kuwa TASAO ni chama kipia na wengi hawajakifahamu. Kuna haja ya kukitangaza chama na watu waelewe malengo ya chama. Moja ya jambo alilosisitiza mwenyekiti ni kuwa lengo la TASAO ni kuendaleza ushirikiano na vyama vingine. TASAO pia iliona kuwa kuna haja ya kupanua ushirikiano na kuheshimu vyama vingine hasa vya Kitanzania hapa Oslo na Norway kwa ujumla

10. Uchaguzi wa viongozi
Ili kuweza kuendesha zoezi la uchaguzi, Kamati ya uchaguzi iliundwa. Wafuatao walichaguliwa
(i) Juma Lungo (M/kiti)
(ii)Kisa Mwakatobe (katibu)
(iii)Jacob Mwangomola (mjumbe)

Mara baada ya uchaguzi wa kamati ya uchaguzi, viongozi wa muda walivuliwa madaraka na zoezi la uchaguzi likaanza.

11. Matokeo ya uchaguzi
NO. Nafasi Jina
1 Rais wa TASAO John Chalukulu
2 Makamu wa Rais Blakson Kanukisya
3 Katibu TASAO Alice Makule
4 Mtunza Fedha Beatrice Chingumile
5 Academi&recreation i)Hezron Nonga ii)Inocent Buberwa
6 Heath Zawadi Kinyamagoha
7 Wajumbe kamati ya fedha Faraja Ingira, Mary Wariro
8 Wajumbe Amir Makame, Linda lugenge

12. Mengineyo
Rais aliwashukuru wanachama kwa kuwa na imani nae na alisisitiza ushirikiano kwa wana-TASAO

13. Kufunga kikao
Kikao kiliahirishwa hadi kitakapo tangazwa tena saa 11:32