Kwa ufupi
Asema idadi inayodahiliwa ni ndogo, ikilinganishwa na nchi jirani.
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amevitaka
vyuo vikuu nchini kuweka nguvu zaidi, kuhakikisha vinadahili wanafunzi
wa shahada za juu ili kupata wahadhiri.
Akizungumza baada ya kutoa hati idhini kwa Vyuo
Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vinane, Rais Kikwete alisema kufanya hivyo
vitakabiliana na tatizo la uhaba wa wahadhiri linalovikabili hivi sasa.
“Pale kwenye upungufu tusisite kutafuta wataalamu
wengine kutoka nje ya nchi. Wakati wa miaka ya 1970 tulipokuwa tunasoma
pale Chuo Kikuu (Mlimani), tulikuwa na wahadhiri wengi kutoka nje,”
alisema Rais Kikwete.
Licha ya suala hilo, Rais Kikwete alisisitiza umuhimu wa vyuo hivyo kuwekeza kwenye utoaji elimu bora.
“Ikumbukwe idadi kubwa ya wanafunzi haitoshi,
lazima tuzingatie ubora. Tunataka mwanafunzi anayepata shahada nchini
ajulikane popote anapokwenda,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Isiwe shahada ya kibongobongo, akifika nje anaonekana kama ana stashahada.”
Pia, alisema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa wanafunzi wa kutosha kujiunga na vyuo vikuu.
Alisema nafasi za vyuo vikuu kwa mwaka ni zaidi ya
78,000, lakini wanaopatikana ni 43,000, changamoto ambayo lazima
wakabiliane nayo.
Alisema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo
vikuu nchini ni ndogo, ikilinganishwa na wanaojiunga na taasisi hizo kwa
nchi nyingine.
Rais Kikwete aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi kuhakikisha inatekeleza kwa ufanisi, mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa ( Big Result Now). Alivitaka vyuo hivyo kuhakikisha vinajitafutia
njia nyingine za mapato, badala ya kusubiri karo.
Vyuo vilivyopata Hati Idhini ni Chuo Kikuu cha
Tumaini Makumira (Tuma), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania
(Saut) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco). Vingine ni Chuo Kikuu
cha Mount Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Arusha (UOA), Chuo Kikuu Kishiriki
cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela
ya Sayansi na Teknolojia, Arusha (NM-AIST) na Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia Mbeya (Must).
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper