Thursday, 29 August 2013

Wabunge watuhumiwa kwa biashara dawa za kulevya


Na Boniface Luhanga, 28th August 2013
Yaelezwa majina yao yakitajwa hatapona mtu
                                 
                            Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Sakata la biashara ya dawa za kulevya sasa limechukua sura mpya baada ya jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kulieleza Bunge kuwa iwapo serikali itaamua kuwataja vigogo wa biashara hiyo nchini kama inavyopewa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, hakuna atakayepona kwani miongoni mwao wamo wabunge wengi.

“Kama serikali ikiamua kuwataja kwa majina wahusika wa dawa za kulevya bila kufanya upelelezi wa kina kwanza, hakuna atakayepona maana miongoni mwao mmo na ninyi humu ndani (wabunge na mawaziri),” alisema Lukuvi.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Lukuvi ilipokewa na baadhi ya wabunge kwa kumzomea kiasi cha kumfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuingilia kati kwa kuwataka waache kufanya hivyo na badala yake wamsikilize kwa makini.

Lukuvi alitoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya nyongeza ya wabunge watatu walioitaka serikali kutaja kwa majina ya vigogo waliohusika na usafirishaji wa dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Dawa hizo zilikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo eneo la Kempton Park,  Afrika Kusini.

Dawa hizo kilo 150 aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 zilikamatwa Julai 5, mwaka huu zikidaiwa kubebwa na wasichana wawili raia wa Tanzania. Waliokamatwa ni Agnes Gerald (25) na Melisa Edward (24).

Wabunge walioibana serikali na kuitaka iwataje vigogo hao walioshirikiana na baadhi ya watumishi wa JNIA ambao tayari wamepoteza ajira zao ni Catherine Magige (Viti Maalum-CCM), Anne-Kilango Malecela (CCM-Same Mashariki) na Mchungaji Israel Natse (Chadema-Karatu).

Maige na Kilango walitaka vigogo waliowatumia watumishi hao wa JNIA kupitisha dawa hizo za kulevya, watajwe ndani ya Bunge.

Kwa upande wake, Mchungaji Natse, alisema hata Rais Jakaya Kikwete, anasema majina ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya anayo lakini serikali haiwataji.

“Inasikitisha kuona kwamba serikali inahangaika kutibu badala ya kuzuia inawataja inaowakamata, lakini haiwataji wanaowatuma,” alisema Mchungaji Natse.

Akijibu maswali ya wabunge hao, Lukuvi alisema: “Ni kweli hivi karibuni kuna watumishi walifanyiwa upelelezi wakishukiwa kwamba wamehusika kuwezesha dawa za kulevya kupita katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.

Mamlaka zinazohusika zimechukua hatua sasa mamlaka nyingine zinazohusika na sheria zinaendelea na upelelezi kamili ili kujua hao waliowatuma na kujua jinsi walivyojihusisha ili wafikishwe mahakamani washtakiwe.”

Aliongeza: “Kwa sasa siwezi kusema ni nani aliwatuma kwa sababu upelelezi unaendelea ili hao waliowatuma wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”

Lukuvi alisema watu hao wanaweza kutajwa hata kabla Bunge halijakutana tena na wakafikishwa mahakamani na watasomwa kwenye vyombo vya habari.

Alisema kama serikali inayo majina ya watu hao haitasita kuwataja kwa sababu ni watu hatari sana katika taifa.

Hata hivyo, Lukuvi alisisitiza kuwa kazi ya serikali siyo kutaja majina ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, bali ni kuwachukulia hatua na haiwezi kuwachukulia hatua bila kuwa na uhakika. “Orodha hizi tukiwaonyesha tutakwisha maana na humu ndani (bungeni), wamo wengi tu...majina haya yanayotembea yako mengi sana, watu wanaandika wanavyotaka.

Kazi ya serikali hata tukiokota karatasi tu lenye majina mawili ama milioni, tunayafanyia uchunguzi na wale wanaothibitika wanapelekwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema na kuongeza:

“Kama ni kutaja tu mimi nasema si jukumu la serikali peke yake mbona gazeti la (analitaja kwa jina) limewataja, mmeona juzi magazeti mawili yametaja, pengine wale wana uhakika kwa sababu kama waliotajwa hawakuridhika, watawafikisha mahakamani, lakini sisi tutaendelea kuyachunguza na kuwachukulia hatua kwa tuliopata vielelezo vya kuwafikisha mahakamani.”

Alisema haiwezekani serikali ikawataja na kuwapeleka mahakamani bila kuwa na vielelezo halafu ikashindwa kesi na kuwa hatua hiyo ni aibu kwa serikali.

Lukuvi alisema serikali bado inaomba ushirikiano kutoka kwa raia wema ili wafichuliwe kwa kasi. “Mwenye vielelezo na majina na ana uhakika kabisa kuwa fulani anahusika na biashara haramu ya dawa za kulevya, avilete hapa na tutawatangaza kwa pamoja,” alisisitiza.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge Magige kuhusu ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya nchini, Waziri Lukuvi alisema kati ya kipindi cha mwaka 2000 hadi Machi, 2012, watuhumiwa 52,810 walikamatwa wakiwa na takriban tani 78 za dawa za kulevya za aina mbalimbali.

Aidha, alisema Watanzania 247 walikamatwa katika nchi mbalimbali duniani kati ya mwaka 2008 na Julai, mwaka huu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya. Kadhalika, alisema raia 31 wanashikiliwa katika mahabusu za magereza ya Keko na Ukonga jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Kutokana na kasi kubwa ya usafirishaji na uingizaji wa dawa hizo kupitia JNIA, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, mwezi huu aliingilia kati na kuwataja maofisa wa usalama wa uwanja huo ambao taratibu za kuwachukulia hatua zinaendelea.

Maofisa hao wanadaiwa kupanga njama kufanikisha kusafirisha dawa hizo kutoka Tanzania. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Kigwangallah, alisema kuwa atawataja kwa majina bungeni wafanyabiashara ya dawa hizo katika vikao vya mkutano wa 12 wa Bunge ulioanza jana na kwamba ameshawasilisha barua kwa Spika wa Bunge Makinda kuhusiana na kusudio lake.
CHANZO: NIPASHE