Thursday, 29 August 2013

Dawa za kulevya zatikisa Bunge

Na Boniface Luhanga, 29th August 2013
  Mbunge amvaa waziri, ataka afute kauli
                                 
                        Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka.
Kauli iliyotolewa juzi bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kuwa wabunge wengi ni miongoni mwa orodha ya majina ya wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, imeoonekana kuwachefua wabunge.

Hali hiyo inatokana na Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, kuomba mwongozo wa spika kuhusiana na kauli hiyo akisema kwamba imewachafua wabunge mbele ya jamii na kumtaka Waziri Lukuvi kuifuta.

Lukuvi alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akijibu maswali ya wabunge watatu walioitaka serikali kutaja kwa majina vigogo walinaohusika na usafirishaji wa dawa za kulevya yenye uzito wa kilo 150 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na baadaye kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, eneo la Kempton Park,  Afrika Kusini.

Dawa hizo kilo 150 aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 zilikamatwa Julai 5, mwaka huu zikidaiwa kubenwa na wasichana wawili raia wa Tanzania. Waliokamatwa ni Agnes Gerald (25) na Melisa Edward (24).

Waziri Lukuvi alilieleza Bunge kuwa iwapo serikali itaamua kuwataja vigogo wa biashara hiyo nchini kama inavyopewa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, hakuna atakayepona kwani miongoni mwao wamo wabunge wengi.

“Kama serikali ikiamua kuwataja kwa majina wahusika wa dawa za kulevya bila kufanya upelelezi wa kina kwanza, hakuna atakayepona maana miongoni mwao mmo na ninyi humu ndani (wabunge na mawaziri),” alisema Lukuvi.

Lakini jana baada ya kipindi cha maswali na majibu, Sendeka alisema kauli ya Waziri Lukuvi imewapaka matope mbele ya wananchi na wapigakura wao kwa ujumla na hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao hawazifahamu hata dawa za kulevya zilivyo.

“Kwa msingi huo, tunamuomba Waziri Lukuvi kuifuta kauli hiyo kwani imeleta sura mbaya kwa jamii kwa ujumla,” alisema Sendeka.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Lukuvi alisema hakumaanisha moja kwa moja kwamba wabunge ni wahusika wa biashara hiyo haramu bali alikuwa akieleza kuwa kama serikali ikitaja orodha inayotolewa na baadhi ya watu, itawagusa watu wengi kwa kuwa na wabunge wengi wamo.

Lukuvi alisisitiza kuwa kamwe serikali haitataja orodha hiyo kwa kuwa haina ushahidi wa kutosha na inafanya kazi kwa kuzingatia utawala bora.

Alirudia kauli yake kwamba kazi ya serikali siyo kutaja majina ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, bali ni kuwachukulia hatua na haiwezi kuwachukulia hatua bila kuwa na uhakika.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Kigwangallah, alisema kuwa atawataja kwa majina bungeni wafanyabiashara ya dawa hizo katika vikao vya Mkutano wa 12 wa Bunge ulioanza jana na kwamba ameshawasilisha barua kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kuhusiana na kusudio lake.

Dk. Kigwangallah, alisema kuwataja bungeni wahusika kutaisaidia serikali kuchukua maamuzi magumu.

Dk. Kigwangala alisema hadi Jumapili iliyopita alikuwa amepokea majina saba ya vinara wanaojihusisha na biashara hiyo na kwamba anaendelea kupokea ushahidi ukiwamo wa picha za watu hao, wanauzia akina nani na wanakaa wapi.

Mbunge huyo alisambaza taarifa kupitia mitandao ya jamii ikiwamo Facebook akiwataka wananchi wenye taarifa za wauza unga kuwasilina naye na kumpa ushahidi ili wiki ijayo awataje bungeni.

Alisema zoezi la kupokea majina hayo na ushahidi linakwenda vizuri na kwamba mwitikio umekuwa mkubwa kutoka kwa wananchi na kusisitiza kwamba lazima awataje kwa majina watu hao.

Alisema haogopi kitu na kwamba akipata ushahidi wa kina atataja majina ya watu wote waliotajwa na wananchi wanaompelekea ushahidi.

Alifafanua kuwa moja ya majina aliyopelekewa ni la kinara anayetajwa tajwa sana.

Aliwataka wananchi wenye taarifa zinazojitosheleza ambazo hazimpelei mtu kumtumia ili azifanyie kazi kwa kabla ya kuwalipua bungeni.

Alisema shinikizo la wanasiasa linaweza kusaidia kuimsha serikali kupitia Jeshi la polisi kuanza kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.
CHANZO: NIPASHE