Thursday, 29 August 2013

CAG aisafisha wizara ya Magufuli

Na Waandishi wetu, 28th August 2013

                                          
                                                              CAG, Ludovick Utouh
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeisafisha Wizara ya Ujenzi dhidi ya tuhuma za ufisadi uliohusisha Sh. bilioni 253 zilizoingia kwenye akaunti ya wizara hiyo kwa ajili ya kulipa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri.

Tuhuma hizo dhidi ya wizara hiyo ziliibulika wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilipotaka kupata ufafanuzi wa matumizi ya fedha katika wizara hiyo kwa mwaka 2011/2012.

CAG, Ludovick Utouh, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa fedha hizo zilijumlishwa kimakosa kwenye hesabu za wizara hiyo, kama matumizi ya akaunti ya maendeleo na kuongeza matumizi.

“Kihasibu fedha hizi zilipaswa kuonyeshwa kwenye hesabu za mtumiaji halisi, ambaye ni Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads)  na siyo wizara. Hivyo, ufisadi katika hili haupo, bali ni makosa ya kihasibu,” alisema Utouh.

Kwa mujibu wa Utouh, Wizara ya Ujenzi imejenga barabara katika kona zote za nchi kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ukilinganisha na miaka mingine.

Alisema kwa mara ya kwanza ofisi yake ilitoa kitabu cha muhtasari wa ripoti za CAG za mwaka 2011/2012 kwa lugha ya Kiswahili, ili kurahisisha usomaji na upatikanaji wa taarifa za ukaguzi wa hesabu kwa kila mwananchi.

Aliongeza kuwa Tanzania  imefanikiwa kwa mara ya kwanza kukagua hesabu za Umoja wa Mataifa (UN) na kukubalika na Bodi ya Ukaguzi ya UN.

“Fursa ya nchi yetu kukagua UN ni sifa kwa Taifa na imeweza kuitangaza Tanzania duniani, kujijengea uwezo na uelewa, kujikomboa kiuchumi, kupata kazi za ukaguzi katika mashirika makubwa pamoja na kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa serikali na taasisi zake,” alisema.

 
CHANZO: NIPASHE