Thursday, 29 August 2013

Ponda atinga Moro kwa basi la Magereza

Na Ashton Balaigwa,29th August 2013
                             
Askari wa Jeshi la Magereza wakimuongoza kuelekea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda kwa ajili kusikiliza kesi yake baada ya kushuka katika basi lililomtoa jijini Dar es Salaam jana.
Baada ya kusafirishwa kwa helikopta ya Polisi kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kurudi ili kusomewa mashitaka mahakamani Agosti 19, mwaka huu, jana Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisafirishwa kwa basi akitokea gereza la Segerea kuja kuhudhuria kesi inayomkabili mjini hapa.

Ponda aliwasili mahakamani hapa jana akiwa ndani ya basi la Magereza na kusomewa mashtaka matatu yanayomkabili, huku upande wa mashtaka ukisema utawasilisha vielelezo kadhaa, ukiwamo mkanda ulirekodiwa na mashahidi 15 kuthibitisha mashitaka dhidi yake.

Wakili wa Serikali, Benard Kongola, alidai hayo mbele ya Hakimu wa Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate.

Wakili Kongola alivitaja vilelelezo vingine watakavyowasilisha mahakamani hapo kuwa ni  kibali kilichotolewa na Kamanda wa  Polisi Wilaya  (OCD) ya Morogoro Agosti mosi, mwaka huu cha kufanyika kwa kongamano la Waislamu la Edi-El Fitri na nakala ya hukumu iliyotolewa na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nongwa, Mei 9, 2013 wa jijini Dar es Salaam baada ya Sheikh Ponda kupatikana na hatia ya kuingia kwa jinai kwenye kiwanja cha Marcus kilichopo Chang’ombe Manispaa ya Temeke.

Awali akisoma maelezo ya awali ya mashitaka yanayomkabili Shekh Ponda ambaye anatetewa na na mawakili watatu, wakiongozwa na Juma Nasoro, Wakili Kongola alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo Agosti 10, mwaka huu saa 11:45 jioni katika maeneo ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.

Alidai kuwa siku hiyo mshtakiwa huyo alialikwa kutoa maelezo machache kwenye kongamano la Edi-El Fitri lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri Morogoro (Uwamo).

Kongola alidai kuwa Sheikh Ponda akizungumza katika kongamano hilo alitamka kuwa “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana.”

Kongola alidai kuwa Sheikh Ponda aliyatamka maneno hayo huku akijua kuwa kutoa maneno hayo ni kosa kisheria.

Alidai kuwa kwa kufanya hivyo alivunja masharti ya mahakama ya kifungo cha nje iliyotolewa na Hakimu Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mei 9, 2013 yaliyokuwa yakimtaka kuhubiri amani.

Katika shtaka la pili, Sheikh Ponda anadaiwa kuwashawishi Waislamu kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia kuwa Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia vurugu ziliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.

Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa Ponda pia alisema kuwa Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliomkataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo, lakini alikiri kushikiriki kwenye kongamano hilo, kukamatwa na polisi Agosti 11, mwaka huu jijini Dar es Salaam na  jina lake ni sahihi kama lilivyoandikwa katika hati ya mashtaka.

Wakili Nasoro kwa niaba ya mawakili wa Sheikh Ponda, aliwasilisha ombi la mteja wao kupewa dhamana kwa madai kuwa kisheria yana dhamana.

Pia aliwasilisha ombi la kupatiwa hati yenye maelezo ya mlalamikaji ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuanda utetezi wa mteja wao.

Wakili Kongola alipinga ombi la mshtakiwa huyo kupatiwa dhamana baada ya kupata kibali kutoka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)  kwa maslahi ya usalama wa nchi.

Kutokana na ombi la dhamana kupingwa, Wakili Nasoro aliiomba mahakama kuendesha kesi hiyo kwa mujibu wa sheria kwani kibali cha DPP kilichotolewa na upande wa mashtaka wakati Sheikh Ponda alipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza hakijazingatia misingi ya sheria ikiwamo kutowekwa kwenye jalada la kesi na  hakikuonyeshwa kama kimesainiwa sehemu yoyote.

Hakimu Kabate alisema kwa sasa hawezi kutoa maamuzi kwa kuwa kesi hiyo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kuihairisha hadi Septemba 11, mwaka huu itakapotajwa tena.

Hakimu huyo alisema Septemba 17 mahakama hiyo itatoa maamuzi endapo mshtakiwa huyo atapewa dhamana au la na kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Mshtakiwa huyo alirudishwa rumande katika Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam huku baadhi ya wafuasi wake wakionekana kutokwa na machozi na wengine wakimsindikiza mita chache kutoka katika viunga vya mahakama hiyo kwa kumpungia mikono.

Kesi hiyo ya jinai namba 128 ya mwaka 2013 ilivuta hisia za watu wengi wa mjini hapa na kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza yaliimarisha ulinzi kwa kutumia  askari waliokuwa na silaha za moto, mabomu ya machozi, mbwa na vifaa vingine vya kiusalama.

Ofisi za serikali zilizopo jirani na mahakama hiyo zilisimamisha shughuli zake kwa muda huku barabara kuu zinazoingia mahakamani hapo zikifungwa kwa muda wakati magari ya askari na gari lililombeba Sheikh Ponda yakiingia na kutoka mahakamani hapo.

Baada ya kufikishwa mahakamani hapo majira ya saa 4:00 asubuhi kwa usafiri wa basi la Magereza namba MT 0029 likiongozwa na magari yakiwamo na maafisa usalama na askari kanzu waliokuwa kwenye gari namba T140 BLA aina ya Toyota Land Cruiser, wafuasi wa Sheikh Ponda walisikika wakisema takbir Allah Akbar (Tukuza Mungu Mkubwa.
 
CHANZO: NIPASHE