Thursday, 29 August 2013

Waziri Kagasheki ambabua Meya

Na Sharon Sauwa, 28th August 2013
                                         
Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki.
Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye  pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, aliyewasha moto wa kupinga mchezo mchafu katika uendeshaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, sasa umezidisha makali na ni dhahiri umembabua vibaya Meya wa Manispaa hiyo, Dk. Anatory Amani.

Ukweli huo umethibitika jana baada ya  Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutengua maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera ya kuwavua uwanachama madiwani wanane wa manispaa hiyo ambao walikuwa wanapinga kwa kauli moja mchezo mchafu uliokuwa unaendelea ndani ya Manispaa hiyo.

Uamuzi huo ambao umefikiwa na CC baada ya kuwahoji Kagasheki, Dk. Amani na viongozi waandamizi wa CCM wa Mkoa huo, ni dhahiri kwamba ni ushindi wa Balozi Kagasheki dhidi ya Meya Amani kwa kuwa madiwani waliovuliwa uanachama walikuwa wanamuunga mkono katika mgogoro mkubwa kati yao ambao uliligawa baraza la madiwani la Manispaa ya Bukoba.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana mjini Dodoma kuwa CC imetoa uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15).

Aliinukuu ibara hiyo inayosomeka kuwa: “Moja ya kazi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ni kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa.”

“…Isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu iwe imearifiwa na kutoa maelekezo.”

Aidha, Nape alisema CC imewaonya madiwani wa CCM wa Manispaa hiyo, Balozi Kagasheki na Meya Amani kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu, mshikamano na amani katika manispaa na chama.

“Kamati Kuu pia imeitaka Serikali kufanya ukaguzi wa haraka wa mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili ukweli ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza Serikali za Mitaa,” alisema.

Wakati tuhuma hizo dhidi ya Meya zikichunguzwa, Nape alisema CC inawataka madiwani wa CCM kurejesha utulivu kwenye manispaa na chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba.

Mgogoro kati ya Dk. Amani na Kagasheki, uliendelea kuitikisa manispaa hiyo licha ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa ziara yake mwezi uliopita mkoani Kagera kuzitaka pande zilizokuwa zinavutana kufikia maelewano.

Akitangaza uamuzi wa kufukuza madiwani hao Agosti 13 mwaka huu, Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera,  Aveline Mushi, alisema hatua ya kuwafukuza uanachama madiwani hao ilitokana na chama kujali maslahi ya wananchi tofauti ya watu binafsi.

Hata hivyo, Mushi alisema Diwani wa Kata ya Kashai, Yusuph Ngaiza, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, ataendelea na wadhifa wake wa uenyekiti wa CCM kwa sababu chama ngazi ya taifa ndiyo inayoweza kulishughulikia suala lake.

Siku moja baada ya uamuzi huo, Nape alisema chama chake kimetengua uamuzi uliotolewa na halmashauri hiyo ya Kagera kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kukiukwa kwa taratibu.

Nape alisema kuwa halmashauri hiyo haikufuata Katiba ya chama hicho kwa kutangaza kuwafukuza madiwani hao bila CC kupewa taarifa na kutoa maelekezo na kwamba kwa viongozi wa kuchaguliwa kama madiwani uamuzi wa kuwavua uanachama ulitakiwa kupata baraka za CC.

Hata hivyo, siku iliyofuatia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusisitiza kuwa maamuzi ya kikao hicho yalikuwa sahihi. Katika hatua nyingine, Nape alisema kuwa CC imemuagiza Mdhibiti Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG), Ludovick Utouh, kufanya ukaguzi wa tuhuma zinazomkabili Meya Amani za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Madiwani waliofukuzwa ni Ngaiza; Samuel Ruhangisa (Kitendagulo); Murungi Kichwabuta (Viti maalumu) na Deusdedith Mutakyawa (Nyanga).
Wengine ni Richard Gaspal (Miembeni); Alexander Ngalinda (Buhembe) ambaye pia ni Makamu Meya; Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Robert Katunzi wa Kata ya Hamugembe.

Uamuzi huo umekuja baada ya CC iliyokaa chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, kuwaita na kuwahoji viongozi wa juu wa chama hicho mkoani Kagera akiwamo Balozi Kaghasheki na Meya Amani. 

Mbali ya Balozi Kagasheki na Dk. Amani kuhojiwa na CC, wengine waliohojiwa ni Mwenyekiti Buhiye na Katibu wake, Mushi.  Wengine waliowekwa ‘kitimoto’ na CC ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini Yusuf Ngaiza na katibu wake, Janeth Kayanda.

Madiwani waliorejeshwa na CC walishirikiana na madiwani wa vyama vya Chadema na CUF kuhoji utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Manispaa hiyo huku wakimtuhumu Meya Amani kwa ubadhirifu na kushinikiza atimuliwe.
 
CHANZO: NIPASHE