Friday, 30 August 2013

Usafirishaji: Yakifanyika haya tutaipiku reli ya Mombasa-Rwanda

              

                                                    Treni ya kisasa ikiwa safarini 



Posted  Alhamisi,Agosti29  2013  saa 12:50 PM
Kwa ufupi
Watafiti wa masuala ya kiuchumi wanasema bandari hii ni lango kuu la biashara ya kimataifa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ambazo hazina bahari na kama ingekuwa na ufanisi kama ilivyo Bandari ya Mombasa, uchumi wa Tanzania ungeingiza takriban Dola za Marekani 1.8 bilioni kwa mwaka (Sh2.88 trilioni) sawa na asilimia 7 ya Pato la Taifa (GDP) kwa sasa.


Bandari ya Dar es Salaam; rasilimali nyingine ambayo Tanzania imejaliwa katika mwambao wa Bahari ya Hindi.
Watafiti wa masuala ya kiuchumi wanasema bandari hii ni lango kuu la biashara ya kimataifa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ambazo hazina bahari na kama ingekuwa na ufanisi kama ilivyo Bandari ya Mombasa, uchumi wa Tanzania ungeingiza takriban Dola za Marekani 1.8 bilioni kwa mwaka (Sh2.88 trilioni) sawa na asilimia 7 ya Pato la Taifa (GDP) kwa sasa.
Mbali na hayo linapokuja suala la usafirishaji wa shehena za mizigo kwenda au kutoka ughabuni; Zambia, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) na Malawi wanatumia Bandari ya Dar es Salaam ili kufikia lengo hilo.
Zambia inatumia bandari hiyo kwa asilimia 46.6, Burundi (9.1), Rwanda (8.5), Malawi(4.1) na nyingine asilimia 9.8.
Takribani asilimia 90 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania hupita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Wakati bandari hiyo ikionekana kuwa muhimu kiasi hicho, hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti kuwa nchi za Uganda na Rwanda zitasitisha kutoitumia bandari hiyo kuanzia mwezi Septemba.
Kwa mujibu wa Chama cha Wasafirashaji wa Mafuta nchini(Tatoa), nchi hizo zimekuwa zikiilalamikia bandari hiyo lakini hakuna hatua zozote zimechukuliwa na serikali kutatua matatizo hayo.
Takriban asilimia 90 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania hupita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Wakati bandari hiyo ikionekana kuwa muhimu kiasi hicho, hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti kuwa nchi za Uganda na Rwanda zitasitisha kutoitumia bandari hiyo kuanzia mwezi Septemba.
Kwa mujibu wa Chama cha Wasafirishaji wa Mafuta nchini(Tatoa), nchi hizo zimekuwa zikiilalamikia bandari hiyo lakini hakuna hatua zozote zimechukuliwa na Serikali kutatua matatizo hayo.
Moja ya malalamiko yanayotajwa ni wafanyabiashara kucheleweshewa mizigo yao katika bandari hiyo na kuwapo kwa vizuizi vingi kwenye barabara za Tanzania.
Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe anasema nchi hizo haziwezi kujitoa katika Bandari ya Dar es Salaam kwani umbali kutoka Kigali hadi Dar es Salaam ni zaidi ya kilometa 1,460) wakati kutoka Kigali hadi Mombasa ni kilometa 1,704 ilipo bandari nyingine ambayo inatarajiwa kutumiwa na Rwanda.

Waziri anabainisha kwamba inachukua saa 18 kutoka Dar es Salaam hadi Kigali wakati Kigali mpaka Mombasa ni saa 25.
Dk Mwakyembe anakiri kwamba kuna vizuizi 56 katika barabara inayotoka Dar es Salaam hadi Rusumo mpakani mwa Rwanda na Tanzania.
Kutokana na vizuizi hivyo Serikali ina mpango wa kuvipunguza na kubaki vitatu, lakini pia anasema atawasiliana na waziri mwenzake wa Rwanda mwenye dhamana ya Uchukuzi kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo.
Rwanda, Uganda kujenga reli
Wakati bandari hiyo ikisifika kwa kutokuwa na tija, Juni Rais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya walikutana mjini Entebe Uganda na kwa pamoja walipitisha uamuzi wa kujenga reli itakayounganisha Miji ya Mombasa, Kampala na Kigali.
Ujenzi wa reli hiyo una thamani ya Dola 13 bilioni za Marekani na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018 na mpango huo unatajwa kuwa muhimu katika kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Mombasa hadi Kigali.
Ujenzi huo bila shaka utaleta changamoto katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo inaonekana kuwa na matatizo chungu nzima, ambayo yamesababisha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kukataa kupitisha ripoti ya Hesabu ya Mamlaka ya Bandari (PTA) kutokana na ubadhilifu wa Sh57.6 bilioni.
Kwa upande wa Tanzania, Dk Mwakyembe anasema mikakati inaendelea ya kuiboresha reli ya kati na itakapokamilika itasaidia kusafirisha mizigo kupeleka maeneo mbalimbali zikiwamo nchi jirani.
Waziri Mwakyembe anafafanua kuwa watahakikisha hadi kufika mwaka 2015 Bandari ya Dar es Salaam, inakuwa na uwezo wa kuingiza tani milioni 12 hadi tani milioni 18 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe anasema ujenzi wa reli ya nchi hizo tatu hautaathiri sana uchumi kwani kuna umbali mrefu kutoka Mombasa hadi Kigali.
Profesa Wangwe anasema kuna umuhimu wa kujenga reli inayotoka Kigoma kwenda nchi za Kongo (DRC) na Burundi ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
Profesa huyo anasema Bandari ya Dar es Salaam inaweza kuwa kitovu cha biashara katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lakini ili ifikia katika kiwango hicho hakuna budi kufanya kazi kisasa.

“Mizigo ishughulikiwe haraka na watumie taknolojia za kisasa,” anasema Profesa Wangwe.
Vizuizi barabarani
Profesa Wangwe anasema ili kuongeza ufanisi zaidi, mambo matatu yanapaswa kutazamwa ambayo ni kuondoa rushwa, kutumia teknolojia ya kisasa katika bandari hiyo na kupunguza vizuizi vya ukaguzi barabarani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Joseph Mbele anasema Tanzania inapaswa kufanya utafiti ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuleta ushindani.
Utafiti uliofanywa na mtandao unaojihusisha na ukaguzi wa hesabu KMPG na Benki ya Dunia(WB) unaonyesha kwamba Mei na Juni 2012, meli zilizokuwa zimebeba makontena zilikuwa zinapanga foleni kwa wastani wa siku 10 ili kusubiri gati katika Bandari ya Dar es Salaam, wakati muda wa kusubiri ulikuwa chini ya siku moja katika Bandari ya Mombasa.
Pia utafiti huo unasema siyo tu kwamba Bandari ya Dar es Salaam haina ufanisi, lakini pia ina gharama kubwa kwa asilimia 74 kuliko Mombasa na kusababisha kampuni nyingi za meli, kulazimika kulipa ada zaidi kwa mawakala kuliko Bandari ya Mombasa.
Ripoti hiyo inaweka wazi kuwa kama hali ya sasa haitapatiwa ufumbuzi, Bandari ya Dar es Salaam inaweza kupoteza nafasi yake katika biashara ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
source : Mwananchi