Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Posted Oktoba12 2013 saa 14:40 PM
Posted Oktoba12 2013 saa 14:40 PM
Kwa ufupi
Enzi hizo Magomeni ndiyo ilikuwa kama Masaki.
Mwalimu Nyerere alimwomba rafiki yake Mustafa Songambele amtafutie
kiwanja katika maeneo hayo, naye akampatia hicho ambacho sasa ipo nyumba
ambayo imegeuzwa Makumbusho ya Taifa.
Dar es Salaam. Wakati Taifa linaadhimisha miaka
13 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, pia anakumbukwa kwa namna alivyoona
umuhimu wa kununua kiwanja na kujenga nyumba yake mwenyewe, eneo la
Magomeni mkoani Dar es Salaam.
Enzi hizo Magomeni ndiyo ilikuwa kama Masaki.
Mwalimu Nyerere alimwomba rafiki yake Mustafa Songambele amtafutie
kiwanja katika maeneo hayo, naye akampatia hicho ambacho sasa ipo nyumba
ambayo imegeuzwa Makumbusho ya Taifa.
Mhifadhi Malikale anayesimamia nyumba hiyo,
Emmanuel Katoroki anasema si serikali iliyoamua kuifanya nyumba hii kuwa
makumbusho bali Mwalimu Nyerere mwenyewe, ambaye alitaka Watanzania
wajue ilipotoka historia yake kisiasa.
Katoroki anasimulia kuwa Mwalimu Nyerere baada ya
kupata tetesi kuwa anaweza kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, alitafuta sehemu
ya usalama na ndipo rafiki yake alipomtafutia kiwanja hicho kilichopo
Magomeni, Mtaa wa Ifunda.
“Mwalimu alikinunua kiwanja hiki mwaka 1957. Hii
ilikuwa ni baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuwa Waziri Mkuu na
wakati ule alihitaji ulinzi kwa kuishi katika mazingira salama, kwa kuwa
Magomeni enzi zile ndiyo ilikuwa kama Masaki sasa hivi, akanunua na
kuanza ujenzi,” anasema Katoroki.
Ulinzi wake
Katoroki anasema kwa wakati ule ulinzi ulikuwa
mdogo hivyo kwa mtu anayeanza kuchipukia kisiasa tena anayetajwa kuweza
kushika nafasi kubwa katika nchi, alihitaji kujilinda kwa kuwa lolote
lingeweza kutokea.
Aidha, Katoroki anasema historia ya kisiasa ya
Mwalimu ilianza wakati akiishi katika nyumba hii na baada ya kuteuliwa
kuwa Waziri Mkuu kwani baada ya hapo alikwenda kuishi katika nyumba ya
serikali Sea View na baadaye Ikulu.
“Pia ni nyumba ya kihistoria kwani aliijenga kwa
kiinua mgongo chake baada ya kuacha ualimu pale Shule ya Sekondari ya
Pugu. Baada ya kuwepo tetesi na pengine mwenyewe alikuwa na taarifa
kamili, aliamua kuachana na ualimu, “ anasema Katoroki.
“Ninasema historia yake kisiasa ilianzia katika
nyumba hii kwani aliamkia katika nyumba hii kwenda kuapishwa kuwa Waziri
Mkuu na kuanza rasmi shughuli za kisiasa na ukombozi wa bara la
Afrika,” anasema.
Kingine ambacho kinaifanya nyumba hii kuwa ya
kihistoria ni pamoja na kuwa alijinyima wakati akijenga, aliishi kwa
muda wa miezi minane tu kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa
Tanganyika Januari 1, 1960.
Katoroki anasema pamoja na nyumba hiyo kuwa ya
pekee, Mwalimu aliwahi kuiuza baada ya kutokea mgogoro katika familia
yake iliyokuwa ikiiogombea.
“Inavyoonekana Mwalimu baada ya kuwa Waziri Mkuu aliitelekeza
nyumba hii na ndugu wakaanza kuigombania. Mwenyewe baada ya kupata
taarifa hizo aliamua kuumaliza ugomvi wa ndugu kwa kuiuza,” anasema
Katoroki.
Hata hivyo historia nyingine iliandikwa mwaka 1973
wakati Jumuiya ya Wafanyakazi (JUWATA), ikitimiza miaka 10 tangu
kuanzishwa kwake ambayo Mwalimu Nyerere alialikwa kuwa mgeni rasmi
katika sherehe hizo na Jumuiya hiyo iliamzawadia nyumba.
“Juwata walimwambia Mwalimu tunataka kukupa
zawadi, alipoifungua alikuta ni hati ya nyumba yake ambayo aliwahi
kumuuzia mtu mwingine,” anasema Katoroki.
Viongozi wa Juwata walimnunulia Mwalimu Nyumba
hiyo kutoka kwa mtu aliyemuuzia kwa Sh 35,000 na kumrudishia mwenyewe
kwa njia ya zawadi.
Aliwashukuru kwa kuirudisha mikononi mwake. Hata
hivyo alisema asingependa ibaki kwenye mikono yake kwani inaweza
kurudisha matatizo aliyoyakwepa na hivyo akaamua kuitoa kwa serikali ili
iifanye kuwa Nyumba ya Makumbusho.
Serikali kwa muda mrefu iliitelekeza nyumba hii na
hivyo kuanza kuharibika na vyombo kuanza kupotea. Hata hivyo, Wizara ya
Utamaduni ilipewa jukumu la kuisimamia nyumba hii chini ya Idara ya
Mambo ya Kale na mwaka 2002 ilikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na
Utalii chini ya Idara ya Mambo ya Kale.
Vitu vyake
Pamoja na kuwa vitu vingi vya Mwalimu vilipotea
baada ya Mwalimu Nyerere na familia yake, ndani ya nyumba hiyo vipo
vitanda vya familia kikiwamo kile alichokilalia mwalimu mwenyewe kabla
ya kuhama.
Vitu vingine vilivyopo ni kabati la jikoni, kabati
la kuhifadhia fedha (kibubu), pasi ya mkaa, mtungi wa kuhifadhia maji,
redio ya mbao, makochi, cherehani na vyombo vya jikoni.
Pamoja na vyombo ndani ya nyumba hiyo, kuna noti
za pesa zilizokuwa zikitumika enzi za utawala wake. Pia vipo vitabu
alivyowahi kuandika kama vile; Ujamaa ni Imani, Maendeleo ni Kazi,
‘Education to Self Relience’, Tujisahihishe, Tanu na Raia, ‘Our
Leadership and Destiny of Tanzania’ na vingine vingi.
Vitu vingi vilivyopo ndani ya nyumba hiyo
vilipatikana kutoka kwa Mzee Omary (Aliyekuwa baba mlezi wa Mwalimu
Nyerere), ambaye inadaiwa kuwa baada ya kuona nyumba haina mwelekeo
alivichukua na kwenda navyo Dodoma ambako anaishi mpaka sasa.
“Mzee huyu ametunza vitu vingi vya Mwalimu na kama
unavyoona humu ndani, hivi vyote tumevipata kwake, tunasikia kuna
vingine walichukua ndugu na sasa wameviuza kwa watu wa makumbusho
binafsi,” anasema Katoroki.
“Nia yetu ni kupata kila kitu ambacho kilikuwamo humu ndani, vingi viliuzwa kwenye makumbusho binafsi na wao wanaviuza kwa bei za juu hivyo si rahisi kuvipata,” anasema Katoroki.
“Nia yetu ni kupata kila kitu ambacho kilikuwamo humu ndani, vingi viliuzwa kwenye makumbusho binafsi na wao wanaviuza kwa bei za juu hivyo si rahisi kuvipata,” anasema Katoroki.
Nyerere alikuwa Mkatoliki haswa
Na Maimuna Kubegeya, Mwananchi
Kwa ufupi
“Tangu atimize miaka 51 babu amekuwa akifanya ibada
za asubuhi na jioni hadi alipokutwa na umauti” anasema Julius Makongoro
Nyerere mjukuu wa Mwalimu Nyerere.
Dar es Salaam. Moja ya urithi mkuu aliouacha
Mwalimu Nyerere kwenye familia yake ni kumcha Mungu, ambapo watu wake wa
karibu wanasema alikuwa Mkristo wa kweli ambaye alikuwa akiishi maisha
ya kumcha Mungu.
“Tangu atimize miaka 51 babu amekuwa akifanya
ibada za asubuhi na jioni hadi alipokutwa na umauti” anasema Julius
Makongoro Nyerere mjukuu wa Mwalimu Nyerere.
Anasema wakati wa uhai wake, alikuwa yuko tayari kukupa adhabu yeyote ile ikiwa tu utakosa kufanya ibada.
“Ilifikia kipindi tulikuwa tukipewa adhabu ya kunyimwa chakula kwa kosa la kushindwa kusali,” anasema.
Kwenye familia yao ilikuwa ni kawaida kusali novena ambayo kwa kawaida husaliwa kila baada ya saa nane.
“Hivyo ikitokea sala hiyo ikaangukia usiku wa manane, babu alikuwa akituamsha nyumba nzima kwa ajili ya kusali,” anasema Julius.
Monsinyori Deogratias Mbiku mlezi na paroko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni miongoni mwa watu wanaomfahamu Mwalimu Nyerere.
“Kwa mara ya kwanza nilikutana na Mwalimu mwaka
1963, pale Nyegezi, Mwanza, alipokuja kumtembelea Fideric Mula aliyesoma
naye huko nchini Scotland.
“Nyerere hakuwa na makuu vaa yake, ongea yake hata
ushiriki wake katika masuala mbalimbali ya kijamii, ulikuwa ni wa
kawaida kabisa”.
Kila mahali alipokwenda alikuwa akiomba apelekwe
kanisani na hakusita kuwaambia walinzi wake; “Nipelekeni kanisani mimi
ni Mkristu.” Alikuwa hafichi hilo.
Mbiku anasema ratiba ya Nyerere siku zote ilianza
kwa sala. “Na siyo tu alikuwa akisali, bali alikuwa pia akitoa
“comments” zake kuhusiana na ibada,” anasema Mbiku.
Anasema pia alikuwa muwazi katika kueleza kama
ameridhishwa au hakuridhishwa, kwa kuwa sehemu nyingi kuna namna
mbalimbali za kufanya ibada.
“Alikuwa akifuatilia ibada na siyo tu kusali kwa kutimiza wajibu,” anasema na kuongeza:
“Kwa mfano alienda kanisa moja, akakuta wanaimba
sana, yaani wanatumia muda mwingi kuimba na kwa muda mfupi wanasali,
Mwalimu hakusita kuwaambia kinachotakiwa ni kusali muda mrefu kila mtu
apate muda wa kufanya toba na siyo kuimba kama kwenye tamasha.
“Halafu hii baba yetu kama kuna ‘tune’ ambayo watu
wanaweza kudaka sawa, lakini hii ni sala ya bwana, tusali wote”
alisisitiza na kuongeza kuwa kutoa huduma za kiroho katika Kanisa la
Mtakatifu Petro kuanzia mwaka 1972 alikokuwa akisali Mwalimu.
Mbiku anasema Nyerere alikuwa ni zaidi ya muumini,
kwani siku zote alikuwa mshauri mzuri wa masuala yanayohusiana na
ibada, akilenga kuweka mazingira mazuri ya kumwabudu Mungu.
“Nilikuwa nikimshuhudia Mwalimu akija kusali kila siku kabla ya kwenda kazini kwake,” anasema.
Sababu hizi na nyingine nyingi zilifanya kiongozi
huyu kuingia kwenye mchakato wa kutangazwa mwenye heri mara baada ya
kifo chake.
Mbiku anasema mchakato huo si wa muda mfupi kwani
una hatua kadha wa kadha. Hivyo katika hatua za awali uchunguzi
hufanyika juu ya maisha yake.
Anasema hatua hiyo ya kwanza inaitwa mtumishi wa
Mungu, halafu hatua pili ni kuangalia miujiza inayomhusisha huyo
mtumishi wa Mungu. Hatua ya mwisho ni kumtangaza mwenye heri. Kwa
kawaida mchakato huo huanza miaka mitano baada ya mhusika kufariki
dunia.
Mbiku anasema mchango wa Mwalimu Nyerere umekuwa ukitambuliwa na watu wengi, hususani waliokuwepo katika Kanisa Katoliki.
“Kwa mfano mwaka 1994 nilikuwa Makamu Mkuu wa Chuo
katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki huko nchini Kenya, kilichokuwa
kikihudumia nchi nane za Afrika ya Mashariki.”
“Wakuu wa chuo kile walipendekeza Mwalimu Nyerere
apewe shahada ya heshima ya Kanisa Katoliki, hivyo nikaagizwa kwenda
kumpelekea taarifa.”
“Nilirudi nyumbani na nikamsubiri kule kanisani,
baada ya kanisa nilimwambia kuwa nahitaji kuongea naye na hivyo
akanikaribisha nyumbani kwake,” anasema.
Alipofika nyumbani kwake siku ya pili yake, alikaribishwa chai na kufanya maongezi.
“Nilimfikishia ujumbe nikimwambia kuwa, viongozi
wa chuo wamemteua yeye kupokea shahada ya heshima,” anasema na kuongeza
kuwa majibu ya Mwalimu Nyerere yalikuwa; “Asante sana kwa kunipa nafasi
hiyo, lakini kwa sasa sitoweza kuhudhuria kwani kwa sasa hali ya nchi
siyo nzuri, kuna matatizo fulani yanayohusiana na masuala ya muungano
yameingia hivyo ninaumiza kichwa katika kuyatafutia ufumbuzi.
“Lengo langu hasa ni kuhakikisha muungano unasimama, nisingependa kuona muungano unakufa mimi nikiwa hai.”
Mbiku anasema baada ya Mwalimu Nyerere kuacha kupokea shahada hiyo, Kadinari Rugambwa alichaguliwa badala yake.
Jambo hili lilinifanya niwe naamka mapema kumuwahi na huo ndiyo ukawa utaratibu wa maisha yangu.
Nyerere alivyoishi na wajukuu
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Kwa ufupi
Unapofika katika nyumba yake iliyopo jijini Dar es
Salaam maeneo ya Msasani maarufu kwa Mwalimu Nyerere,
kinachoyatofautisha maisha ndani ya nyumba hiyo na zile za Magomeni na
Ilala ni mazingira nadhifu.
Si urithi wa mali, isipokuwa ni mapenzi kwa
binadamu wenzake na hekima ambavyo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere ameviacha katika vitabu, maandiko mbalimbali na kwa
familia yake, tangu afariki dunia miaka 14 iliyopita.
Unapofika katika nyumba yake iliyopo jijini Dar es
Salaam maeneo ya Msasani maarufu kwa Mwalimu Nyerere,
kinachoyatofautisha maisha ndani ya nyumba hiyo na zile za Magomeni na
Ilala ni mazingira nadhifu.
Wenyeji ndani ya nyumba hii kwa mwonekano na
mazungumzo hawana tofauti na Watanzania wa kawaida, hawana majivuno na
wanamkaribisha mgeni kama ndugu au jamaa waliyemfahamu miaka mingi.
Pamoja na kuwa nyumba ni kubwa na wenyeji ni
wengi, lakini kwenye maegesho ya magari lipo gari moja tu. Mwonekano wa
nje wa nyumba hii unaweza kukufanya ufikiri ndani kuna magari zaidi ya
matatu tena ya kifahari.
Wanafamilia ni wakarimu sana, kwa kawaida
ungetarajia kusikia wenyeji wakitumia maneno kama “Yes, No” na maneno
mengine ya Kiingereza kwa kuwa hiki ni kitambulisho cha vijana waliopata
elimu angalau ya sekondari, lakini hapa ni tofauti, wote wanazungumza
Kiswahili na bahati mbaya wakichanganya huwa ni lugha ya Kizanaki.
Wajukuu wa Baba wa Taifa, Moringe Magige na Julius
Makongoro wanasema huu ndiyo urithi ambao Baba wa Taifa aliwaachia
ndugu zake wakisema kuwa walilelewa kuamini kuwa mali siyo kitu kuliko
utu na ndivyo walivyo.
Maisha ya Mwalimu Nyerere kama babu
Wengi tunafahamu historia ya Baba wa Taifa hasa
katika majukumu yake ya uongozi wa Tanzania na ukombozi wa bara la
Afrika, lakini Moringe na Julius wanaturudisha nyumbani wakisimulia
walivyomfahamu babu yao.
Moringe anasimulia akisema; “Kwanza mimi
sikufahamu kwa jinsi gani babu alikuwa mtu muhimu katika nchi hii na
bara la Afrika kwa ujumla, nilijua baada ya kufariki dunia na kuanza
kusoma historia yake na kugundua vitu vingi alivyofanya,”
“Sikuiona tofauti yake na mababu wengine kwani
shuleni nilisikia watu wakisimulia jinsi walivyoishi na babu zao na
sikuona tofauti na babu yangu,” anasema Moringe.
Anasema Mwalimu Nyerere aliwapenda wajukuu zake,
alipenda kufanya shughuli za shamba akiwa na wajukuu zake, hakutaka hata
mmoja azembee kwenda shambani.
“Babu aliipenda familia yake, tumeishi na ndugu
wengi kwa sababu hakutaka kukaa mbali na ndugu zake na kila mmoja
alihakikisha anapata wasaa wa kukaa naye na kuzungumza naye, mfano
alikuwa na utaratibu wa kula chakula cha jioni na sisi wajukuu zake,”
anasema Moringe.
Aidha anasema kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akiwahimiza kuongeza juhudi shuleni hasa katika masomo ya Kiingereza na Hisabati.
“Babu alikuwa akifuatilia maendeleo yetu shuleni,
kila mwisho wa muhula alikagua matokeo ya kila mmoja wetu na alikuwa
akisisitiza zaidi masomo ya Kiingereza na Hesabu akisema hayo ndiyo ya
msingi,” anasema Moringe.
Alikuwa anapenda kupiga makonzi
Kila mtu anakumbuka adhabu gani alikuwa anapewa na
bibi au babu yake pale anapokosea, lakini Julius anatuambia kuwa
Mwalimu Nyerere alikuwa akiwapiga makonzi wajukuu zake pale wanapokosea.
Julius anasema adhabu kubwa waliyokuwa wakipewa na
babu yao ni kupigwa makonzi hata hivyo utaokoka tu kwa juhudi zako za
kutoka mbio kwani ukisimama anaendelea kukupiga. “Babu alikuwa na tabia
ya kutupiga makonzi hasa ukiwa mtundu au ukimpitia karibu wakati
anacheza bao lazima atakupiga japo konzi moja,” anasema.
Pia anasema kamwe hatasahau siku moja alipomuomba
babu yake akaangalie mkanda wa video mchana;” Nilimwambia babu tunaomba
kuangalia mkanda kwa sababu Tv ilikuwa inakaa Maktaba, alinikubalia na
kuniambia nenda ukawaite na wenzako unaotaka kuangalia nao. Basi
nikaenda kuwaita tulivyofika alitufungia na kuanza kutupiga makonzi ,”
anasema Julius.
Aidha anasema babu yao aliwapangia muda maalumu wa
kuangalia televisheni pia aliwachagulia mikanda ya kutazama kwa kuwa
alipenda wawe na maadili mema.
Vituko,utani wa babu na wajukuu zake
Pamoja na kuwapiga makonzi wajukuu zake lakini
kuna wakati alikuwa akiketi chini na kufanya utani na kushuhudia vituko
vya wajukuu zake.
Moringe anasema moja kati ya maswali ya utani
waliokuwa wakimuuliza babu yao ni iwapo enzi za ujana wake alikuwa
akifanya starehe za aina mbalimbali.
“Tulikuwa tunamuuliza babu hivi unajua kuogelea au
kucheza muziki kwa sababu hatujawahi kukuona hata siku moja ukicheza,
alijibu ‘siwezi’, tukawa tunamuuliza sasa wewe ujana wako ulikuwa
unafanya nini, alisema ‘kusoma tu’, anasema Moringe.
Aidha wanasema utani mwingine kwa babu yao ilikuwa
ni kuwa hajui kuendesha gari. Julius anasema “Tangu nimepata akili
sijawahi kumuona akiendesha gari, nina wasiwasi alikuwa hajui
kuendesha”.
Julius pia anasema hajawahi kumuona babu yake akiwa amevaa suti
au kuchomekea huku akisema inawezekana zamani alikuwa analazimishwa
kuvaa hivyo. “Sijawahi kumuona babu amevaa suti au amechomekea shati,
hata hakupenda ndugu wavae suti hasa tukiwa Butiama, alipenda kuvaa
‘simple’.
Alisisitiza maadili
Moringe na Julius wanasema wanaamini babu yao
alikuwa akilinda maadili kwa kutowaachia watazame televisheni ovyo na
kuwahimiza kushiriki kanisani.
“Babu hakuwa na mchezo linapokuja suala la
kanisani, yaani usipoenda kanisani ni ugomvi mkubwa anaweza hata
kukufukuza usile naye chakula cha jioni,” anasema Moringe.
Wakizungumzia iwapo Baba wa Taifa angekuwa hai leo
angebariki matumizi ya mitandao ya kijamii kama ‘facebook’ na ‘twitter’
kwa pamoja walisema asingepinga kwani alikuwa mpenda maendeleo.
“Watu wengi huwa wanazungumza wakisema kuwa babu
alikuwa hataki watu waendelee kwa kutumia teknolojia, sio kweli, babu
alikuwa anapenda maendeleo lakini aliheshimu utamaduni,” anasema Julius.
Akitolea mfano wa dada yao mmoja aliyekuwa akiishi
Ulaya walisema, babu yao hakuwa na tatizo na mavazi yake lakini
alimwonya kuwa ni lazima aangalie anavaa wapi.
“Mfano tukiwa hapa Msasani babu hakumkataza kuvaa
nguo zake anazopenda, lakini tulipoenda Butiama alikuwa akimrudisha pale
anapovaa nguo anazoona haziendani na utamaduni wa watu wa kule,”
anasema Julius.
Anaongeza kuwa Mwalimu asingekuwa na tabu na
mitandao hiyo au teknolojia yoyote isipokuwa pale itakapotumikwa visivyo
kama wafanyavyo wengi.
“Ukiukwaji wa maadili unaotokana na teknolojia
unawakwaza watu wengi, watu wanatumia ndivyo sivyo na hiki pengine
kingemkera babu,” anasema Julius.
Siri ya kifimbo cha babu yao
Moringe na Julius wanasema wamesikia hadithi
nyingi kuhusu kifimbo cha Mwalimu Nyerere alichokuwa akipenda kukibeba,
wengine wamediriki kusema alizikwa nacho.
Julius anasema kwanza wanavyofahamu wao babu yao alikuwa nazo
zaidi ya nne, nyingine alinunua mwenyewe na nyingine alipewa zawadi.
“Babu alikuwa na fimbo nyingi, alibeba yoyote
anapotoka nyumbani, wakati mwingine aliweza kuisahau na kutuagiza
tumpelekee nje kama ameshatoka,” anasema Julius.
Aidha Moringe anasema amewahi kusikia kuwa asili
ya babu yao kutembea na fimbo hiyo ilitokana na nia yake ya kuacha
kuvuta sigara. “Niliwahi kusikia babu alikuwa akivuta sigara, sasa
alipotaka kuacha alipewa fimbo kama njia mbadala ya kushika kitu mkononi
ili aweze kuacha,” anasema Moringe.
Wasifu wa Julius na Moringe
Julius Kambarage (28) ni mtoto wa Makongoro ambaye
ni mtoto wa tano wa Mwalimu Nyerere na Moringe ni mtoto wa Magige
ambaye ni mtoto wa tatu.
Hivi sasa Julius anafanya kazi katika Kampuni ya
Uingizaji na Utoaji wa Mizigo (Clearing and Forwading) iitwayo Tesna
Quality wakati Moringe ni Ofisa Uwekezaji katika Mfuko wa Hifadhi za
Jamii (NSSF).
Mwalimu Nyerere alimfanya kila mmoja ajione muhimu
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Kwa ufupi
Mimi siku zote alikuwa akiniita ‘rafiki yangu’ kwa
kuwa alinipa jina la rafiki yake kipenzi, hakuwahi kuniita kwa jina
langu la Moringe hata siku moja
Oktoba 14 ya kila mwaka Watanzania hukumbuka
siku ya huzuni, ambapo walimpoteza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
aliyefariki dunia tarehe na mwezi huo, mwaka 1999 katika Hospitali ya
Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alipokwenda kwa matibabu.
Madaktari walieleza kuwa kifo cha baba wa taifa
kilitokana na ugonjwa wa saratani ya damu. Julius Nyerere alikuwa Waziri
Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika huru na baadaye alikuwa Rais wa kwanza wa
Tanganyika.
Mwalimu alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Baada
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo alikaa madarakani
akiiongoza Tanzania kwa miaka zaidi ya 20.
Oktoba 14 ya kila mwaka imefanywa kuwa ya kitaifa
ikitoa nafasi ya kumbuka, kutafakari aliyolitendea taifa, lakini zaidi
kuenzi yote mema na mazuri kwa Tanzania aliyoipenda.
Tangu kufariki kwake mengi yamekuwa yakikumbukwa na kutajwa kama mfano na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo viongozi.
Ni wazi na hakuna anayeweza kupinga kuwa Mwalimu
Nyerere ameacha mambo mengi mazuri ya kujivunia na mfano wa kuigwa na
jamii ya Watanzania.
Historia hiyo ipo katika nyanja mbalimbali kama
vile siasa, elimu, uchumi hata utamaduni katika taifa la Tanzania
linaloelezwa kuwa na makabila zaidi ya 120, hivyo pia kuwa na tamaduni
tofauti kati ya kabila moja na nyingine, ingawa baadhi ya makabila
hufanana mila na utamaduni wao kwenye baadhi ya mambo.
Katika makala haya leo, tunaangalia namna Mwalimu
Julius Kambarage alivyoacha historia ya kipekee katika kuenzi utamaduni
wa kabila lake na kuheshimu uhusiano katika familia na urafiki wake na
watu wengine.
Ukweli wa hilo unadhihirishwa na jinsi Mwalimu
alivyokuwa akitoa majina kwa watoto wake, wajukuu na jinsi alivyokuwa
akiwaita kila mmoja kwa namna yake, akizingatia uasili na heshima kati
yake na watu wengine.
Ndivyo ilivyo, Mwalimu aliwapa majina watoto wake
akitaka kila mmoja awe na jina lenye maana kama siyo kwa familia, basi
kwake binafsi.
Hapa mfano wa karibu ni namna alivyowapa majina
watoto wake kwa kuwapa majina ya pili ambayo ni ya kiasili na kwa namna
tofauti, huku kila jina likiwa na maana kwa familia na kwake.
Katika uhai wake, Mwalimu Nyerere alibahatika
kupata watoto saba ambapo mbali na majina yaliyotokana na imani yake ya
dini ya Kikristo, kila mmoja alimpa pia jina la kiasili ya Kizanaki,
kabila alilotokea, ukoo wake au wa mkewe mama Maria Nyerere.
CHANZO: MWANANCHI
Akionyesha mfano wa kuthamini uafrika na asili yake Nyerere
alimwita mtoto wake wa kwanza kwa jina la Burito au Andrew, mwingine
alimwita Watiku (Anna), Magige(Emily), Nyerere (John), Makongoro
(Charles) na Madaraka ambaye ni Godfrey.
Mmoja wa wajukuu zake aliyempa jina la Moringe
anasema kuwa anaamini kila mtu katika familia ya mwalimu alipewa jina
kwa sababu maalumu, kwani pamoja na kuwa majina mbalimbali, bado babu
yao aliwaita kwa maana ya jina la kiasili.
Anatoa mfano wa baba yake yeye, (Mzee Magige)
ambaye alipewa jina la baba wa Mama Maria Nyerere, hivyo Mwalimu alikuwa
akimwita Magige ‘mkwe’.
“Babu alikuwa akimwita baba yangu kwa lugha ya
Kizanaki ‘Tata Kyara’ akimaanisha baba mkwe, nimemsikia akimwita hivyo
siku zote na hakuwahi kutumia jina lake la Magige au Emily.
Anasema hata yeye alipewa jina la Moringe ambalo
ni la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine kwa sasa ni
marehemu, ambaye alikuwa ni rafiki mkubwa wa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
“Mimi siku zote alikuwa akiniita ‘rafiki yangu’
kwa kuwa alinipa jina la rafiki yake kipenzi, hakuwahi kuniita kwa jina
langu la Moringe hata siku moja,” anasema.
Anaongeza kuwa alifanya vivyo hivyo kwa ndugu wote
akiwaita kutokana na asili ya majina yao na kwa kuwa wengi walikuwa na
majina ya Kizanaki aliwaita kutokana na uhusiano au tafsiri ya majina
hayo.
Moringe anasema kuwa Nyerere aliwalea watoto na
wajukuu zake katika maisha yaliyolenga kuwaonyesha Watanzania kuwa kila
mtu ni sawa kwa kuwa pamoja na kuwa na madaraka, hakuyatofautisha maisha
yake na ya Watanzania wengi.
“Nchi hii matajiri ni wachache kuliko maskini,
alitaka familia yake iishi maisha ya kawaida, yanayofanana na ya
Watanzania wengi ingawa alikuwa na uwezo wa kuwafanya waishi kama wako
peponi.
Hii ililenga kuonyesha kwamba alijali usawa na kutaka kila mmoja ajione muhimu katika nchi yake,” anasema Moringe.
Anabainisha kuwa Mwalimu hakutaka Watanzania
wajione wanyonge kwa tabaka na walionacho na wasionacho na yeye alipinga
hali hiyo kwa kuonyesha mfano.
“Isingekuwa na maana kwa babu kufanya mambo ambayo
kwa Watanzania ni mageni, kama angefanya hivi pengine leo hii sisi kama
familia au kama Watanzania tusingejivunia kupata mtu kama yeye,”
anasema Moringe.
Anaongeza kuwa unapotaka kusisitiza jambo fulani lifanyike,
mwenyewe unatakiwa kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano na hiki
ndicho alichokuwa akifanya Baba wa Taifa.
“Kama angejihusisha na biashara nyingine wakati
akiwa kiongozi wa nchi, maana yake angetengeneza mwanya kwa viongozi
wengine kufuata nyayo zake na hii ingeweza kutengeneza mianya ya rushwa
na ukiukwaji wa maadili,” anasema Moringe. Akizungumzia yeye kutaka
kujiingiza katika siasa anasema atafuata nyayo za babu yake ambaye kabla
alitumikia taaluma yake na baadaye ndipo akajiingiza huko.
“Ninapenda kufuata nyayo za babu, alisoma, akawa
mwalimu na baadaye ndiyo akajiingiza katika siasa, nami nitafanya hivyo,
sasa hivi ni wakati wangu wa kuitumikia taaluma yangu mpaka pale
nitakaporidhika ndipo nitaingia kwenye siasa,” anasema Moringe.