Posted Jumapili,Oktoba13 2013 saa 12:15 PM
Kwa ufupi
Akitoa mhadhara nchini Afrika Kusini, kiongozi huyo
mstaafu aliyeiongoza UN kati ya 1996 na 2006 na ambaye ni raia wa Ghana
alisema ni viongozi wachache tu wanaoipiga vita ICC na kuonya kuwa,
kujiondoa katika mahakama hiyo watakuwa wanalinda masilahi yao binafsi
na si ya Waafrika wote.
Katika nyakati tofauti wiki hii zimesikika sauti
za watu wawili mashuhuri barani Afrika zikiwahadharisha viongozi wa
nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), kuhusu dhamira yao ya kuzitoa
nchi zao katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), iliyoko The
Hague, Uholanzi kwa madai kwamba mahakama hiyo inawadhalilisha na
kuwalenga tu viongozi wa bara hilo.
Sauti hizo zimekuja wakati mwafaka, kwani wakati
zikitoka, mawaziri wa nchi za nje wa nchi wanachama wa AU walikuwa
wakikutana mjini Addis Ababa, Ethiopia kutayarisha ajenda za kikao cha
wakuu wa nchi hizo kilichofanyika nchini humo jana. Ajenda maalumu ya
kikao cha wakuu hao wa nchi ilikuwa kujadili uwezekano wa nchi hizo
kujitoa ICC iwapo kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na makamu
wake, William Ruto wanaokabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya
binadamu katika mahakama hiyo zisingefutwa au kuhamishiwa katika
mahakama za Kenya.
Sauti ya kwanza kusikika ikiwaonya wakuu hao wa
nchi wanachama wa AU dhidi ya kujitoa ICC, ilikuwa ya Katibu Mkuu
mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan ambaye alisema itakuwa
alama ya aibu kwa Bara la Afrika iwapo nchi hizo zitajitoa katika
Mkataba wa Roma ambao uliunda mahakama hiyo mwaka 2002 na kusema iwapo
watachukua hatua hiyo watakuwa wanajilinda wenyewe, huku waathirika wa
uhalifu dhidi ya binadamu wakikosa wa kuwatetea.
Akitoa mhadhara nchini Afrika Kusini, kiongozi
huyo mstaafu aliyeiongoza UN kati ya 1996 na 2006 na ambaye ni raia wa
Ghana alisema ni viongozi wachache tu wanaoipiga vita ICC na kuonya
kuwa, kujiondoa katika mahakama hiyo watakuwa wanalinda masilahi yao
binafsi na si ya Waafrika wote.
Alisema njama za viongozi hao kutaka kujiondoa ICC
ni ishara dhahiri kwamba Waafrika wana desturi ya kutoheshimu sheria,
huku akisema viongozi wanaokabiliwa na mashtaka katika ICC walipelekwa
huko kama watu binafsi na si Bara zima la Afrika kama inavyopotoshwa
makusudi.
Sauti ya pili iliyosikika ilikuwa ya Jaji Stephen
Bwana, raia wa Tanzania ambaye ameteuliwa majuzi kuwa jaji wa ICC,
ambaye amesema viongozi wa nchi za Afrika wanaotaka kujitoa kwenye
mahakama hiyo wana lengo la kuficha uovu uliopo katika nchi zao, kwani
baadhi yao wanajifanya miungu watu. Jaji huyo alisema hayo juzi baada ya
kuapishwa kuwa jaji wa ICC atakayesimamia kesi za uhalifu dhidi ya
binadamu nchini Cambodia. Kabla ya kuteuliwa na UN, Jaji Bwana alikuwa
Jaji wa Mahakama ya Rufani hapa nchini.
Jaji huyo alisema nchi za Afrika zikijiondoa ICC
ni kukubali udhaifu wetu na kuficha madudu yetu. Aliwashauri viongozi
makini wa Afrika wasijiondoe, kwani sababu zilizowafanya wajiunge na
ICC, ambayo alisema inatimiza wajibu wake bado zipo. Alikanusha vikali
madai kwamba mahakama hiyo inawalenga viongozi wa Afrika pekee.
Tumetumia muda mrefu makusudi ili Serikali ya Rais
Jakaya Kikwete iweze kupata ujumbe kutoka katika sauti za Waafrika hao
wawili wenye utumishi uliotukuka. Sauti hizo zinashauri nchi za Afrika
ziendelee kushirikiana na ICC na kuheshimu Mkataba wa Roma. Tunadhani
kuwa, pengine kitu ambacho sauti hizo zinasita kusema ni kwamba nchi
zitakazojitoa zitatengwa na jumuiya ya kimataifa.
SOURCE: BBC
SOURCE: BBC