Monday, 28 October 2013

Mwalimu Nyerere na mbwa wa Manzese!


 


Posted  Jumapili,Oktoba27  2013  saa 14:26 PM
Kwa ufupi
Binafsi najiona ni mtu huru. Na siku zote nimepigania nibaki kuwa mtu huru. Kwa uhuru kabisa nakutana na kuongea na watu wengi; vijijini na mijini. Nakutana na kuongea na wasomi na wasio wasomi, matajiri na maskini.

Watanzania tumeadhimisha miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Nyerere. Ulikuwa na unabaki kuwa wakati wa kuyakumbuka yale mema aliyoyafanya Mwalimu kwa nchi yetu. Mchango wake kwa taifa letu.
Ama hakika, Mwalimu alikuwa na kipaji cha kuongea na bingwa hasa wa simulizi. Hotuba zake ziliwavuta wengi. Nakumbuka, kuwa Mwalimu Nyerere alipata kusimulia kisa cha mbwa wa Manzese. Wakati huo nilikuwa bado kijana mdogo sana.
Hiyo ilikuwa ni mwanzoni mwa miaka ya 80. Ni kwenye kilele cha sherehe za Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi. Sherehe zile zilifanyika pale Uwanja wa Taifa. Nilibahatika kuwapo uwanjani.
Baadhi ya mabango ya wafanyakazi yaliyopita mbele ya Mwalimu siku ile yaliwakilisha ujumbe juu ya hali ngumu ya kimaisha iliyokuwa ikiwakabili wafanyakazi; mishahara midogo na mengineyo.
Wakati huo, Serikali ya Mwalimu ilikataa masharti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia(WB) pia. Hii ni kwa sababu, licha ya athari nyingine mbaya kwa masharti hayo kwa nchi yetu, uhuru wetu wa kujiamulia mambo yetu nao ulikuwa hatarini.
Ilipofika wakati wa kutoa hotuba yake, Mwalimu Nyerere alisema; “ Ndugu zangu watu wa Dari Salama ebu nisikilizeni; kulikuwa na mbwa wawili, mmoja wa Manzese na mwingine wa Oysterbay. Ikatokea siku moja mbwa wa Manzese akatembea hata akafika Oysterbay.
Kwenye moja ya nyumba za huko Oysterbay akamwona mbwa mwenzake aliye ndani ya geti. Mbwa yule wa Manzese akasogea getini huku akimshangaa mbwa wa Oysterbay. Mbwa yule wa Oysterbay alinenepeana huku manyoya yake yakiwa yameteremka hadi machoni. Mbwa wa Oysterbay naye alimshangaa mwenzake wa Manzese. Mbwa yule wa Manzese alionekana kukondeana, huku masikio yake yakiwa yameteremka hadi shingoni. Mbwa wa Oysterbay kwa mshangao akamwuliza mwenzake wa Manzese; “ Hivi nawe ni mbwa kama mimi?!
“Naam, miye ni mbwa kama wewe.” Alijibu mbwa wa Manzese. “ Sasa mbona umekondeana hivyo, njoo humu ndani kwa bwana wangu nawe uwe kama mimi.” Mbwa wa Manzese akajibu;
“ Lakini wewe umefungiwa, mwenzio niko huru!” Sitakisahau kamwe kisa kile alichosimulia Mwalimu Nyerere pale Uwanja wa Taifa. Naamini katika alichokisema Mwalimu, nitaendelea kuamini hivyo hata katika muda wangu uliobaki humu duniani. Mwalimu alizungumzia dhana ya uhuru. Ingawa ni neno fupi sana, lakini neno uhuru lina maana kubwa. Asiye na uhuru ni mtumwa.
Binafsi najiona ni mtu huru. Na siku zote nimepigania nibaki kuwa mtu huru. Kwa uhuru kabisa nakutana na kuongea na watu wengi; vijijini na mijini. Nakutana na kuongea na wasomi na wasio wasomi, matajiri na maskini. Nakutana na kuongea na watu wenye imani na itikadi tofauti.
Na wala sioni aibu kuweka bayana kuwa naamini katika itikadi ya kijamaa. Maana, ujamaa umejengwa katika misingi ya haki na usawa. Naamini, kuwa ujamaa na kujitegemea kama itikadi, bado ndiyo itikadi inayofaa kuongoza siasa ya nchi yetu. Bila shaka, ujamaa na kujitegemea unahitaji kufanyiwa marekebisho ya kimsingi ili uendane na wakati.
Simulizi ya Mwalimu juu ya ‘Mbwa wa Manzese’ imejengeka katika misingi ya ujamaa na kujitegemea. Taifa linalojitegemea linabaki siku zote kuwa taifa huru. Vivyohivyo , kwa mwanadamu. Binadamu anayejitegemea ni binadamu huru. Katika siasa lililo kubwa ni itikadi. Kama chama kinafuata itikadi ya kibepari, basi, kuahidi kutoa elimu na afya bure kunakinzana na misingi ya itikadi husika. Katika ubepari hakuna cha bure.

Ndiyo maana, Barack Obama alisakamwa na anaendelea kusakamwa na wenzake wa chama cha Republican, kuwa anataka kuwapeleka Wamarekani kwenye ujamaa. Ni pale Obama alipopigania kupitishwa muswada wa Huduma za Afya za bure kwa jamii. Hapa ina maana, kuna Wamarekani watakaolipa ili wenzao wanyonge wanufaike. Kwenye mfumo wa kibepari, kuna wanaoliangalia hili kwa macho ya shaka.
Katika itikadi ya kijamaa, huduma za kijamii kama vile elimu na afya ni kawaida kutolewa bure au kwa gharama nafuu sana. Fedha za kugharimia huduma hizo hutokana na kodi inayokusanywa kutokana na shughuli za uzalishaji. Wajamaa wanaamini katika kuwatoza kodi zaidi wenyenacho ili kuwamegea wasionacho.
Hapa kwetu vyama na wagombea wameshindwa kujipambanua katika itikadi. Mgombea anayetokea kwenye chama chenye sera za kibepari anasikika kama anatoka kwenye chama cha kijamaa na kinyume chake. Wakati mwingine unaingiwa shaka, kama kweli vyama vina itikadi zenye kueleweka. Inatokea pia, kuwa itikadi ya mgombea, mara nyingi haionekani wazi anapoongea. Kimsingi chama cha kisiasa chenye nguvu kinatokana na kazi ya timu iliyoandaliwa vyema. Siyo kazi ya mtu mmoja. Kielelezo cha nguvu na umakini wa chama cha kisiasa ni wingi na ubora wa makada wake. Chama ni makada kwa vile chama ni itikadi, malengo na shabaha na wala siyo nasaba na umaarufu wa mtu mmoja mmoja ndani ya chama.
Ni bahati mbaya sana siku hizi; unaposema au kuandika jambo kama nifanyavyo sasa, haraka kuna wanaokimbilia kutafuta kabati la kukupachika; CCM, CUF, CHADEMA, Dini, Kabila na mengineyo. Tumelisahau kabati muhimu sana, nalo ni kabati la Tanzania. Na hakika, katika kila tuyafanyayo, tutangulize kwanza masilahi ya nchi yetu.Nahitimisha.


SOURCE: MWANANCHI