Na Mussa Juma, Mwananchi
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 8:31 AM
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 8:31 AM
Kwa ufupi
Mwigamba asema kikao kilichomsimamisha hakina
mamlaka, adai chanzo ni kudaiwa kutumiwa na Zitto; Mnyika apigilia
msumari wa mwisho hukumu hiyo.
Arusha. Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amepinga uamuzi wa kusimamishwa kwa
maelezo kuwa kikao kilichochukua uamuzi huo hakitambuliki kikatiba huku
akikanusha tuhuma za kutumiwa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe,
kukisambaratisha chama hicho.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mwigamba alisema
kikao ambacho kina mamlaka ya kumwajibisha ni Kamati Kuu baada ya
kupokea tuhuma na kumsikiliza.
“Baraza la uongozi la Kanda halina mamlaka ya
kunisimamisha uenyekiti, lakini kwa kuwa mimi bado ni mwanachama hai wa
Chadema na sitahama Chadema, nitakaa pembeni ili chama kifanye uchunguzi
wa tuhuma zangu nikiwa nje ya ofisi,” alisema Mwigamba.
Hata hivyo, alisema anakusudia kufafanua chanzo
cha mgogoro wake na baadhi ya viongozi leo, baada ya kukabidhiwa
kompyuta mpakato (laptop) na viongozi wa chama hicho ambao waliichukua
ili kuifanyia uchunguzi.
Akana kutumiwa na Zitto
Akizungumzia tuhuma za muda mrefu kuwa, amekuwa
akitumiwa na Zitto hasa kuelekea uchaguzi ndani ya chama hicho,
alisema wanaofikiri hivyo ni vipofu wa kisiasa.
“Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa
nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu
yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa biashara, najua
ninachokifanya ni kwa masilahi ya chama,” alisema Mwigamba.
Alisema kama angekuwa mtu wa kutumiwa sasa,
angetumiwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye ana uwezo
wa kifedha kuliko Zitto au Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa ambaye atakuwa
mgombea wa urais wa chama hicho na ana uwezekano wa kushinda.
Alisema kabla ya tuhuma za sasa kwamba anatumiwa
na Zitto, aliwahi kutuhumiwa pia na Zitto kuwa anatuhumiwa na Mbowe hasa
kutokana na misimamo yake na kauli zake katika vikao na maeneo
mbalimbali, lakini baadaye ilithibitika kuwa alikuwa na hoja za msingi.
“Mimi ni mwanachama hai wa Chadema na nimekuwa
nikitoa maoni yangu si kama Mwenyekiti wa Chadema Mkoa. Nina uhuru wa
kutoa maoni katika kuhakikisha chama changu kinashika dola,” alisema
Mwigamba.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini,
Mchungaji Israel Natse alitangaza juzi kusimamishwa Mwigamba hasa
kutokana na tuhuma za kukichafua chama hicho kwenye mitandao ya kijamii.
Kabla ya hatua hiyo, Mwigamba alipata kipigo
kutoka kwa vijana wa Chadema baada ya kutuhumiwa kurusha kwenye mtandao
wa Jamii Forum tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ndani ya chama
hicho akiwa ndani ya kikao cha Baraza la viongozi Kanda ya Kaskazini.
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanaamini kuna uwezekano kuwa
mgogoro katika chama hicho unatokana na vuguvugu la uchaguzi uliosogezwa
mbele hadi mwakani.
Kuna wasiwasi huenda yakajirudia ya mwaka 2009
wakati Zitto alipojaribu kuwania nafasi ya Mwenyekiti dhidi ya Mbowe na
kuzua mvutano mkubwa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, Zitto aliweka bayana kuwa hawezi kuzungumzia mambo hayo kwani hafahamu hata huo uchaguzi wa ndani utafanyika lini.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mwenezi wa
Chadema, John Mnyika alifafanua kuwa kikao kilichomsimamisha Mwigamba
kilikuwa halali.
Mnyika alisema, hata hivyo, ikiwa Mwigamba
hajaridhishwa na hatua hiyo anapaswa kukata rufaa na siyo kulalamika
kwenye magazeti.
Alisema kuwa Mwigamba anapaswa kusoma katiba ya
chama hicho na kuelewa mambo ya chama yanamalizwa na kikao husika na
siyo kwenye vyombo vya habari.
“Kikao kile kinaweza kumsimamisha ila kama hajaridhishwa na uamuzi ule basi aende kwenye ngazi inayofuata,” alisema Mnyika.
Mnyika, hata hivyo, alisema kwa ngazi ya taifa
wanasubiri taarifa ya kikao kilichomsimamisha kwani walikuwa hawajapokea
na wala kutumiwa malalamiko yoyote na Mwigamba.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI