Na Anthony Mayunga, Mwananchi
Posted Jumapili,Oktoba27 2013 saa 7:39 AM
Posted Jumapili,Oktoba27 2013 saa 7:39 AM
Kwa ufupi
Polisi wawili wa Kitengo cha Upelelezi katika
Kituo cha Polisi Mugumu wilayani Serengeti wakishirikiana na raia
wawili, wamekamatwa na kikosi maalumu cha ‘Okoa Maliasili’ wakijaribu
kuuza jino moja la tembo.
Serengeti. Polisi wawili wa
Kitengo cha Upelelezi katika Kituo cha Polisi Mugumu wilayani Serengeti
wakishirikiana na raia wawili, wamekamatwa na kikosi maalumu cha ‘Okoa
Maliasili’ wakijaribu kuuza jino moja la tembo.
Kukamatwa kwa askari hao kumethibitishwa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Fernandi Mtui ambaye alidai si msemaji
wa operesheni hiyo na kuwa anaendelea kufuatilia kwa kuwa wamepelekwa
kwenye kambi maalumu inayotumiwa na kikosi hicho.
“Kwa kweli sijajua kwa undani ilivyotokea,
naendelea kufuatilia maana hawako kwetu hao. Kama itabainika kuwa
walihusika ama walikuwa kwenye kazi ya kusaidia kukamatwa kwa watuhumiwa
lazima itakuwa wazi. Haya mambo hakuna kitakachofichwa”alisema kamanda.
Taarifa zilizolifika gazeti hili kutoka katika
vyanzo vya uhakika, askari hao waliotajwa kwa jina moja moja la Koplo
Isaack na Sixbert wa Idara ya Upelelezi walikamatwa Oktoba 25, kati ya
saa 4-5 usiku eneo la Sedeco mjini Mugumu baada ya kuwekwa mtego
maalumu.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo polisi
zinadai kuwa askari hao wakiwa na gari aina ya Toyota Corolla yenye
namba za usajili T269 BRN mali ya Sixbert walifika eneo hilo na jino
hilo kwa ajili ya kuuza wakiwa na raia wawili ambao majina yao
hayajajulikana ndipo wakanaswa.
Habari hizo zilisema baada ya kukamatwa watuhumiwa
wote pamoja na gari walichukuliwa na kupelekwa eneo la Andajenga
lililomo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambako kikosi hicho kina
kambi maalumu.
Hata hivyo kuna habari zinasema kuwa kukamatwa kwa
askari hao kunatokana na kuwapo kwa taarifa za kuhusika na biashara
hiyo kwa kuuza vielelezo mbalimbali vinavyokamatwa na kuhifadhiwa
polisi.
Tuhuma za askari polisi kujihusisha na mitandao ya
ujangili kwa wilayani Serengeti zimekuwa nyingi huku baadhi ya taasisi
zikibainisha ugumu wa kuwakamata watuhumiwa kwa kuwa hupewa taarifa
mapema na askari walioko kwenye mtandao huo na kukimbia.
Mwanzoni mwa mwaka huu askari polisi wawili kutoka
Mkoa wa Kagera walikamatwa wilayani Serengeti wakiwa na meno ya tembo
kilo 18 wakidaiwa kutumiwa na mfanyabiashara kutoka
Biharamulo,walifukuzwa kazi na kesi iko mahakamani.
Kukamatwa kwao hao kunafanya idadi ya askari
waliokamatwa na operesheni hiyo kufikia wanne ,wawili wakiwa idara ya
wanyamapori wa halmashauri hiyo.
Askari hao akiwemo Kaimu Afisa Wanyamapori Wilaya,
Cathbert Boma ambaye alikutwa na meno ya tembo ofisini na Omary
Rutiginga ambaye anadaiwa kukutwa na kipande cha nyama ya ngiri.
Wote wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Bunda ambako walipewa dhamana.
SOURCE: MWANANCHI