Tuesday, 29 October 2013

‘Tumewabaini wahujumu’


Na Peter saramba, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Oktoba28  2013  saa 22:1 PM
Kwa ufupi
Ni Chadema wakidai kubaini mtandao wa wanaokihujumu chama hicho.


Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kugundua mtandao mkubwa wa wanachama na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho wanaoshirikiana na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha aliyesimamishwa, Samson Mwigamba kupanga njama za kukihujumu Chadema.
Akizungumza kwa tahadhari, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mwigamba pamoja na baadhi ya viongozi wameunda mtandao mpana ambao lengo lake siyo jema kwa afya na masilahi ya Chadema.
Kauli ya Golugwa inaungwa mkono na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye anadai Mwigamba ni mbuzi wa kafara anayetumika kufanikisha malengo ya watu waliojificha nyuma yake.
Golugwa alisema baada ya kugundua maovu mengi yaliyotendwa na Mwigamba, Chadema haitajibizana naye na tayari baraza la viongozi la mkoa limeridhia uamuzi wa kumsimamisha uongozi na ilitarajia kumkabidhi barua yake jana jioni kabla ya kufikisha uamuzi huo kwa kamati kuu kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake, Mwigamba jana alikutana na waandishi wa habari jijini Arusha na kukiri kuandika andiko linaloelezea udhaifu wa kiuongozi ndani ya chama hicho, lakini akiapa kumalizia maisha yake kisiasa ndani ya Chadema.
Licha ya kusisitiza kukipenda Chadema, Mwigamba alimtupia lawama Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kuwa ndiye kiini cha maswahibu yanayomkuta kutokana na kuhofia nafasi yake ya ubunge.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mwigamba alisema bado anaamini yote aliyoyaandika kwenye mitandao atayatetea kwa sababu ndiyo ukweli.
“Kwanza kabisa nasema bila kumung’unya maneno kwamba nilimaanisha nilichokiandika (kwenye mtandao) na nilikuwa sibahatishi kwamba kuna udhaifu mkubwa katika mfumo wa uendeshaji wa chama ambao vikao rasmi vimeshindwa kushughulikia,” alisema Mwigamba
Alirejea hoja yake kuwa baadhi ya viongozi wamechakachua Ibara ya 6.3.2, kipengele C ya katiba ya Chadema kinachozungumzia ukomo wa uongozi kwa kiongozi aliyeshikilia nafasi moja kwa vipindi viwili mfululizo.

SOURCE: MWANANCHI