Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 10:22 AM
Kwa ufupi
Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda,
alipoulizwa na Mwananchi jana, alisema kuwa hana taarifa za kuwapo
mpango wa kumng’oa mwenyekiti wake kama inavyoelezwa.
Dodoma na Zanzibar. Baraza Kuu
la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) linakutana leo jini
Dodoma huku hatma ya Mwenyekiti wa umoja huo, Sadifa Hamisi Juma ikiwa
mashakani.
Mkutano huo wa baraza ulitanguliwa na kikao cha
Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM kilichokaa jana jioni mjini Dodoma kwenye
Ukumbi wa White House ambako ni makao makuu ya CCM.
Sadifa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge,
analalamikiwa kutokana na matatizo mbalimbali ya kiutawala, matumizi
mabaya ya fedha na usimamizi mbovu wa mali za chama hicho.
Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa vuguvugu la
kumng’oa, Sadifa alijibu kwa kifupi tu; “Asante Nashukuru.” “Ninaambiwa
nimekuwa mtu wa kutukana watu, nimemtukana nani? Asante
Nashukuru.,”aliongeza Sadifa hata pale mwandishi alipomuuliza kwa zaidi
ya mara tatu aliishia kutoa jibu: “Asante nashukuru.”
Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda,
alipoulizwa na Mwananchi jana, alisema kuwa hana taarifa za kuwapo
mpango wa kumng’oa mwenyekiti wake kama inavyoelezwa.
“Sikiliza, mimi ndiye Mtendaji Mkuu wa UVCCM,
ajenda za mkutano, sisi kama sekretarieti tumeshaziandaa na hakuna
agenda kama hiyo. Umoja huu unaendeshwa kwa kanuni na taratibu,”alisema
Mapunda.
Mapunda aliyechukua mikoba hiyo Agosti mwaka huu,
alipoulizwa kuhusu mkutano huo kugharamiwa na CCM makao makuu badala ya
Jumuiya yenyewe, alikanusha taarifa zilizozagaa akisema: “Mimi ndiye
niliyeitisha mkutano huu, sasa chama kinatoka wapi?”
Mjumbe aanika madudu ya UVCCM
Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Ruvuma, Alex
Nchimbi alifafanua hakuna njama za kumtoa ila mambo anayotakiwa
kurekebisha ndio yanaweza kumtoa.
Nchimbi alisema kuwa UVCCM inakabiliwa na tatizo
la matumizi mabaya ya fedha na kibaya zaidi hesabu za chama hicho
hazijakaguliwa kwa muda mrefu.
Alisema jumuiiya hiyo hupata kiasi cha Sh80
milioni kutokana na miradi mbalimbali kama jengo lililoko makao makuu ya
UVCCM, lakini fedha hizo zinafujwa.
“Ila utashangaa kaka yaani zile fedha
zinavyofujwa. Hadi kwa mwezi jumuiya inabakiwa na Sh8 milioni au wakati
mwingine hadi Sh6milioni,” aliongeza Nchimbi.
Nchimbi aliongeza tatizo jingine ni uteuzi wa viongozi bila kufuata taratibu.
Alisema kuwa Sadifa aliteua sekretarieti kabla ya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ambapo ni kinyume na utaratibu.
Alitaja viongozi hao kuwa ni Mkuu wa Idara ya
Uchumi na Fedha, Omar Suleimani, Mkuu wa Chipukizi na Uhamasishaji, Omar
Justus na Tumaini Mwakasege, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa
Oganaizesheni.
“Umoja wetu una pikipiki 10, lakini kapeleka
pikipiki mbili Morogoro na nane kazipeleka Zanzibar kwenye jimbo lake.
Ukichunguza uandikishaji wake utagundua bado zinamilikiwa na UVCCM”,
alisema Nchimbi.
Nchimbi pia alimtuhumu Sadifa kwa kuanzisha nafasi za makatibu wasaidizi wa mikoa bila ya baraka za Baraza Kuu.
“Hivi nani angewalipa watu hawa. Lazima tujiulize
UVCCM ina fedha gani za kuwalipa makatibu wa mikoa na wasaidizi?,”
alisema Nchimbi
Wanataka UVCCM izaliwe upya
Nchimbi alisema UVCCM wanakabiliwa na changamoto
ya kusafisha uoza ndani ya jumuiya na hasa kwa kuzingatia kuwa Sadifa
anatoka Zanzibar.
“Kwa hali ya kawaida, kama si kulindwa na wazee
kwa hoja za kulinda Muungano na amani katika jumuiya na kuelekea
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa basi tusingekuwa naye,” alisema Nchimbi.
Nchimbi, hata hivyo, alionya kuwa uongozi wa
vijana uliopo usiporekebishwa hawawezi kumsaidia balozi wa nyumba 10
kushinda uchaguzi
Jaribio la pili kumtoa Sadifa
SOURCE: MWANANCHI
Mpango huo wa kumtimua Sadifa ni wa pili ndani ya siku
zisizozidi 60 baada ya awali kuibuka mvutano mkubwa ndani ya jumuiya
hiyo, kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja huo
kudhamiria kumng’oa madarakani mwenyekiti huyo.
Mgogoro huo ulisababisha kikao cha Baraza Kuu
kilichokuwa kikifanyika Zanzibar, ambacho mgeni rasmi alikuwa Makamu wa
Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali
Iddi na baadhi ya wajumbe kumtaka Sadifa na Kamati yake ya Utekelezaji
kutoka nje ili wajadiliwe kwa kukiuka kanuni.
Aking’olewa Sadifa, itakuwa mara ya pili kwa
mwanachama wa Jumuiya hiyo kutoka Zanzibar kung’olewa baada ya Masauni
Yussuf Hamad kung’olewa mwaka 2010 kwa tuhuma za kughushi umri.
SOURCE: MWANANCHI