Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 8:15 AM
Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya
Vijana wa CCM (UVCCM), wameanza kupanga upya mikakati ya kuwang’oa
viongozi wa juu wa jumuiya hiyo baada ya kushindwa kwa mpango uliokuwa
umepangwa kutekelezwa wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika
juzi mjini Dodoma.
Wanamapinduzi walikuwa wamepanga kuwatoa
madarakani Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis na makamu wake, Mboni
Muhita, lakini jaribio hilo
lilishindwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni
wahusika kutojipanga vizuri, pia uwapo wa Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana katika mkutano huo.
Kinana anatajwa kukwamisha mapinduzi
yaliyokusudiwa kutokana na kauli yake aliyoitoa wakati akifungua mkutano
huo kwamba haukuwa kwa ajili ya kuibomoa jumuiya bali kuijenga, hali
ambayo iliwafanya wajumbe waliokuwa na ajenda ya kumng’oa mwenyekiti
kunywea.
Hata hivyo, jana gazeti hili lilielezwa kuwa
baadhi ya wajumbe hawakuridhika na hatua ya kutokujadiliwa kwa hali
ilivyo ndani ya UVCCM, hivyo wameamua kujipanga upya ili kutekeleza azma
yao ya kuwasulubu viongozi wao katika mkutano ujao.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho alisema kumekuwa
na woga unaowafanya viongozi wa juu wa UVCCM kutoruhusu kuwapo kwa
ajenda zaidi ya moja katika vikao vya Baraza Kuu na kwamba huo ni
utumiaji mbovu wa rasilimali za jumuiya.
“Kikao kimoja cha baraza kinagharimu zaidi ya Sh60
milioni, lakini mwaka huu pekee tumefanya vikao vitatu kwa hiyo
tumetumia zaidi ya Sh180 milioni. Fedha hizi zingeweza kugharimia mambo
mengine kama uhaba wa kadi na kanuni za jumuiya kwenye ngazi za chini,”
alisema mmoja wa wajumbe kutoka mikoa ya Kanda ya Kati, huku akiomba
jina lake lihifadhiwe.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo,
kikao cha Baraza Kuu kinapaswa kuwa kimoja kwa mwaka, lakini mwaka huu
tayari wamefanya vikao vitatu ambavyo kimsingi havina tija kwani hakuna
kilichojadiliwa kutokana na woga wa viongozi.
Mjumbe mwingine kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini
alisema jumuiya imeshindwa kuteua makamanda wa wilaya na mikoa kwa muda
mrefu, pia kutofanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za chipukizi katika
ngazi za wilaya na mikoa.
“Mwakani tunakabiliwa na Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, lakini cha ajabu hadi sasa tuna viporo vingi, mikutano kama hii
ingetumika kufanya kazi hizo badala ya kujadili ajenda moja tu kama
tulivyofanya Zanzibar mwezi uliopita na jana (juzi) hapa Dodoma,”
alisema.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda
akijibu hoja hiyo alisema: “Uhai wa jumuiya ni vikao, kwa hiyo siyo kosa
kufanya vikao hata kama vitakuwa ni zaidi ya 10 kwa sababu katika vikao
ndiko mambo muhimu yanakojadiliwa”.
Kuhusu uteuzi wa makamanda wa vijana wa wilaya na
mikoa, Mapunda alisema kazi hiyo ilifanyika na kukamilika juzi katika
kikao cha Kamati ya Utekelezaji cha jumuiya hiyo na kwamba suala la
wagombea wa chipukizi nalo litakamilishwa.
SOURCE: MWANANCHI
Sarakasi za Sadifa
Uchambuzi wa kisiasa unaonyesha kuwa Sadifa
alifanya mambo mawili makubwa katika kuwakabili wapinzani wake waliokuwa
wamenuia kumng’oa katika nafasi yake.
Kwanza alikesha akiomba radhi katika vikao
vilivyowahusisha wenyeviti wa UVCCM wa mikoa na baadaye wajumbe wengine
wa Baraza Kuu na pili ni hatua yake ya kumteua hasimu wake kisiasa, Paul
Makonda kuwa mmoja wa wakuu wa idara za umoja huo.
Wakati huo huo, Baraza la UVCCM, limeitaka
Serikali kurejesha bungeni kwa hati ya dharura muswada wa marekebisho ya
tozo ya Sh1000 kwa kila kadi ya simu.
Mapunda akizungumza na na waandishi wa habari jana
alisema “Lengo ni kufanikisha malengo ya kufikisha mawasiliano ya simu
kwa Watanzania wengi kwa haraka”.
Tozo hiyo ya Sh1000 kwa kila kadi ya simu,
imetokana na sheria mpya ya fedha ya mwaka huu iliyopitishwa na Bunge .
Hatua hiyo ya Serikali inalenga kukusanya Sh 178 bilioni katika Bajeti
ya 2013/2014.
SOURCE: MWANANCHI