Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumapili,Septemba15 2013 saa 2:2 AM
Posted Jumapili,Septemba15 2013 saa 2:2 AM
Kwa ufupi
Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amefanya
ziara mkoani Tabora na kusimikwa kuwa Mtemi wa Unyanyembe na mlezi wa
watemi akisema watemi na wakuu wengine wa kimila wana nafasi kubwa
kuzuia mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Lowassa jana alikuwa mgeni rasmi katika
maadhimisho ya miaka 124 ya Shujaa wa Unyanyembe, Mtemi Isike Mwana
Kiyungi, yaliyofanyika mkoani Tabora anapotokea Sitta ambaye ni Waziri
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Lowassa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa mnara
wa kumbukumbu ya Isike. Tukio hilo la kuwa mgeni rasmi na kusimikwa kuwa
mtemi ndani ya mkoa huo ulio asili na makazi yake Sitta linaweza
kutafsiriwa kisiasa kuwa sawa na Lowassa kuvamia ngome ya mwanasiasa
huyo mkongwe.
Sitta na Lowassa wote wanatajwa kutaka kuwania
urais wa Tanzania huku kila mmoja akielezwa kuwa na kambi yake ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa pia na jimbo lake la uchaguzi pamoja na
ngome yake kisiasa. (Mwandishi Wetu)
, Mwananchi
Wakati Lowassa ni mbunge wa Monduli mkoani Arusha,
Sitta ni mbunge wa Urambo Mashariki, mkoani Tabora, wote wakiwahi
kushika nyadhifa za juu kitaifa ambapo Lowassa aliwahi kuwa Waziri Mkuu
na baadaye kujiuzulu, wakati huo Sitta akiwa Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo Lowassa alisema:
“Hawa machifu wanaweza kusaidia tatizo hili, Mimi kule kwetu Monduli ni
Laigwanan mkuu.., kuna wakati maambukizi ya Ukimwi yalikuwa makubwa kwa
Wamasai, nikawaita Malaigwanan wezangu nikawaomba waondoe baadhi ya mila
zinazochangia hali ile. Tukakubaliana na kupita kijiji kwa kijiji
kuelezea na kweli ikaleta mafanikio makubwa, maambukizi yale
yakapungua.”
Aidha, Lowassa alipongeza hatua ya kuenzi
kumbukumbu hiyo na kusema kuwa kizazi cha sasa kina kila sababu ya kuiga
mfano wa Mtemi Isike wa kutetea utu wake huku akiwataka pia wakazi wa
Tabora kuwekeza katika mkoa huo aliouelezea kuwa wa kitalii kutokana na
historia yake.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika Kijiji cha
Itetemia ilipo Ikulu ya Mtemi huyo wa Unyanyembe, aliyepigana dhidi ya
majeshi Mjerumani, Von prince(Mwana Sakaraga) kuanzia mwaka 1889 hadi
1893.
SOURCE: MWANANCHI