Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Posted Jumapili,Septemba29 2013 saa 1:0 AM
Posted Jumapili,Septemba29 2013 saa 1:0 AM
Kwa ufupi
Maazimio hayo yametangazwa na kamati hiyo
pamoja na Baraza la Katiba Zanzibar (Bakaza) katika mkutano na waandishi
wa habari uliofanyika huko Shangani mjini Zanzibar jana.
Zanzibar. Kamati ya Maridhiano
Zanzibar imetangaza maazimio sita inayotaka yazingatiwe katika mchakato
wa Katiba Mpya kabla ya Bunge la Katiba kujadili rasimu ya mwisho na
kupigwa kwa kura ya maoni mwakani.
Maazimio hayo yametangazwa na kamati hiyo pamoja
na Baraza la Katiba Zanzibar (Bakaza) katika mkutano na waandishi wa
habari uliofanyika huko Shangani mjini Zanzibar jana.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Nassor Moyo,
alisema kwamba marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanywa na Serikali na
kupitishwa na Bunge kibabe yana upungufu mkubwa katika utaratibu wa
kuandaa muswada huo na uchukuaji wa maoni yake.
Alisema kuwa kabla Rais Kikwete hajasaini muswada
huo, wadau kutoka Zanzibar wapewe nafasi ya kutoa maoni yao kisha
urudishwe upya bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa kwa manufaa ya pande
mbili za Muungano – Tanganyika na Zanzibar.
Alifafanua kuwa kifungu kinachotoa nafasi kwa
wabunge wa Bunge la Katiba kupitisha Katiba kwa wingi wa kura ikiwapo
theluthi mbili zitashindikana kupatikana mara mbili, kifutwe, badala
yake utaratibu wa awali wa kupitisha kwa kupata theluthi mbili kila
upande utumike.
Mambo mengine yaliyopendekezwa na kamati hiyo, ni
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wawe idadi sawa baina ya Zanzibar na
Tanzania Bara kwa sababu Katiba Mpya inayoandaliwa ni ya Jamhuri ya
Muungano unaotokana na washirika hao wawili, ambao walikuwa na sifa sawa
kabla ya muungano huo mwaka 1964.
Moyo alisema pia kuwa wajumbe 166 wa Bunge la
Katiba kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na asasi za kiraia
wachaguliwe na makundi na Taasisi zenyewe, badala ya kazi hiyo kufanywa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Rais wa
Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kuwa Kamati yake inaunga mkono
ushauri wa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba, wa kutaka viongozi wa kisiasa na makundi ya kijamii kukaa
pamoja kuzungumzia mvutano uliojitokeza baada ya kufanyika kwa
marekebisho ya muswada huo.
Upande wake Mwenyekiti wa Bakaza, Profesa Abdul
Shariff alisema kuwa muundo wa Bunge la Katiba una walakini na kutaka
uangaliwe upya kutokana na chama kimoja cha siasa kuwa na uwakilishi wa
asilimia 72 katika Bunge la Katiba, jambo alilosema linaweza kuathiri
upatikanaji wa Katiba inayozingatia matakwa ya masilahi ya wananchi.
“Bakaza tunapendekeza wabunge wa Bunge Maalumu
wangechaguliwa na wananchi kwa kazi maalumu ya kuandika katiba tu ili
kupata ridhaa ya wananchi kuhusu aina ya Katiba wanayoitaka wakati huu,”
alisisitiza Profesa Shariff.
Alisema kuwa haikuwa sahihi kwa Zanzibar kunufaika
na theluthi moja kati ya wajumbe 166 ambao watateuliwa kutoka katika
makundi ya kijamii na asasi za kiraia, akitaka kila upande wa Muungano
utoe idadi sawa bila ya kuzingatia udogo wa ardhi, uchumi au idadi ya
watu baina ya pande mbili za Muungano.
Mkutano huo uliudhuriwa na Katibu Mtendaji wa
Kamati ya Maridhiano, Ismail Jussa Ladhu, ambaye alisisitiza umuhimu wa
amani na umoja wa kitaifa wakati huu wa mjadala wa kupata Katiba Mpya
kwa wananchi.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI