Monday, 30 September 2013

Binti afa kwa kumwagiwa maji ya moto na bibi yake


29th September 213
 
Kisa alichelewesha mwiko wa kusongea ugali

Mtoto mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Zuhura (6), mkazi wa Lulumba, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, amefariki dunia baada ya kumwagiwa maji ya moto na bibi yake.


Imedaiwa kuwa bibi huyo, Magreth Sombi (55), alimmwagia mtoto huyo maji ya moto baada ya kuchelewa kumpelekea mwiko wa kusongea ugali aliomtuma.

Akielezea kisa hicho, Mwenyekiti wa mtaa huo, Abel Seth, alisema tukio hilo lilitokea Jumanne iliyopita.

Alisema bibi huyo anadaiwa kumtuma mtoto huyo mwiko na alipochelewa alimmwagiwa mwilini maji ya moto yaliyokuwa yamechemka kwa ajili ya kupikia ugali.

"Kama haikutosha, Magreth kwa ushirikiano na mtoto wake, Naomi walimkamata kwa nguvu Zuhura na kutumbukiza viganja vyake vyote ndani ya sufuria iliyokuwa na maji yaliyochemka...mtoto aliungua sana na nyama zote kutoka..." alisema kwa masikitiko.

Aliongeza kuwa binti huyo alifariki dunia kesho yake (Septemba 25) wakati akipatiwa tiba katika hospitali ya wilaya ya Iramba.

Alisema baada ya binti huyo kufariki, Magreth alimtuma mtoto wake aliyemtaja kwa jina la Naomi kwenda nyumbani kwa mwenyekiti huyo kutoa taarifa ya kifo hicho bila ya kutoa taarifa kwa majirani wanaowazunguka.

"Nilipomhoji ni kwanini hajawajulisha majirani zao juu ya kifo hicho, alinionya kuwa nisiwaambie watu wengine wala majirani kwa sababu hataki watu wajue au waje warundikane kwake eti mwili wa Zuhura utachukuliwa na wazazi wake kwenda kuzikwa Singida mjini wakati wowote," alisema Seth.
Mmoja wa majirani wa karibu katika msiba huo, Elieza Mgwali, alisema msichana huyo ambaye ana miezi miwili tangu aanze kuishi na bibi yake alikuwa na wakati mgumu kutokana na mateso makubwa aliyokuwa anapata kutoka kwa mtuhumiwa Magreth.

"Mtoto ameteseka sana, alifanyishwa kazi nzito zilizo nje ya uwezo wake na mara nyingi alikuwa akinyimwa hata chakula...alikuwa anakuja kwetu na moja kwa moja anaingia jikoni kujichukulia chakula bila hata kuomba, tulishatambua mateso yake hivyo tulikuwa tunamruhusu ale mpaka ashibe," alisema Mgwali.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa huo, mtuhumiwa Magreth na mwanawe Naomi wanashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo.

Jeshi la polisi Mkoa wa Singida kupitia kamanda wake, Geofrey Kamwela, amekiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba taarifa kamili anatarajia kuitoa kwa wanahabari wakati wowote.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI