Monday, 30 September 2013

HEKAYA ZA MLEVI: Mganga: Napasisha wanafunzi

Posted  Septemba28  2013 
Kwa ufupi
“Napasisha Wajinga, Naunganisha mtandao wa Freemason, Natoa kozi ya Ubunge.” Lakini ningependa jamii itambue kuwa huwezi kujua maana ya kitabu kwa kusoma jina lake tu, ni lazima ukisome kitabu hicho zaidi ya mara moja. Huwezi kuelewa maana ya makala hii kwa kichwa chake tu.
 

Hali ya maisha inazidi kuwa ngumu. Jiko limenuna hadi mamaake paka kalala juu ya jivu, katikati ya mafiga. Asubuhi nimsalimiapo Bibi Mlevi anaitikia huku macho yake yakigota katikati ya mboni ya jicho langu. Kwangu kitendo hicho kina tafsiri ya swali; “We mwanamume mbona sikuelewi?”
Kwa sababu tupo duniani kupambana na changamoto za dunia, nikaanza kutumia muda mrefu kutafakari namna ya kurudisha heshima inayoanza kutepeta nyumbani. Uzuri wa imani yangu ni kuwa “Mlango mmoja ukifungika, mwingine unafunguka.
Nikasoma alama za nyakati na kugundua kuwa Elimu yetu inaaga dunia. Kadiri matokeo ya mtihani yanapokaribia kutoka, asilimia ya machizi, wezi, wabwia unga na makahaba inaongezeka. Nikaamini naweza kufanya ‘Huduma ya Ualimu na Ushauri Mbadala’ itakayoiokoa jamii yangu na kuniongezea kipato. Nikapachika bango juu ya mlango: “Nafundisha Pre-form One, Tuition n.k.”
Mtalaa wangu ni rahisi sana: kuwatayarishia vijana maisha bora baada ya kuibuka na divisheni ziro. Kwanza waijue nchi yao sawasawa; Kwamba hii ni moja ya nchi za dunia zenye maajabu ya kipekee. Kwa uchache sana tuna Mlima Kilimanjaro, Kreta ya Ngorongoro na madini ya Tanzanaiti.

 Hivi havipatikani popote ulimwenguni isipokuwa katika kanchi haka kenye amani iliyopitiliza.
Unaona sasa? Ninapoitaja kuwa ni nchi ya amani, wote mnakasirika. Siyo nchi ya amani, ni nchi ya amani iliyopitiliza. Wala tusibishane, nenda ulimwenguni kote, kaulize unakopatikana Mlima Kilimanjaro utaambiwa Kenya. Lakini kwa amani yetu tumejituliza kama kasuku asiyependa matata.
Kaulize ni wapi inakochimbwa Tanzanaiti utajibiwa ni Afrika Kusini. Lakini wenyewe tumetulia tuli tukiwaacha washadadie maliasili zetu.

Tumetulia kama mshumaa unaowaka huku ukiteketea, au mgomba unaokatwa na kuuawa mara tu baada ya kuzaa. Si sawa na Wamalawi waliokuja juu wakitudai mpaka wa Ziwa Nyasa. Hii ni amani iliyopitiliza.
Hata hivyo, tangazo langu halikufanya vizuri kwa sababu ati sikukidhi viwango. Mtaalamu mmoja aliniponda kuwa twisheni pekee haiwezi kumtoa mtu udenda. Ati ningeandika “Napasisha Wajinga, Naunganisha mtandao wa Freemason, Natoa kozi ya Ubunge.” Lakini ningependa jamii itambue kuwa huwezi kujua maana ya kitabu kwa kusoma jina lake tu, ni lazima ukisome kitabu hicho zaidi ya mara moja. Huwezi kuelewa maana ya makala haya kwa kichwa chake tu.
 
Nataka wanafunzi wangu waelewe kusoma si kufaulu mtihani, bali ni kuongeza maarifa juu ya changamoto za maisha. Maisha yanapatikana popote, na yanakuwa bora kama utayaishi kwa sayansi za maisha. Kwamba kama unataka kuwa mwanasiasa ukubali kufa zaidi ya mara moja. Ile nayo ni Elimu na mnaona jinsi wanasiasa wanavyoishi maisha tofauti na wao wenyewe. 

Mmoja alidai kuwa hawezi kukikihama chama chake kipenzi kabla hajamuoa mama yake mzazi. Kwa mshituko wa wengi alikihama chama hicho; alipoulizwa kama alishaifunga ndoa ile alitangaza kuwa mama yake alikwisha kufariki! Huko ndiko kufa mara mbili.
Wanafunzi wangu wataelewa kuwa wingi wa vyama vya siasa si upana wa demokrasia. Pia utitiri wa Shule si ukomavu wa Elimu. Nitawakumbusha jinsi wazazi tulivyomwaga machozi baada ya wenetu kukosa nafasi (msiseme kufeli) katika shule chache za Serikali. Lakini hivi leo mzazi anakwenda kumwondoa mtoto kwenye Shule nyingi za Serikali na kumpeleka kwenye shule binafsi.
Nadhani hili lilikuwa jibu la watoto kulazimishwa kuchora sawaka kwenye karatasi ya mtihani. Jibu la yule aliyeongoza kutoka kidato cha kwanza kupata divisheni yai, na huyu asiyejua kuandika hata jina lake kupata daraja ya juu. Hilo nalo nitaliingiza kwenye maajabu yasiyo na idadi ya Tanzania; Msitu wa Amani.
Tanzania ndiyo nchi yenye Utawala Bora wa Sheria. Mambo mengine bado yapo kwenye utafiti na utafiti ukikamilika hamtapewa matokeo. Ila msije mkalalamika kwa nini anayeiba Ma-trilioni anahamishiwa ubalozini, na anayeiba kuku anapigwa moto. Msiandamane. Acheni kwanza tume zijisikie kujiunda na matokeo yahifadhiwe kwenye makabati yenye lakiri. Pengine ghorofa litaanguka na tutayaokota matokeo hayo kule Jangwani, katikati ya vifusi.
Hiyo ndiyo habari, na siyo tangazo. Namtazama kwanza Bibi Mlevi; kama jicho analonikodolea likianza kuwa jekundu nitakaribisha maombi ya fomu mara moja kwa gharama nitakayoipanga. Kama jeuri itaisha na heshima kunirudia basi tutasubiri. Alamsiki.

SOURCE: MWANANCHI