29th September 2013
Inaweza ikadhaniwa kuwa vitendo vya kigaidi
vilivyofanyika maeneo ya kibiashara ya Westgate jijini Nairobi huko
Kenya kuanzia wiki iliyopita, vinawahusu wananchi wa Nairobi na
vitongoji vyake tu.
Ukweli ni kwamba mauaji yaliyotokea katika
eneo la kituo cha biashara cha Westgate chenye mtandao wa biashara
kimataifa, yaliwagusa hata raia wa nchi mbalimbali akiwamo mmoja
aliyefahamika kwa jina la Vedasrus Nsanzungwanko wa kutoka Tanzania,
ambaye taarifa zilisema alijeruhiwa kwa risasi mguuni.
Shambulizi la Westgate, pamoja na ukweli
kwamba kikundi cha al Shabaab, chenye uhusiano wa karibu na al Qaeda
kinadai kuhusika, bado mtandao wa maharamia hao haujajulikana kama
umelenga kufanya nini baada ya shambulizi la Westgate.
Bado akilini mwa wengi hayajasahaulika
mashambulizi yaliyowahi kufanywa kwa wakati mmoja na kikundi cha al
Queda katika majengo ya balozi za Marekani jijini Dar es Salaam na
Nairobi tarehe 17 Agosti 1998 ambapo yalisababisha hasara ya vitu pamoja
na mauaji ya raia zaidi ya 200.
Waasi hao wa Kiislamu, walitamka wazi kuwa
shambulizi hilo, lilikuwa ni la kulipiza kisasi kwa hatua ya Kenya ya
kupeleka vikosi vyake nchini Somalia mwaka 2011 kwa ajili ya kupambana
nao. Msemaji wao pia alisisitiza kupitia televisheni kuwa watu kutoka
Magharibi hawatakuwa salama nchini Kenya hadi hapo nchi hiyo
itakapoyatoa majeshi yake nchini Somalia.
Msemaji wa al Qaeda aliendelea kutishia
kupitia mtandao wao mpya wa Twitter kuwa “Wakenya wana damu viganjani
mwao. Yeyote aliye tayari kuja Kenya anapaswa kujiandaa kukabiliana na
hali halisi".
Akasema tena 'Hatuogopi watu kutoka Ulaya
na Marekani kwa sababu sisi si dhaifu, na tunawaambia hao wazungu kwamba
yeyote ambaye amekuwa akisaidia waliokuwa wakitushambulia, waambieni
Wakenya kuacha mashambulizi yao kama wanataka kubaki salama."
Tukio hilo la ugaidi, ambalo, limefanyika
nyakati za mchana kukiwa kweupe katika viunga vya jumba la kibiashara
la Westgate huko Nairobi, kwa mara nyingine ni kama limeziweka nchi za
Afrika Mashariki kuwa tishio kubwa kwa mashambulizi zaidi.
Kutokana na uzoefu wa mashambulizi ya aina
hiyo, Nairobi pamoja na miji mingine mikubwa ya Afrika Mashariki
yanaweza kuwa yamelengwa kuhujumiwa kwa nyakati tofauti. Wao al Qaeda
wanafahamu kuwa shambulio hili limezigusa nchi wanachama wa Afrika
Mashariki na kwamba hawawezi kubakia kimya.
Inafahamika wazi kuwa karibia watu 70
walipoteza maisha wakati wengine zaidi ya 250 wakijeruhiwa katika
shambulio hilo baya zaidi ambalo halijawahi kutokea miaka ya hivi
karibuni.
Tunaamini kuwa hujuma za aina hizo, ambazo
mara nyingi huwakuta makundi yasiyojihami kama watoto, akina mama na
wengine wasiojiweza, zinaweza kuelekezwa kwa makundi ya aina hiyo ambako
magaidi wanajua hawatapambana na upinzani mkubwa.
Vitendo vya ugaidi tayari vimeshazigusa
nchi za Afrika Mashariki, ambapo mwaka 2010 wananchi zaidi ya 70 pia
walipoteza maisha jijini Kampala kutokana na mauaji ya kujilipua mabomu
yaliyotokea wakati wanaangalia mashindano ya dunia ya mpira wa miguu.
Hakuna anayeweza kujua kama magaidi hao
sasa wanalenga kufanya mashambulizi eneo gani, na kwa vile al Shabaab
tayari wametoa onyo la kuendelea na mauaji, ni wajibu wa nchi za Afrika
Mashariki kuunda mtandao wa kudhibiti ugaidi usitokee tena.
Tunaamini kuwa nchi zote sasa zinachukua
tahadhari za kuimarisha usalama, tunatoa wito kwa wananchi wote kutoa
taarifa za mienendo ya watu wanaoweza kutiliwa mashaka kwa mamlaka
husika, kila mwananchi na awe mwanausalama, tukishikamana pamoja
tutatokomeza ugaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI