Na Kelvin Matandiko, Mwananchi
Posted Jumatano,Septemba25 2013 saa 13:53 PM
Posted Jumatano,Septemba25 2013 saa 13:53 PM
Kwa ufupi
Oktoba 10 mwaka huu umoja wa vyama vya siasa
vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, na vingine kadhaa visivyokuwa na wabunge
wameitisha maandamano nchi nzima kuendelea kushinikiza rais asikubali
kusaini muswada huo.
Kila upande miongoni mwa wanasiasa
unaonzungumzia Katiba Mpya unajificha kwenye kivuli cha masilahi ya
wananchi. Chama tawala, CCM, kinasema kinatetea maslahi ya wananchi na
wapinzani nao wanadai kutetea maslahi hayo hayo.
Swali kuu, ni nani kati yao hasa anatetea
wananchi? Mwenye majibu ni Rais Jakaya Kikwete anayetupiwa mpira wa ama
kusaini au kutosaini sheria ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, ambayo inaaminika kuwa ama inaweza kuipatia Tanzania Katiba bora
au bora Katiba.
Wakati upande wa CCM wamekwishatumia nguvu ya
wingi wao kwa kupitisha sheria hiyo ndani ya Bunge, wapinzani wameanza
kuunganisha makundi mbalimbali ya jamii kuikataa, huku wakisema “Katiba
Mpya lazima ipatikane kwa gharama yoyote.”
Miongoni mwa makundi yaliyokutana na viongozi
upinzani, ni wanahabari, viongozi wa dini, wasomi, wanaharakati na sasa
wameanza kufanya mikutano ya wananchi wa kawaida.
Pamoja na kauli “katiba kupatikana kwa gharama
yoyote”, viongozi hao wa upinzani waliokutana na wananchi jijini Dar es
Salaam, wameweka bayana kuwa iwapo Rais Kikwete hatasikiliza hoja za
umoja wao na kuachana na sheria hiyo, mapambano yataendelea kufanyika
ndani na nje ya Bunge, lakini hawataingia katika Bunge Maalumu la
Katiba.
Vilevile Oktoba 10, mwaka huu, umoja wa vyama vya
siasa vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, na vingine kadhaa visivyokuwa na
wabunge wameitisha maandamano nchi nzima kuendelea kushinikiza rais
asikubali kusaini muswada huo.
Viongozi hao Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), Profesa Lipumba(CUF), na akina Fahmi Dovutwa (UPDP),
Emmanuel Makaidi (NLD) na Said Miraji (ADC) wanasema hawatarudi nyuma
katika suala hili kwa kuwa lina maslahi ya wananchi.
Mbowe anaweka msisitizo: “Kosa kubwa katika kudai
haki ni woga. Hatutapata Katiba Mpya kama tutaendelea kuwa taifa la watu
wenye hofu. Hatutakubali kurudi nyuma katika mchakato huu na endapo
rais atasaini muswada huu, tutajitoa kabisa katika harakati za kuandaa
Katiba na badala yake tutaendelea kupiga kelele mpaka dunia yote itambue
tunataka Katiba Mpya yenye tija kwa Watanzania.
Kwa vyovyote vile, mtu pekee wa kutegua
kitendawili hiki ni Rais Kikwete, ambaye tayari viongozi wa CCM na
Serikali yake wamekuwa wakimwomba asaini sheria hiyo na pengine kumtisha
kuwa iwapo atasaini sheria hiyo machafuko yatazuka bungeni.
Marekebisho ya sheria hiyo yanaelezwa kuwa
yamepitishwa bila kuwashirikisha Wazanzibari, wakati kwa ushirika wao
wana haki sawa na Tanganyika ndani ya Muungano.
Inaelezwa pia kuwa marekebisho hayo yameweka
wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalumu la Katiba kuwa asilimia 36 ya
wahumbe wote wakati nchi hiyo licha ya odogo wake kijiografia, ina haki
sawa na Tanganyika. Usawa huo unaonyeshwa tu kwenye idadi ya wajumbe wa
Tume ya Marekebisho ya Katiba ambayo inaundwa na wajumbe 15 kutoka kila
nchi.
Pamoja na hoja ya kupinga Rais kuteua wajumbe 166
wasiokuwa wabunge, muswada huo unadaiwa kuwa, kinyume na katiba ya sasa,
umeruhusu iwapo theluthi mbili za kila upande hazikupatikana kwa mara
mbili katika Bunge Maalumu la Katiba, kwa mara ya tatu itakuwa kwa
uwingi wa kawaida (‘simple majority’) ya kila upande.
SOURCE: MWANANCHI
Sheria yenye vipengele hivyo ilipishwa na wabunge wa CCM baada
ya wale wa upinzani kutoka nje ya Bunge kupinga kuwa sehemu ya uamuzi
hayo na tangu kuanza kwa mvutano huo Rais Kikwete yuko kimya, bila shaka
akitafakari ni njia ipi yenye unafuu aweze kupenya ili abaki na heshima
yake na usalama ndani na nje ya chama chake.
Kwa upande wa CCM na Serikali yake, pia shinikizo
si haba. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano, Uratibu wa Sera,
Stephen Wasira yeye anakipinga hoja zote za kumshinikiza asisaini mswada
huo. Anasema endapo Rais hatakubali kusaini mswada huo, taifa litaingia
kwenye mgogoro wa kikatiba.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
anaongeza kuwa mswada huo ulipitishwa kwa haki na demokrasia ya kuhesabu
kura ya wabunge, hivyo Rais anapaswa kuusaini.
Mitego aliyovuka JK
Huu si mtego wa kwanza kwa Rais Kikwete tangu kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kukuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk Azaveli Lwaitama anasema hatua ya Watanzania kutaka Katiba
Mpya ilipingwa na viongozi wengi wa CCM, lakini Rais Kikwete akafikia
uamuzi wa kukubaliana na ombi hilo.
Mbali na hatua hiyo, Dk Lwaitama anasema Rais
Kikwete aliamua pia kutofautiana na chama chake baada ya kuagiza mjadala
wa sheria ya mabadiliko ya Katiba urudishwe bungeni kwa mara ya pili
ili kuleta maridhiano.
“Ninaamini huu pia ni mtego mwingine anaokutana
nao Rais kutoka ndani ya chama chake, ninaamini kama kiongozi anayepima
hoja za Katiba kwa mustakabali wa kizazi kijacho, atafanya uamuzi wa
kutokusaini muswada huo,” anasema Lwaitama.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full
Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe anasema kuwa Rais Kikwete
akisaini muswada huo, Watanzania watajua kuwa hana nia njema na taifa
kwa kuwa wengi wanaupinga.
Hofu ya Kakobe juu ya muswada huo, anasema
inatokana na mamlaka ya Rais kuteua wajumbe nje ya majina
yaliyopendekezwa. “Sina hakika kama CCM ina dini ya kutuwakilisha hata
sisi, ni hatari sana kuiteka Katiba ya Watanzania, ninamwomba Rais
usikubali mtego huo,” anasema Kakobe.
Naye kiongozi wa maimamu nchini, Sheikh Rajab
Katimba anasema Katiba Mpya ni kwa ajili ya Watanzania na siyo chama,
dini au kundi lolote.
“CCM ilikataa Katiba isianzishwe, Jakaya Kikwete
pekee alijipiga kifua akakubali, ingawa alishambuliwa na chama chake,
kwa hiyo ninaomba kwa msimamo aliotumia awali, asisaini muswada huo,”
anasema Shekh Katimba.
SOURCE: MWANANCHI