September 28, 2013 By
Kufungiwa
kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai ya “uchochezi” ni
mwendelezo wa matumizi ya sheria mbovu ya magazeti ambayo imekuwa
ikitumika mara kwa mara kuzima au kuzuia mawazo na maoni ambayo serikali
inayaoona kuwa hayafai. Kwa vile sheria hii imeweka madaraka makubwa
kwa Waziri mwenye dhamana ya vyombo vya habari basi neno lake ni la
mwisho na haitaji hata kufafanua maamuzi yake. Na baya zaidi ni kuwa
uamuzi wake hauwezi kuhojiwa na mahakama yoyote.
Wakati umefika
kwa vyombo vya habari, wananchi na wadau wengine kuanzisha vuguvugu
litakalosababisha sheria hii ibadilishwe na hata kufutwa ili yeyote
mwenye dhamana ya vyombo vya habari asichukue uamuzi bila kuangaliwa na
chombo kingine (kama mahakama). Katika demokrasia ni muhimu kuhakikisha
uwepo wa mfumo wa kusimamiana (checks and balances) ili kwamba mtu au
chombo kimoja kisiwe na nguvu za kiimla (dictatorial powers). Kama
Waziri angetakiwa kwenda mahakamani kufungua kesi dhidi ya magazeti haya
– kesi ya uchochezi- ni wazi kuwa mahakama ingetakiwa kuangalia
ushahidi uliopo na uzito wa ushahidi huo ukilinganishwa na haki za
kikatiba zinazolinda vyombo vya habari na watoa maoni.'
Kwa msingi
huo, japo ninatambua uwezo na mamlaka ya Waziri kuchukua maamuzi
aliyoyafanya nasimama kupinga na kulaani maamuzi haya kwani yanadumaza
uhuru wa maoni, yanatisha vyombo vya habari na yanalengo la
kuwalazimisha Watanzania kusoma na kusikiliza maoni yenye baraka za
watawala tu na hivyo kuwapa watawala nguvu juu ya fikra na akili za
wananchi. Lakini zaidi napinga uamuzi huu kwa sababu unaifanya serikali
ni mlezi wa akili za wananchi kiasi kwamba kunaifanya serikali kuwa
‘hausigeli/hausiboy’ wa fikra za wananchi – kwamba wananchi hawajui
kupima habari.
Ikumbukwe hadi leo hii hakuna kesi hata moja au
mtu hata mmoja ambaye amewahi kushtakiwa na kukutwa na hatia ya kufanya
jambo dhidi ya serikali au viongozi ati kwa vile amesoma habari
ikamchochea kufanya jambo hili – maana ndio msingi wa hoja ya uchochezi!
Napinga, Nakataa na ninakebehi madaraka haya ya Waziri.
Baada ya
kusema hayo ni muhimu kusema pia kuwa uhuru wa habari na uhuru wa maoni
unataka vyombo vya habari kuwajibika na kujiangalia vyenyewe
(self-censorship) ili kuhakikisha kuwa habari wanazoandika zinaendana na
ukweli na uhalisia na hili ni muhimu hasa kwa magazeti ambayo yanadai
kuwa ni objective. Habari za kuvuta hisia (sensational news) zinatakiwa
zibakie kwenye vyombo vya habari vya namna hiyo (tabloids). Kwa kadiri
sheria hii bado ipo Wahariri na waandishi wajipime wasiwape sababu
watawala kuingilia vyombo vyao vya habari.
SOURCE: MMM