28th September 201
Akizungunza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Fastjet, Ed Winter alisema wasafiri waliokwama, walirudishiwa nauli zao, lakini mwezi ujao watasafirishwa bila kutozwa nauli.
Winter alisema fastjet inatambua umuhimu wa wateja wake na Watanzania kwa ujumla, hivyo wanahitaji kupatiwa huduma bora na zenye gharama nafuu.
Aidha, alisema kwa sasa safari za fastjet kutoka nchini hadi Afrika Kusini, zitakuwa zinafanyika mara tatu kwa wiki siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
“Tunajivunia mafanikio makubwa tangu kuanza kwa safari zetu miezi 12 iliyopita hapa nchini, tukiwa na ndege moja iliyosajiliwa kwa namba A319 na kutoa huduma Dar es salaam, Mwanza na Kilimanjaro,” alisema Winter.
Alisema safari za fastjet kuelekea Afrika Kusini zitawapa kile wanachostahili wateja pamoja na fursa kupata huduma bora kwa bei nafuu.
Naye ofisa mkuu wa biashara wa fastjet, Richard Bodin, alisema wamepewa siku saba za kusubiri ndipo waanze kutoa huduma ya kusafirisha abiria waliokwama kutoka Tanzania hadi Afrika Kusini.
Bodin alisema fastjet inawapa fursa wateja wake kusafiri kwa gharama nafuu toka Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro na Mwanza, hivyo baada ya ndege hiyo kutoka Tanzania kwenda Johanesburg wataongeza safari za kwenda Songwe pamoja na Mbeya.
Alisema gharama za fastjet kutoka Dar es Salaam hadi Kilimanjaro na Dar es Salaam kwenda Mwanza bila kodi ni Sh 32,000.
CHANZO:
NIPASHE