Na Aidan Mhando, Mwananchi
Posted Jumatatu,Septemba30 2013 saa 10:3 AM
Posted Jumatatu,Septemba30 2013 saa 10:3 AM
Kwa ufupi
Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na kutoa sura mpya
ya Taifa ni pamoja na kuwa na Serikali tatu, Spika wa Bunge kutokuwa
Mbunge wala mwanachama wa chama cha siasa.
Tume ya mabadiliko ya Katiba imetangaza Rasimu
ya Katiba ambayo imetoa sura mpya ya muelekeo wa Taifa.Rasimu hiyo
ilizinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam Juni tatu mwaka huu na Makamu wa
Rais Dk, Mohamed Gharibu Bilali.
Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na kutoa sura
mpya ya Taifa ni pamoja na kuwa na Serikali tatu, Spika wa Bunge
kutokuwa Mbunge wala mwanachama wa chama cha siasa.
Mengine ni kuwepo na mgombea binafsi jambo ambalo litatoa fursa kwa wananchi kushiriki kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Wakati wa uzinduzi wa rasimu hiyo wadau mbalimbali
walijitokeza kuhudhuria sherehe za uzinduzi huo ambapo wapo
waliyopongeza hatua hiyo na wengine kulalamika kwamba kuna baadhi ya
mambo yameachwa.
Mgombea binafsi
Jambo kubwa ambalo lilifurahiwa na kuungwa mkono
na watu wengi wakiwamo viongozi wa juu wa serikali na wa kimataifa
kuruhusiwa kuwepo kwa mgombea binafsi.
Kwa mujibu wa Tume ya Katiba kupitia Mwenyekiti
wake Jaji mstaafu Joseph Warioa anasema Tume imeridhia kuwa na mgombea
binafsi baada ya kuchambua maoni mengi yaliyotolewa na wananchi.
Hiyo inamaana kwamba kila Mtanzania atakuwa na haki ya msingi ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi anayo itaka ndani ya nchi.
Migiro anena
Lakini jambo hilo liliungwa mkono na aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dk Asha Rose Migiro ambaye naye
alihudhuria sherehe za uzinduzi huo na kupata nafasi ya kutoa maoni yake
kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu hiyo. Dk Migiro anasema hatua
hiyo ni nzuri na itasadia wananchi kupata fursa ya kushiriki kuomba
nafasi za uongozi wanazozitaka.
Anasema jambo hilo litazidi kuimarisha demokrasia
ya nchi na kwamba huu ndiyo wakati sahihi wa wananchi kushiriki kwa
wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wanazozitaka.
“Mimi nimevutiwa sana na Rasimu ya Katiba kuwapa
nafasi wananchi kuweza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani hiyo
itakuwa fursa nzuri kwao kuonyesha uwezo wao,” anasema Migiro.
Anasema kitu kikubwa alichokuwa anakifikiri ni kwamba Tanzania
itaweza kuandika historia ya kutengeneza Katiba kwa njia ya amani.
“Mimi nilipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa nilikuwa nafikiria sana suala la Katiba. Kitu kikubwa ni kwamba
Tanzania itaandika historia ya kutengeneza Katiba kwa njia ya amani.”
Dk Migiro anaeleza kuwa jambo hilo limefanikiwa na
sasa Tanzania inaandika historia katika nchi za Afrika kwa kuwa na
Katiba iliyowashirikisha wananchi na iliyoundwa kwa njia ya amani.
Historia ya Tume
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Warioba anasema
Rasimu hiyo ya Katiba imekamilika baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
kufanya mikutano 1942 ambayo ilihudhuriwa na watu 1,306,500.
“Watu 395,000 walitoa maoni ana kwa ana na makundi
160 maalumu, yalitoa maoni yao. Pia tulizungumza na viongozi wa
kitaifa; walioko madarakani na wastaafu. Viongozi 43 walitoa maoni,”
anasema.
Jaji Warioba anaeleza kuwa baada ya maoni hayo
walikuwa na miezi mitatu kuyachambua na kuandaa Rasimu ya Katiba, lakini
wakalazimika kuongeza muda huo hadi Mei mwaka huu.
“Kutokana Sheria, Rasimu hii itakchapishwa kwenye
gazeti la Serikali na baadaye kwenye magazeti kabla ya Mabaraza ya
Katiba kuanza kazi mwanzoni mwa wiki ijayo,” anasema Jaji Warioba .
Anabainisha kuwa mchakato huo wa Mabadiliko ya
Katiba ulioanza kwa sheria iliyotungwa Novemba 2011 na baadaye kufanyiwa
mabadiliko Februari 2012 umepangwa kumalizika ndani ya miezi 18.
“Hivyo Tume imekusudia kumaliza mchakato huo Novemba Mosi mwaka huu,”anasema.
Katika awamu tatu za ukusanyaji maoni Tume ya
wananchi 1,015,564 walitoa maoni yao kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja
na waliohudhuria mikutano ya moja kwa moja, waliotuma ujumbe mfupi wa
simu(sms), barua pepe na kutumia mitandao ya kijamii kama facebook.
Idadi ya makundi yaliyotoa maoni ni 170 zikiwemo
asasi 22 za dini, kiraia 72, taasisi za serikali 71, vyama vya siasa 19,
viongozi na watu mashuhuri 43 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
SOURCE: MWANANCHI