Na Rehema Matowo,Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Marangu. Baba mzazi wa mabinti
wawili mkazi wa Kijiji cha Kiria Kata ya Mamba Kusini, wilayani Moshi,
mkoani Kilimanjaro, amewabaka na kuwalawiti binti zake hao wenye umri wa
miaka 10 na 13 na kuwajeruhi vibaya.
Kitendo cha baba huyo kufanya unyama huo kimedaiwa
kuwapandisha hasira kinamama wa kijiji hicho walioamua kumkamata na
kumpeleka Kituo cha Polisi Himo huku wakitishia kumuua iwapo polisi
watamwachia huru, kwa madai imekuwa ni kawaida yao kila akifikishwa
kituoni hapo kuhusiana na unyama anaowafanyia watoto hao huachiwa.
Mwanamume huyo anadaiwa kuwa na tabia ya
kuwatendea vitendo hivyo wanaye hao kwa muda mrefu, kutokana na ugomvi
baina yake na mkewe uliosababisha mkewe akimbie na kuwaacha watoto hao
na baba huyo.
Akizungumza Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiria, Doroth
Mtui, alisema taarifa hizo alizipata kutoka kwa majirani wa watoto hao,
ambapo mtoto mmojawapo alimweleza kwa undani juu ya ukatili huo na
baadaye walimkamata mwanamume huyo na kumpeleka Kituo cha Polisi Himo.
Alisema walipofika kituoni, walitakiwa kumpeleka mtoto huyo hospitalini ili kuthibitisha kama kweli amebakwa.
Taarifa iliyotolewa na daktari wa Hospitali Teule
ya Kilema, ilionyesha mtoto huyo kuharibiwa sehemu zote mbili na kwamba
kitendo hicho kimekuwa kikifanyika kwa muda mrefu.
Mtui alidai kuwa mwanamume huyo, alikuwa akiishi
na watoto hao wawili ambao aliwatumia wote kwa zamu na kwamba mtoto
mdogo, alifanikiwa kutoroka na mpaka sasa hajulikani aliko, aliendelea
kumtendea ukatili huo mtoto aliyebaki huku akimtisha kumuua iwapo atatoa
siri hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi wamekamilisha
uchunguzi na huenda mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI