Na Elias Msuya, Mwananchi
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 11:0 AM
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 11:0 AM
Kwa ufupi
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo anabainisha kwamba shauri
hilo lipo mahakamani na kwamba kumekuwapo uovu mwingi kwenye sekta ya
madini.
Urani inayochimbwa kote Tanzania haina hatari hadi isafishwe ndiyo maana inapatikana juu ya ardhi, Mungu ni wa ajabu kabisa.
Wakati Tanzania ikitegemea kuanza kufaidika na
madini ya urani, tayari kuna harufu ya ufisadi inayogubika kampuni za
uchimbaji wa urani wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.
Akifafanua utafiti alioufanya kuhusu athari za
uchimbaji madini ya urani nchini hivi karibuni jijini Dar es Salaam,
mwanasheria wa mazingira Dk Lugemeleza Nshala anasema harufu hiyo
inatokana na kampuni ya Mantra Resources Limited yenye leseni katika
eneo la Mkuju River kujigawa katika kampuni mbili yaani ARMZ na Uranium
One.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo anabainisha kwamba shauri hilo lipo
mahakamani na kwamba kumekuwapo uovu mwingi kwenye sekta ya madini.
“Ni kweli kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wamepeleka suala hilo mahakamani, lakini mkataba wa kuchimba madini
hayo ni mwingine kabisa. Nakubaliana na wewe pia kwamba kumekuwa na
mikataba mibovu, sijui kuna watu wamekula, lakini Watanzania tuwe na
mtazamo wa kuendelea siyo kuangalia nyuma.
“Huo ni mtazamo wa kizamani, tumekuwa na muda
mwingi wa kujadili matatizo tu, tumekuwa waoga mno wa kuthubutu, haya
matatizo popote yapo. Mfumo wa dunia kwa sasa ni uwekezaji, tuwekeze
ndani na nje ya nchi ili kupata fedha na ajira,”anabainisha Profesa
Muhongo.
Ukwepaji kodi
Dk Nshala anasema: “Oktoba 2010 Mantra Resources
Limited ya Australia inayomiliki leseni ya Mkuju River iliingia kwenye
utekelezaji wa mkataba na kampuni ya Atomredmetzoloto (ARMZ) ya Russia
katika makubaliano yao na ARMZ ilitakiwa iwalipe Mantra dola 1.6 bilioni
za Marekani ikiwa ni asilimia 100 ya kumiliki Mantra.
“Hivyo makubaliano ya kuuza hisa zake yalikuwa ni
dola 8.00 za Australia kwa kila hisa, lakini kutokana na tetemeko
lililotokea Fukushima Japan kwenye kinu chake cha nyuklia miezi minne
baadaye, ARMZ wakataka kujitoa.
“Lakini baadaye wakaja na makubaliano mapya na
Mantra hawakuwa na la kufanya ila kuingilia makubaliano ya kushusha bei
ya dola za Australia 7.02 kwa kila hisa ambayo ni sawa na dola 1.04
bilioni za Marekani ya hisa zote. Hadi Juni 7, 2011 makubaliano
yakafikiwa na ARMZ ikamilikishwa hisa zote.
“Mwaka huohuo, ARMZ ikaingia mkataba wa kununua
hisa 51.4 za kampuni ya Uranium One ambayo ni kampuni tanzu ya Canadian
uranium mining company,” anasema Dk Nshala.
Anaendelea kufafanua: “Hivyo kuhamishwa kwa Mantra
Resources Limited kutoka ARMZ ili wadau wa awali kupata dola 1.04
bilioni za Marekani bila kulipa kodi ya mapato kwa Tanzania.
“Sheria ya madini ya mwaka 2010 inaruhusu kampuni ya madini
kugawa faida yake baada ya kupata ruhusa kutoka kwa mamlaka ya leseni
ambaye kimsingi ni kamishina wa madini.
Kifungu cha 36(1) cha Sheria ya Kodi ya mapato
kinaonyesha Mantra Resources Limited ya Australia ilitakiwa kulipa kodi
kwa Serikali ya Tanzania,” anabainisha Dk Nshala.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipeleka
mfululizo madai kwa ARMZ ikitaka kulipwa dola 200 milioni za Marekani
kama kodi ya faida. Sasa TRA imepeleka kesi hiyo Bodi ya Rufaa ya Kodi
ya Mapato.
Jitihada za kuutafuta uongozi wa Mantra Tanzania
ili kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda licha ya Mkurugenzi
Mtendaji, Assa Mwaipopo kumtaka mwandishi kumtumia maswali kwanza ayaone
jambo mbalo mwandishi wa makala haya alifanya hivyo. Licha ya Mwaipopo
kupelekewa maswali na kukumbushwa mara kwa mara kujibu, mpaka leo
hakujibu maswali hayo.
“Kwa sasa niko kwenye mkutano wa bajeti, nitumie maswali kwanza niyaone,” anasema Mwaipopo kwa njia ya simu.
Mazingira
Mbali na kuwapo utata katika ulipaji wa kodi, Dk
Nshala amesema katika taarifa yake Tanzania bado haijawa tayari kwa
uchimbaji huo kwani hakuna maandalizi ya kutosha.
Anaeleza kwamba utoaji wa leseni kwa Kampuni ya
Mantra Tanzania Ltd na ziara ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa
Rais, Dk Terezya Huvisa katika ofisi za Mantra Tanzania na wilayani
Namtumbo, ilikuwa kinyume cha sheria ya EMA kifungu cha 95 na 206(2(c)
na unaweza kupingwa katika Mahakama ya Rufaa ya Mazingira.
“Waziri alikaririwa akisema kampuni kupitia
taarifa yake ya mradi imemshawishi kwamba mradi umejengwa nje na mbali
ya makazi ya watu hivyo ina faida.”
Dk Nshala anabainisha sheria haisemi popote kwamba
Waziri anatakiwa akubaliane na mawasilisho ya mradi huo kama
alivyofanya yeye.
Dk Huvisa anasema: “Kwa nini nisitembelee mradi
huo, Watanzania ni watu wa ajabu sana, mimi kama Waziri najiamini na
nina hofu ya Mungu kwa nini nisiende?
Nimetembelea machinjio, nimetembelea Double Tree
hotel na hatua zimechukuliwa, kwa nini niende kwenye mradi wa Mantra?”
anahoji Dk Huvisa.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI