Saturday, 28 September 2013

Unyama wa Al-Shabaab wabainika ndani ya jengo

Mabaki ya jengo la Westgate lililoporomoka baada ya shambulizi la kigaidi jijini Nairobi, Kenya.Picha na Daily Mail 


Posted  Septemba28  2013  saa 8:9 AM
Kwa ufupi
Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Daily Mail la uingereza zikiwakariri wanausalama wa Kenya zinadai kuwa magaidi waliwatesa, kuwakata vidole, kuwanyofoa macho, kuwahasi wanaume na kisha kuwaning’iniza darini.


Nairobi. Wiki moja baada ya shambulizi la kigaidi kwenye jengo la Westgate jijini Nairobi, Kenya, unyama wa kutisha uliofanywa na magaidi wa Al-Shabaab dhidi ya raia waliokuwa wametekwa umebainika
Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Daily Mail la uingereza zikiwakariri wanausalama wa Kenya zinadai kuwa magaidi waliwatesa, kuwakata vidole, kuwanyofoa macho, kuwahasi wanaume na kisha kuwaning’iniza darini.
Baadhi ya mateka walinyofolewa kucha kwa koleo na maiti za watoto zilikutwa ndani ya majokofu zikiwa na zimechomwa visu.
Askari walieleza kuwa matukio hayo yalibainika muda mfupi baada ya kuingia kwenye jengo hilo lililokuwa likishikiliwa na magaidi kwa siku tatu, na baadaye kuporomoka kutokana na mashambulizi baina ya magaidi na majeshi ya Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, miili ya magaidi iliyopatikana ilikutwa imeungua na kubaki majivu, tukio lililotafsiriwa kuwa ilikuwa njia ya kuficha utambulisho wao.
Inaelezwa kuwa miili hiyo iliteketezwa na gaidi mmojawapo aliyebaki kwa ajili ya usimamizi wa kufika utambulisho wao.
Hata hivyo wapelelezi wa Kenya wanaoshirikiana na wenzao kutoka Shirika la Kijasusi la Marekani (FBI) na Police wa Kimataifa wanaendelea kuchunguza mabaki ya jengo hilo huku ikikadiriwa kuwa itachukua wiki moja kumaliza kazi hiyo.
Idadi ya vifo kuongezeka
Baada ya vifuso vya jengo hilo kufukuliwa, idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye shambulio hilo imeelezwa inaweza kuongezeka kufikia 130 kutoka 61.
Hata hivyo, hadi jana takwimu zilizotolewa na serikali ya nchi hiyo, zilikuwa zinaonyesha kuwa watu waliopoteza maisha walikuwa 67, saba kati yao wakiwa ni wanausalama.
Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, limesema kuwa watu 63 walikuwa hawajulikani walipo.
Kama watu hao watakuwa chini ya kifusi ambacho tayari kimeanza kufukuliwa, uwezekano wa vifo kuongezeka na kufikia 130 ni mkubwa.

SOURCE: MWANANCHI