Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salaam limeagiza makamanda wote wa mikoa mitatu kuanza kuweka askari polisi wenye silaha katika benki zote ili kuimarisha ulinzi dhidi ya matukio wa wizi wa fedha yanajitokeza kwa kasi katika taasisi hizo za fedha jijini Dar es salaam.
Agizo hilo limetolewa na kamanda wa polisi Kanda maalum Suleiman
Kova wakati alipozungumza na waaandishi wa habari,ambapo amesema
uchunguzi wa matukio ya wizi wa fedha katika mabenki umeonyesha kuwepo
kwa njama za dhahiri kati ya wahalifu na watumishi na hata walinzi wa
kampuni binafsi, na kusisitiza benki zote zitalazimika kufuata taratibu
zilizowekwa na benki kuu ili kuhakikisha siri za benki hazivuji kwa
wahalifu kama ilivyosasa.
Aidha kamishna Kova amesema Jeshi la Polisi limelazimika kuchukua
hatua hizo kutokana na matukio hayo kuendelea kujirudia na kuhatarisha
uwekezaji ambao pia unaingia katika mfumo mzima wa kukuza uchumi kwa
Watanzania na kusisitiza jeshi hilo litahakikisha mtandao wa wizi huo wa
Mabenki unakomeshwa ikiwa ni pamoja na kuwakamata wanaotoa taarifa za
benki ili kusaidia hujuma zinazofanywa na kundi la wahalifu.
SOURCE: ITV -DAIMA