Monday, 30 September 2013

THE PRESIDENT OF UNITED REPUBLIC OF TANZANIA: Rais Kikwete ahutubia Baraza Kuu UN









 President Jakaya Kikwete addresses the 68th plenary session of the United Nations General Assembly, in New York yesterday. (Photo: Freddy Maro, State House)



Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete akihutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York 
Na Mwandishi Wetu

Posted  Jumatatu,Septemba30  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi

“Hili ni jambo ambalo halikubaliki kabisa katika dunia iliyojaa neema ya kila aina tunamoishi leo ambako kuna maendeleo ambayo hayajapata kuonekana katika historia ya binadamu ya sayansi na teknolojia ambayo yanaweza kutumika kumaliza changamoto zote za maendeleo zinazokabili jamii ya binadamu sasa.


New York. Rais Jakaya Kikwete juzi alihutubia kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (Unga), New York, Marekani na kusema kama nchi tajiri duniani zingetoa fedha za kutosha kama zilivyokuwa zimeahidi, ni dhahiri kuwa dunia ingeweza kufanikisha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) na malengo yake yote katika kipindi cha miaka 15 kama ilivyokuwa imeamuliwa mwaka 2000.
Aidha, Rais Kikwete alisema Afrika haitochoka kudai haki ya kufanyika kwa mageuzi ya msingi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), ili kuliwezesha bara hilo lenye idadi kubwa zaidi ya wanachama kwenye Umoja wa Mataifa (UN) kuwa na uwakilishi wa kudumu.
Katika hotuba yake ya dakika 15, Rais Kikwete alisema ni jambo lisiloelezeka kuwa dunia ya leo inaendelea kushuhudia umasikini wakati kuna raslimali na utajiri wa kutosha wa kumaliza tatizo hilo ikiwa kuna utashi wa kisiasa kumaliza tatizo hilo.
Rais Kikwete alikiambia kikao hicho ambacho mada yake kuu ilikuwa `Mjadala Kuhusu Ajenda ya Maendeleo Duniani baada ya mwaka 2015' kuwa pamoja na kwamba umasikini mkali zaidi duniani umepunguzwa kwa nusu katika kipindi cha utekelezaji wa MDG, bado zaidi ya watu bilioni 1.2 wanaishi katika mtego wa umasikini mkubwa.
Alisema kuwa mbali na watu hao, bado kiasi cha watoto wanaokadiriwa kufikia 19,000 chini ya umri wa miaka mitano na wanawake 800 hupoteza maisha kila siku kwa magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika na kutibika.
“Hili ni jambo ambalo halikubaliki kabisa katika dunia iliyojaa neema ya kila aina tunamoishi leo ambako kuna maendeleo ambayo hayajapata kuonekana katika historia ya binadamu ya sayansi na teknolojia ambayo yanaweza kutumika kumaliza changamoto zote za maendeleo zinazokabili jamii ya binadamu sasa.
“Katika dunia ambako kuna chakula cha kutosha kumlisha kila mtu, hakuna sababu ya mtu yeyote kulala na njaa na kukabiliwa na ukosefu wa lishe. Katika dunia yenye utajiri mkubwa kama wa sasa, hakuna sababu kwa nini umasikini, njaa na dhiki viendelee kuleta dhiki na kusababisha shida kubwa kwa watu wengi kiasi hiki.”

Rais Kikwete alisisitiza: “Katika hali hiyo, ni jambo lisiloingia akilini kwa nini Malengo ya Milenia hayakufanikiwa kwa kiwango cha juu kabisa.
“Kama nchi tajiri na zilizoendelea duniani zingekuwa zimetoa fedha na rasilimali za kutosha kama ilivyokuwa imekubaliwa chini ya lengo la nane kwa mipango hiyo kwa mujibu wa makubaliano na ahadi zao katika mikutano ya nchi tajiri duniani ya G8 na G20, tungefanikiwa kutekeleza mipango hiyo,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kwa maana hiyo, litakuwa ni jambo la kujidanganya kama tulijadili nini tufanye kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia Baada ya 2015 bila kujadili na kukubaliana kuhusu jambo la msingi la jinsi ya kugharimia mipango hii.”
Mapema leo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na baadaye alikutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani (anayeshughulikia siasa), Wendy R Sherman.

SOURCE: MWANACHI AND IPP MEDIA