Saturday, 28 September 2013

Waathirika wa tindikali wafunguka

27th September 2013
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akimjulia hali Sheha wa Shehia ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi Unguja, Mohamed Said Kidevu (kulia) aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar baada ya kumwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana.
NI saa 12:38 jioni. Nafika Mwanakwerekwe, nyumbani kwa Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.  Kunako lango kuu la kuingilia nyumba ya sheikh huyu nakutana na mlinzi aliyekamilika kwa kila kitu.

Ana mabuti ya kiaskari na begani alikuwa amening'iniza bunduki nisiyoijua ni ya aina gani. Namkaribia na kuuliza ili kupata uhakika wa mambo mawili.

Kwanza kujua kama hapo ndipo kwa katibu wa mufti, Sheikh Soraga. Pili, kama ndipo, basi nihakikishiwe vilevile kuwa yupo ili nionane naye.

Mlinzi huyu anayeonekana kuijua vyema kazi yake hanipi jibu lolote. Ananitaka nisubiri. Dakika chache baadaye anatoka mama mweupe kwa rangi asiyekula chumvi nyingi. Si mtu mzima kiasi hata cha kukaribia tu kuitwa bibi.

Huyu ananichangamkia vya kutosha. Kauli yake wakati akinisalimia kabla ya kutaka kujua shida yangu ilijaa ustaarabu wa watu wengi wa visiwa hivi vya Unguja. Ndiyo. Uungwana ulijidhihiri katika kila nukta ya alichokisema.

Maamkizi yakakamilika. Kisha bila kupoteza muda, nikarudia kumuuliza swali lilelile nililolitoa kwa mlinzi. Kwamba je; hapa ndipo kwa Sheikh Soraga? Na je; nimemkuta?

Badala ya kunijibu, mama akarudia tena kunitazama kwa haraka. Akanitupia jicho kuanzia juu mpaka chini. Nadhani alikuwa akijaribu kunijua walau kwa muonekano wangu tu kuwa miye ni nani, nina nia gani na kwa nini nimefika muda huo kumuulizia Sheikh Soraga.

Mara moja, nami nikabaini kile kinachomkwaza mama huyu. Na sikutaka kumpotezea muda wake. Sikutaka nimtese kwa kufikiri sana kabla ya kuamua nini anijibu.

Badala yake, nikamuwahi kwa kujitambulisha. Nikajieleza pasi na kujikwaa. Kwamba miye ni mwandishi wa habari kutoka gazeti la NIPASHE, Dar es Salaam, makao makuu ya magazeti ya The Guardian Limited.
Nimetua siku hiyo (Jumatano) kwa nia ya kuonana na Sheikh Soraga ili nipate mawili matatu kutoka kwake.

"Ndiyo hapa kwa Sheikh Soraga… Karibu ndani tafadhali," alinieleza.
Nikavua viatu vyangu nje tu ya lango la kuingilia ndani. Nukta chache zilizofuata nikawa sebuleni. Naam. Palikuwa ni mahala penye muonekano sahihi kwa mtu wa wasifu wa Sheikh Soraga. Panavutia sana.

SEBULENI KWA SHEIKH SORAGA

Eneo hili lote, ambalo ni la chumba kipana chenye nafasi ya kutosha lilikuwa limenakshiwa kwa marumaru za rangi ya dhahabu.

Madirisha matatu yalikuwa pia yamepambwa kwa pazia safi za rangi ya dhahabu. Na pazia za mlango pia zilikuwa za rangi ya dhahabu, sawa na feni kubwa la pangaboi na hata makochi na rangi ya vimto vyake vidogo. Vitu vingi  hapa vilipambwa kwa rangi ya dhahabu na kupafanya mahala hapo pawe pa kuvutia sana.

Katikati ya eneo hili pana palikuwa na zuria kubwa lenye manyoya ya kuvutia kwa mchanganyiko wa rangi ya dhahabu na nyekundu. Kwa mbele, katika sehemu iliyoinuka kidogo, palikuwa na televisheni kubwa, nyembamba yenye umbile bapa (plasma).

Mvuto wa eneo hili lililoonekana kutunzwa likatunzika uliongezwa pia na harufu nzuri ya uturi wa Kiunguja, usiochosha pua hata kidogo. Ni mahala palipovutia sana.

"Karibu sana," alisema mama aliyenikaribisha. Kisha akanitaka nisubiri ili akamwite Sheikh Soraga ambaye muda huo alikuwa ametoka kuswali. Ni nyakati za kukamilisha swala ya jioni (swalat Maghrib).

Punde, pazia kubwa lililokuwa upande wa kulia wa sebule likafunguka.  Akatoka baba mtu mzima, akiwa amevalia msuli na shati jepesi. Nilistuka. Moyo ukanienda joshi.

WAJUA NI KWA NINI?
Ni kwamba, mtu huyu alikuwa na muonekano tofauti sana. Uso wake ulikuwa kama ulioungua. Tembea yake ya hatua za kuhesabu iliashiria maumivu makali ya mwili.

Sehemu kubwa ya mkono wake wa kulia pia ilionekana kana kwamba imetoka kuunguzwa kwenye tanuru la moto mkali na kisha kuondolewa kwa muda.

Kwangu ilikuwa ni huzuni tupu kumuona mtu huyu. Na aliponisalimia kwa sauti yake ya chini iliyojaa uungwana, nikajikuta nikiwa katika shinikizo kali la kuzuia machozi yasinitoke. Naam. Haikuwa kazi rahisi kumtazama mara mbili na kutaka kumsemesha pasi na nguvu ya huruma kukwaza kasi ya ulimi katika kuzungumza.

Baada ya kusalimiana nami kwa kushikana mikono, Sheikh Soraga akaketi kwenye kochi mojawapo lililokuwa wazi. Nami nikalazimika kuhama nilikokuwa awali. Nikaenda karibu yake na kuketi chini kwenye zuria ili nisimpe shida ya kutumia nishati kubwa wakati akizungumza nami.

Nikaanza kwa kujitambulisha kwake. Nikamueleza sababu za kumtembelea muda huo. Kwamba, anieleze mengi kuhusiana na mkasa wake wa kumwagiwa tindikali kuelekea mwishoni mwa mwaka 2012.

Anieleze ni nani anafikiria yuko nyuma ya mpango huo wa kinyama. Anafikiri ni kwa nini alifanyiwa hivyo yeye na si mtu mwingine? Ni kwa nini matukio hayo ya watu kumwagiwa tindikali yanatokea zaidi sasa visiwani Zanzibar? Na kwamba, anadhani ni kwa nini pia wamemwagiwa wageni wawili, sheha, mkurugenzi wa manispaa na padri wa kanisa Katoliki?

Je, maisha yake yakoje sasa baada ya kukumbwa na mkasa huo?

Hakika maswali yangu yalikuwa mengi. Hata hivyo, hakuna nilichofanikiwa. Mara tu nilipojitambulisha na kueleza dhamira yangu (ya kumhoji kuhusiana na masahibu yaliyomkuta), Sheikh Soraga alinikatisha na kunisihi niache kabisa mazungumzo hayo.

Nikashangaa. Nilipomuuliza ni kwa nini hataki tuzungumzie mambo hayo ilhali ndiyo sababu ya kumtembelea jioni hiyo, Sheikh Soraga alinieleza kwa kifupi kuwa niridhike kuamini tu kwamba hayuko tayari kuzungumza na vyombo vya habari; na kwamba hata familia yake haimruhusu kufanya hivyo.

"Niwie radhi… familia yangu haitaki nizungumzie masuala haya. Naomba uheshimu maamuzi haya," alinijibu, wakati huo yule mama niliyethibitisha baadaye (kama hisia zangu zilivyoniambia kitambo) kuwa ndiye mke wa Sheikh Soraga,  akanikaribia mahala nilipokuwapo na kunisihi kuwa niache kabisa kumtonesha machungu mumewe kwa kuzungumzia masuala ya tindikali.

Nikakosa namna. Nikalazimika kufunga kila kilicho changu. Nikawaaga wote na dakika chache baadaye, tayari nilishakuwa mbali na eneo hilo la Mwanakwerekwe. Nuru ya jua ilishatoweka, giza lilishakamata utawala wake. Siku hii ikapita.

SHEHA WA TOMONDO

Siku iliyofuata, mishale ya saa 4:00 asubuhi, nilishakuwa katika ofisi ya Shehia ya Tomondo. Kwa Tanzania Bara, ofisi hii ina hadhi sawa na zile za serikali za mitaa au za vijiji. Viongozi wao huitwa Sheha.

Kilichonipeleka hapo ni kutaka kuonana na Sheha Mohamed Omar Said ‘Kidevu’, ambaye ni mmoja wa waathirika wa mashambulizi tofauti ya tindikali visiwani Zanzibar.

Kwa bahati nikamkuta. Nikashuhudia unyama mwingine. Sheha Kidevu alikuwa ameumia sana. Na hata nilipomkuta mahala hapo ambako ni upenuni tu mwa nyumba yake, alikuwa bado na dalili za kuuguza majeraha tele kuzunguka shingo yake.

Baba huyu mweupe wa rangi aliharibiwa haiba yake. Upande wake wa kulia, chini tu ya taya, alikuwa bado ana majeraha ya kutisha yaliyoshuka chini kuelekea shingoni, begani na kifuani.

Jicho mojawapo pia lilionekana kuathirika. Alionekana akilitumia kutazama kwa shida kama mtu anayechungulia kunako tundu ya kitasa cha mlango.

Kwa ujumla, Sheha huyu angali bado akihuzunisha sana. Wakati mimi nilipokutana naye, aliniambia kuwa ndiyo kwanza alitoka kuhudhuria kliniki kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja ambako amepangiwa kwenda kila baada ya siku mbili.

Nilijitambulisha. Na kama nilivyotarajia, kamwe haikuwa kazi rahisi kuzungumza naye kuhusiana na madhila yaliyompata. Baadaye alinikubalia, lakini kwa sharti kwamba iwe ni kwa dakika chache sana kwani bado hajisikii vizuri. 

ALIVYOMWAGIWA TINDIKALI

Sheha Kidevu anasema kuwa tukio la kushambuliwa kwake lilitokea Mei 21, 2012, saa 2:30 usiku. Anasema siku hiyo alikuwa akitembea katika eneo la giza, jirani kabisa na nyumba yake. Ghafla akahisi kama anafuatiliwa na mtu asiyemfahamu.

Kutahamaki, akastukia mtu huyo akimwagia kimiminika pembeni kidogo ya uso ambacho baadaye kilisambaa kwa kasi kuelekea katika sehemu nyingine za mwili. Kisha mtu huyo akatupa chini kopo lililokuwa na kimiminika hicho na kukimbia zake.

Kidevu anasema kuwa baada ya hapo, mara moja akabaini kuwa hicho alichomwagiwa hakikuwa maji, bali ni kitu cha hatari.

Ni kwa sababu maeneo ya mwili yaliyoguswa na ‘majimaji’ hayo yalikuwa yakiuma sana kana kwamba yako katikati ya mwali wa moto mkali; chembechembe zilizotua machoni za kimiminika hicho zilimuwasha sana na kumlazimu kufumba macho. Kilio kikubwa kikafuatia, kilio cha kuomba msaada.

Kidevu anasema kuwa baadaye wasamaria wema wakaja na kubaini kuwa amemwagiwa tindikali. Baada ya hapo akakimbiziwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja. Matibabu yake yalimfikisha pia India kufanyiwa operesheni.

“Hadi sasa nimeshafanyiwa operesheni mbili. Namshukuru Mungu kuwa walau sasa nina nafuu kubwa kulinganisha na awali,” anasema Kidevu.

“Kwa  kweli nimeumia sana… watu hawa  wamenirudisha nyuma kiuchumi kwani shughuli zangu nyingi za kusaka kipato kwa ajili ya familia yangu zimetetereka,” anaongeza Sheha Kidevu (59), baba wa watoto saba, wakiwamo watano ambao bado ni wanafunzi na hivyo wangali wakimtegemea kwa asilimia 100.

Nilipomuuliza ni watu gani anahisi kwamba ndiyo waliomfanyia unyama huo, na ni kwa sababu zipi, Kidevu alinijibu: “Sijui kwa kweli. Sielewi kama ni matokeo ya siasa, sijui kama ni kwa sababu ya utekelezaji wa majukumu yangu kikazi… nategemea kuna siku Polisi watasema kuwa hawa ni watu gani na wamenifanyia unyama huu kwa sababu zipi.”

Akieleza zaidi, Kidevu anasema kuwa Zanzibar hivi sasa inakabiliwa na wakati mgumu kutokana na mfululizo wa vitendo vya watu kumwagiwa tindikali.

Kwa sababu hiyo, anashauri kuwa wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuwabaini waovu hao na mwishowe hatua za kisheria zichukuliwe.

“Mambo haya yanapoendelea kutokea, halafu bado kukawa kimya bila kuonekana watu wakifikishwa mahakamani ni hatari sana… ni vyema jitihada zikaongezwa katika kuwanasa wahusika na sheria ichukue mkondo wake,” anasema Kidevu.

Anaishukuru serikali na wananchi wenzake kwa kumpa ushirikiano wa kutosha muda wote tangu akumbwe na janga hilo, ikiwa ni pamoja na kugharimia matibabu yake na pia kutembelewa mara kadhaa na viongozi wakuu wa serikali akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye anasema ameshamtembelea mara nne.

CCM KISIWANDUI
Baada ya kutoka kwa Sheha Kidevu, nikaenda kuonana na Ali Mwinyi Msuko. Huyu ni mmoja wa waathirika wa shambulizi la tindikali, aliyemwagiwa wakati wa vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Msuko ambaye hivi sasa anajitambulisha kuwa ni Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, nilimkuta akiwa amejaa tele ofisini kwake Kisiwandui, kwenye Makao Makuu ya CCM Zanzibar.

“Nilimwagiwa tindikali nikiwa Pemba wakati wa uchaguzi mwaka 1995, enzi hizo nikiwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM katika Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba,” anasema.
CHANZO: NIPASHE