Kwa ufupi
Unashabikia mambo ya Tundu Lissu leo, endelea
ila mtashughulikiwa,” aliunukuu ujumbe huo na kuongeza kuwa hafahamu
umetoka kwa mbunge gani ila wahudumu wa Bunge ndio waliompelekea.
Dodoma.Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni jana
jioni walitoka ndani ya Ukumbi wa Bunge, baada ya kupuuzwa kwa mwongozo
wao wa kutaka kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa.
Wabunge waliotoka bungeni jana yapata saa 12.15 ni
kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi huku Mbunge wa Vunjo na
Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP, Augustine Mrema
akiendelea kubaki ukumbini.
Kitendo cha wabunge hao wa upinzani kilionekana
kuwakera baadhi ya wabunge wa CCM, ambao walisikika wakiwakejeli kwa
kupiga meza huku wakisema: “Kwendeni zenu, tumewazoea.”
Wakati wabunge hao wakiondoka, Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai, alikuwa akiwasisitiza wabunge wanaobakia wawe
watulivu, maana kuna usalama wa kutosha ndani ya ukumbi huo.
“Mnaotoka nimewaona wote na mnanijua,” alisikika Naibu Spika Ndugai akiwatahadharisha wabunge wa upinzani waliosusa mjadala huo.
Wabunge wa CCM waliendeleza vituko ambapo baada ya
wapinzani kutoka, wabunge Juma Nkamia (Kondoa Kusini), Hilary Aeshi (
Sumbawanga Mjini) na Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini) walikwenda kukaa
katika viti vya kambi ya upinzani.
Kabla ya kutoka kwa wabunge hao wabunge wawili
kutoka CUF waliomba mwongozo wa Spika, wakitaka muswada huo kuondolewa
ili kuwapa nafasi Wanzanzibar kutoa maoni yao.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF)
aliomba mwongozo akitaka muswada huo uondolewe, hadi hapo Wazanzibar
watakaposikilizwa.
Alisema kuwa kwa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria
na Utawala wamesikiliza maoni ya wadau wengi, lakini Zanzibar
hawakwenda kuwasikiliza wadau wa eneo hilo.
“Na hili suala zima katika masuala ya katiba
linahitaji usawa wa washirika, tunazungumza kitu kinachohusiana na
Zanzibar na Tanzania Bara, ili kupata maoni ya nchi nzima kuna uhalali
gani wa Bunge hili kuendelea na mjadala huu?” alihoji.
Hata hivyo, alikatizwa na kelele za Mbunge wa Viti
Maalumu, Pindi Chana (CCM), ambaye alitoa taarifa kuwa Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala ilialika wajumbe mbalimbali ikiwamo Zanzibar.
“Miongoni wa wajumbe walioalikwa ni pamoja na
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na wadau
mbalimbali ambao walikuja mbele ya Katiba,” alisema Pindi ambaye pia ni
Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Mbunge wa Konde, Khatibu Said Alli (CUF), alitaka mwongozo wa
Spika kuhusiana na ujumbe mfupi wa maneno ambao aliupokea ukimtisha,
kutokana na kitendo chao cha kumuunga mkono Msemaji wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Tundu Lissu.
“Unashabikia mambo ya Tundu Lissu leo, endelea ila
mtashughulikiwa,” aliunukuu ujumbe huo na kuongeza kuwa hafahamu
umetoka kwa mbunge gani ila wahudumu wa Bunge ndio waliompelekea.
Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema kuwa ni
miongoni mwa mambo ambayo anayachukua na kuyafanyia kazi ni suala hilo.
Pia Ndugai aliomba ujumbe huo apelekewe.
“Hii ni demokrasia mara nyingi imeshatolewa
miongozo, jibu linatolewa hapo hapo ama baadaye na kwa hoja zilizotolewa
inakilazimu kiti kupata ushauri hapo baadaye,” alisema Ndugai.
Hata hivyo, baada ya Ndugai kutoa majibu hayo, wabunge wa upinzani waliamua kutoka ndani ya ukumbi huo.
Baada ya wabunge hao kutoka Naibu Spika Ndugai
aliendelea na ratiba ya Bunge kwa kusema, jambo hilo halikupangwa
kumalizika jana na kwamba litaendelea kujadiliwa hata ikibidi hadi
keshokutwa.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama kabla ya
mjadala kuendelea na kutetea hoja kuwa makundi yote yalisikilizwa
tofauti na inavyodaiwa na wapinzani.
“Hata katika marekebisho ya sheria mbili hizi,
mimi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumekutana na viongozi wengi na
mawaziri na ndiyo maana tumeahirisha Muswada wa Sheria ya Kura ya
Maoni,” alisema.
Alisema, yeye (Lukuvi) alikuwa Mwenyekiti wa
ujumbe uliotumwa na Rais kuitisha makundi ya siasa ambayo yalijadili
muswada huo. Lukuvi alisema kuwa, pande zote zimeshiriki kikamilifu
katika kutoa maoni yao, “kama hizi ni sarakasi za kisiasa mimi sijui.”
Baada ya kutoka, wabunge wa vyama vya Chadema, CUF
na NCCR-Mageuzi walifanya mkutano wa pamoja kwenye Ukumbi wa Pius
Msekwa. Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa, wabunge hao
walikubaliana kufanya kila njia kuhakikisha wanazuia mjadala huo leo.
Pia wabunge wa CCM nao walikutana nao mara baada ya Ndugai kuahirisha kikao cha jioni.
Lissu achafua hali ya hewa
Hotuba ya Lissu ndiyo iliyochafua hali ya hewa baada ya
kuituhumu Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kwa kutohoji watu
wa Zanzibar wakati wakikusanya maoni kuhusu muswada huo.
Alisema licha ya kamati hiyo kukusanya maoni ya
taasisi za kidini na za kiraia, taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma,
vyama vya siasa na asasi nyingine, lakini bado haikwenda Zanzibar
kukusanya maoni ya watu wa huko.
“Wadau pekee walioshirikishwa kutoa maoni yao juu
ya muswada huu ni Watanzania Bara tu. Wazanzibari hawakupatiwa fursa
hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya sheria yenyewe kuwa na mambo
mengi yanayoihusu Zanzibar,” alisema Lissu.
Pamoja na suala hilo, Lissu alitaka pia Rais wa
Jamhuri ya Muungano aondolewe madaraka ya kuteua Wajumbe wa Bunge
Maalumu wasiokuwa wabunge au wawakilishi kuwa inavuruga au kuondoa
kabisa dhana ya uwakilishi wa wananchi na uhalali wa kisiasa katika
mchakato wa Katiba Mpya.
Pia alipendekeza kuongezwa kwa idadi ya wajumbe
ifikie 792, kwani Tanzania ina idadi ya watu milioni 45 kwa takwimu za
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Lissu pia alitaka wawakilishi wa Zanzibar
waongezwe bungeni, kwa Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 kwenye Bunge
lenye wajumbe 604, sawa na takriban 36% ya wajumbe wote. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inataka idadi iwe nusu kwa nusu kati ya pande mbili za
Muungano.
Wajumbe 166
Kutakuwa na wajumbe 166 wasiotokana na Bunge na
Baraza la Wawakilishi watateuliwa na Rais. Kutakuwa na Wabunge 357 na
Wawakilishi 81 na kufanya Bunge Maalumu kuwa na jumla ya wajumbe 604.
Chikawe asoma muswada
Mapema akisoma muswada huo, Waziri wa Sheria na
Katiba, Mathias Chikawe alisema Rais atakaribisha makundi mbalimbali
kuwasilisha majina yasiyozidi matatu kila kundi ambao watateuliwa kama
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Alisema pia Kifungu cha 27 (2)
kitatoa fursa kwa uhuru wa maoni katika mijadala ya Bunge Maalumu na
maoni hayo hayatahojiwa mahakamani au sehemu yoyote nje ya Bunge
Maalumu.
Chikawe alisema Bunge Maalumu la Katiba litakaa
kwa siku 70 mfululizo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili rasimu
hiyo. Hicho kitakuwa kikao kirefu zaidi cha Bunge kuwahi kukaa nchini
Tanzania.
“Kutokana na unyeti wa suala lenyewe muswada huo
unampa nguvu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuongeza siku 20
ili kujadili katiba,” aliongeza Chikawe.
Imeandikwa na Daniel Mjema na Sharon Sauwa
source: Mwananchi
Imeandikwa na Daniel Mjema na Sharon Sauwa
source: Mwananchi