Thursday 5 September 2013

Mahakama ijichunguze kuhusu tuhuma hizi

 


Posted  Jumatano,Septemba4  2013  saa 20:51 PM
Kwa ufupi
  • Tumewahi kusema katika safu hii kwamba mmoja wa majaji waadilifu wanaochukia rushwa kwa dhati kabisa ni Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu.


Mahakama Kuu imewakingia kifua majaji na mahakimu dhidi ya tuhuma kwamba baadhi yao wamekuwa wakiwaachia au kutoa dhamana kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya kinyume cha sheria na kusababisha watoroke. Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu amesema Mahakama haipaswi kubebeshwa lawama katika suala hilo, bali Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ambayo amesema imekuwa haitimizi masharti ya kisheria wanapofungua kesi mahakamani.
Kauli hiyo ya Jaji Jundu ni nzito na imekuja baada ya gazeti moja hapa nchini kuchapisha habari iliyotaja majina ya baadhi ya mahakimu na majaji iliyodai kwamba wamekuwa wakiwalinda washtakiwa wa dawa za kulevya. Uzito wa kauli hiyo hasa unatokana na kitendo chake cha kuelekeza lawama hizo kwa mhimili mwingine wa dola, yaani Serikali kupitia Ofisi ya DPP.
Shutuma na tuhuma hizo dhidi ya Mahakama zimekuwapo kwa muda mrefu, ingawa hakuna chombo cha habari kilichowahi kuweka hadharani majina ya mahakimu na majaji na kuwatuhumu kupokea rushwa na kuwaachia au kutoa dhamana kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Pamoja na kwamba Mahakama imekuwa ikitajwa kuwa moja ya taasisi ambazo zinanuka rushwa, ukweli ni kwamba baadhi ya mahakimu na majaji wamekuwa na rekodi ya uadilifu na utumishi uliotukuka. Tumewahi kusema katika safu hii kwamba mmoja wa majaji waadilifu wanaochukia rushwa kwa dhati kabisa ni Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu.
Hivyo ni rahisi kumwelewa Jaji Jundu pale anapotaharuki na kufadhaishwa na hatua ya gazeti hilo ya kuituhumu Mahakama kwa kuzorotesha vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya. Pia tunamwelewa pale fadhaa hiyo inapomtuma kufikiria kulipeleka gazeti hilo mahakamani ili litoe ushahidi wa tuhuma hizo.
Hata hivyo, tungependa kumshauri Jaji Jundu na Mahakama kwa jumla kwamba haitapata manufaa au tija yoyote kupambana na mtoa tuhuma badala ya kujielekeza kwanza katika kuchunguza tuhuma zenyewe. Yafaa ieleweke kwamba uadilifu na unyofu wa Jaji Jundu na baadhi ya mahakimu na majaji hauwezi kamwe kuwa kielelezo kwamba mahakimu na majaji wote ni waadilifu na wanyofu.
Itakumbukwa kwamba shutuma hizo dhidi ya Mahakama zilichangiwa na matukio mengi ya kulundikana mahakamani kwa miaka mingi kesi za dawa za kulevya bila kutolewa uamuzi. Kesi nyingine zilikuwa zinaisha kimyakimya tu. Tukio la hivi karibuni ambapo raia wawili wa Pakistan waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya dawa za kulevya walitoroka baada ya kupewa dhamana na jaji mmoja wa Mahakama Kuu, kinyume na Sheria Na. 9 ya mwaka 1995.
Ni kweli alivyosema Jaji Jundu kwamba sheria hiyohiyo, katika kifungu Na. 27 (1) (b) kinamtaka DPP kuambatanisha katika hati ya mashtaka kiapo kinachoonyesha thamani halisi ya dawa za kulevya alizokamatwa nazo mshtakiwa. Lakini hata kama DPP hakufanya hivyo kwa makusudi au bahati mbaya, kwa nini Mahakama zisiwe na uzalendo na utaratibu wa kisheria wa kumrudishia DPP hati hiyo ili kasoro zilizojitokeza zifanyiwe marekebisho kama tunavyoshuhudia Bunge likirudisha serikalini miswada iliyowasilishwa pasipo kuwa na vichwa wala miguu?
Yapo madai kuwa, kwa sababu ya rushwa Ofisi ya DPP kwa makusudi inapeleka mahakamani hati za mashtaka zenye makosa. Hata hivyo, tunadhani uovu katika vyombo vya dola utaisha baada ya ujio wa Katiba Mpya.

source: Mwananchi