Urusi yaigomea ICC kesi ya Greenpeace
Serikali ya Urusi imesema kuwa haitafika katika kesi dhidi yao kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC Uholanzi.
Serikali ya Urusi imesema kuwa haitafika katika kesi dhidi yao kwenye
mahakama ya kimataifa ya ICC Uholanzi, ambapo inakabiliwa na mashitaka
ya kuikamata meli ya Uholanzi, iliyokuwa na wanamazingira wa kimataifa
katika eneo la bandari ya mji wa Murmansk nchini Urusi.
Wanaharakati hao wa kimazingira pamoja na waandishi wa habari, walikuwa
katika ziara ya mgomo wa kupinga shughuli za uchimbaji mafuta katika
eneo la bahari huru, zinazoendeshwa na kampuni ya uchimbaji mafuta ya
Serikali ya Urusi.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema, nchi
yake imeitaarifu Uholanzi na mahakama ya kimataifa ya ICC kuwa,
kuhusiana na sheria ya mipaka ya bahari, haitashiriki katika kesi hiyo
na kuongeza kuwa Urusi itashughulikia hali hii inayojitokeza baina ya
nchi hizo mbili, bila ya kufafanua kwamba watahitaji nini kwa maridhiano
ya baadae.
Taswira Mpya ya uhusiano
Uamuzi huo unapelekea hatua nyingine ya kuongezeka kwa mvutano baina ya
nchi hizo mbili zenye uhusiano wa kibiashara kwa muda mrefu, ambapo kwa
sasa kuna mfululizo wa visa wanavyofanyiana nchi hizo, ikiwa ni pamoja
na afisa wa kibalozi wa Urusi aliyetiwa nguvuni nchini uholanzi kwa
madai ya kumtesa mtoto wake na kwa upande wa Urusi, wametishia kuzuia
uingizwaji bidhaa kutoka Uholanzi na wiki iliyopita afisa wa kibalozi wa
uholanzi nchini Urusi alipigwa nyumbani kwake mjini Moscow na mtu
asiejulikana na kumwandikia ujumbe katika kioo wa kumtaka kuunga mkono
haki za mashoga.
Uholanzi ilitangaza kuishitaki serikali ya Urusi katika mahakama ya
kimataifa ya ICC kufuatia kukamatwa kwa meli yake katika bandari ya
Murmansk nchini Urusi mwezi uliopita , iliyokuwa na wanaharakati wa
mazingira wa kimataifa kutoka nchi 18, na waandishi wa habari, waliokuwa
katika harakati za kupinga mradi unaoendeshwa na Urusi wa kuchimba
mafuta katika eneo huru la bahari . Kesi hiyo katika mahakama ya
kimataifa ya ICC iliyofunguliwa na Uholanzi, inaitaka serikali ya Urusi
kuiachia meli hiyo pamoja na wanaharakati wakiwamo waandishi wa habari
waliokuwa humo. kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa wiki mbili au
tatu kuanzia sasa.
Aidha serikali ya Urusi imewafungulia mashitaka ya uharamia wanaharakati
hao, ambayo kwa sheria za Urusi makosa ya uharamia adhabu yake ni
kifungo cha miaka 15 jela.
Nchi hizo mbili zenye mvutano,
Mahakama ya icc
tayari zimefikia hatua ya kutishiana kuvunja mahusiano ya kibiashara na
kibalozi. Mapema mwezi huu afisa wa ngazi ya juu wa afya wa Urusi,
alitoa onyo kuwa Moscow inaweza kuzuia uingiaji wa bidhaa za vyakula
kutoka uholanzi kwa sababu za usalama wa kiafya kwa walaji.
Pia Urusi imeshutumiwa kwa kutumia uhusiano wa kibiashara kama silaha
katika masuala ya kidiplomasia ,ambapo iliwahi kusimamisha uingiaji wa
vyakula kutoka nchi za umoja wa Ulaya na nchi zilizokua katika Muungano
wa Jamhuri ya Ki-sovieti, ambao sasa umesambaratika.
Mvutano huo kati ya Urusi na uholanzi ulipamba moto wakati polisi mjini
The Hague walipomkamata afisa wa kibalozi wa Urusi nchini Uholanzi, kwa
madai ya kumtesa mwanawe ambapo baadae walimwachia afisa huyo. Hata
hivyo serikali ya uholanzi iliomba radhi kwa hilo kutokana na kukiuka
masharti ya mkataba wa Vienna, unaohusu makubaliano ya taratibu za
kidiplomasia za kimataifa
Mwandishi:Diana Kago/AFP/DPA
Mhariri: Moahammed Abdul-Rahman
Mhariri: Moahammed Abdul-Rahman
SOURCE: DW