Monday, 28 October 2013

Mahakama yatishiwa kuchomwa sababu ya rushwa

28th October 2013
Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola.
Baadhi ya wananchi wa Tarafa za Nansimo na Kenkombyo, katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wametishia kuichoma moto Mahakama ya Mwanzo ya Nansimo, kwa madai kuwa hakimu wa mahakama hiyo hawatendei haki katika maamuzi.

Wananchi hao walitoa kero hiyo juzi katika kijiji cha Nansimo kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola.

Walisema kutokana na watumishi  wa mahakama hiyo kutowatendea haki katika maamuzi na kushughulikia kesi zao, wako tayari kufanya lolote kwake ikiwa ni pamoja na kuchoma majengo ya mahakama hiyo ikiwa baadhi yao hawatahamishwa.

Walidai kuwa mahakama hiyo imegeuzwa na watumishi kama kijiwe cha kujipatia rushwa kutoka kwa wananchi wanaokabiliwa na kesi.

Aidha, wananchi hao waliokuwa wamebeba mabango ya ujumbe wa kuilahumu mahakama hiyo, walidai inatoa maamuzi ya kesi ambazo haziihusu zikiwamo za ardhi ambazo hushughulikiwa na mabaraza ya ardhi ya kata.

Pia walidai kuwa kesi za madai zikiwamo za mashamba, zimekuwa zikigeuzwa na kuwa za jinai ili kumdhoofisha mshtakiwa kwa lengo la kujipatia rushwa.

Walisema pia mahakama hiyo imekuwa ikitoa hati ya kukamatwa kwa mtu yeyote anayetoa kero za mahakama hiyo kwenye mikutano inayoitishwa na viongozi mbalimbali.

Mathalani, walisema hivi karibuni, Diwani wa kata hiyo, Sabato Mafwimbo (CCM), aliandikiwa barua ya wito wa kuitwa mahakamani baada ya kuhutubia wananchi waliokuwa wakitoa kero za mahakama hiyo.

“Kama (anamtaja jina mtumishi mmoja), hatahamishwa na kupelekwa sehemu nyingine, sisi wananchi tunamhakikikishia kuwa ipo siku tutafanya lolote kwake…mimi nilikuwa mtu wa kwanza kushawishi wananchi kwamba iwapo diwani huyo akichukuliwa na kuhukumiwa, tuchome moto mahakama hiyo au kuua mtu,” alisema mwananchi mmoja huku akishangiliwa.

Walisema kuwa mbali na hayo, pia mtumishi mmoja (jina tunalihifadhi), anatuhumiwa kujipatia fedha kwa njia za rushwa kwani kila kesi inayofikishwa katika mahakama amekuwa kikwazo kwa dhamana ya mtuhimiwa.

Walismea kitendo hicho huwafanya watuhumiwa wapelekwe mahabusu katika Gereza la Bunda kwa muda wa siku 14, lengo likiwa ni kujenga mazingira ya kujipatia rushwa.

Waliongeza kuwa kesi ambazo washtakiwa wamekuwa wakihukumiwa kwa kutoa faini, stakabadhi halali za serikali hazitolewi, badala yake huandikiwa kwenye karatasi na kupiga muhuri wa mahakama hiyo.

Kwa msingi huo, wananchi hao wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine kufanya uchunguzi kuhusiana na faini hizo.

Wananchi hao waliwataja watumishi wawili wa mahakama hiyo na mgambo mmoja kwamba wamekuwa wakitumika kuandikia washtakiwa bara za wito maakamani kinyume cha sheria huku wakimtaka mlalamikaji atoe Sh. 5,000.

Pia walisema kuwa hivi karibuni wanawake wawili wajasiriamali wakazi wa kijiji cha Nansimo, walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela au faini ya Sh. 400,000 kila mmoja kwa kosa la kutokuwa na vyoo kwenye maeneo yao ya biashara.

Akijibu kero hizo, Lugola aliwataka wananchi hao kuacha kuchukua sheria mkononi kwa kuchoma moto mahakama hiyo na kwamba kero zao amezichukua na atazipeleka kunakohusika ili zitafutiwe ufumbuzi.

Mbunge huyo alisema kuwa katika mkutano huo asingeingilia uhuru wa mahakama, ila anasikiliza kero za wananchi katika matukio ya kesi ambazo zimeshatolewa maamuzi na kwamba ni haki ya wananchi hao kulalamika na kutoa kero zao kwa viongozi waliowachagua.

“Mahakimu ni watumishi wa umma, wanalipwa msharaha na kodi zenu…hapa Nansimo kumeibuka mamba mla watu kwenye chombo kinachotoa maamuzi ya kisheria, sasa wana-Nansimo tutakimbilia wapi?” Alihoji.

Aidha, alisema alilazimika kwenda katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda kuwalipia faini wanawake wawili walikokuwa wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela, kwa makosa ya kutokuwa na vyoo kwenye maeneo ya biashara zao.

Aliongeza kuwa pia alikwenda katika gereza la Nyasura na kushuhudia msongamano mkubwa wa mahabusu katika gereza hilo huku idadi kubwa wakiwa ni kutokea katika mahakama hiyo.

Mbunge huyo alisema kwa mjibu wa Mkuu wa gereza hilo, uwezo wake ni kupokea mahabusu na wafungwa 217, lakini kwa sasa kuna mahabusu zaidi ya 400.

Aliongeza kuwa pia bweni la kuhudumia wafungwa wanatakiwa wawe 43, lakini kwa sasa kuna wafungwa 136, hali ambayo alisema ni hatari kwani kuna msongamano mkubwa.

Lugola aliwaambia wananchi hao kuwa vielelezo walivyompatia atavipeleka Takukutu na pia atamuona Mkuu wa Wilaya ya Bunda, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Mahakama ya Wilaya na baadaye kukutana na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, kuwasilisha kero hizo.

Lugola alisema kuwa kuna baadhi ya mahakimu ambao siyo waadilifu ambao wamekuwa wakitumia vibaya madaraka kuonea wananchi na kuahidi kwamba ataendelea kuwatetea pale wanapoonewa.

Hakimu wa mahakama hiyo, Juma Dishon, hakupatikana kuzungumzia madai ya wananchi hao dhidi ya mahakama yake.
 
CHANZO: NIPASHE