- JWTZ watisha, maofisa Maliasili 16 wakamatwa
- Mmoja akutwa anamiliki bunduki 5 za rifle kali
- Mbunge Mtutura ahojiwa, Nchambi naye atajwa
- RCO aliahidiwa dola 3,000 akawaachia Waarabu
Operesheni
Tokomeza inayoendeshwa chini ya usimamizi wa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), imewakamata watumishi kadhaa wa Serikali
wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili. Operesheni hiyo inaongozwa na Luteni Kanali A. Sibuti.
Pamoja na watumishi hao, wamo pia baadhi ya wabunge waliohojiwa na
wengine wakitarajiwa kuhojiwa. Miongoni mwa waliohojiwa ni Mbunge wa
Tunduru, Mtutura Mtutura (CCM).
Mtutura amezungumza na JAMHURI na kukiri kuhojiwa na makamanda wa Operesheni Tokomeza. Hata hivyo, amesisitiza kuwa hajihusishi na ujangili.
Uchunguzi
uliofanywa umebaini kuwa wabunge wengine, akiwamo Mbunge wa Kishapu,
Suleiman Nchambi (CCM), watahojiwa wakati wowote kuanzia leo. Kwa upande
wake, Nchambi ameliambia JAMHURI kwamba hana taarifa za kuwamo kwenye
orodha ya watuhumiwa wa ujangili wanaotakiwa kuhojiwa.
Majina ya watuhumiwa yaanza kuanikwa
Hakuna
shaka kuwa watuhumiwa wakuu wa mtandao wa ujangili nchini ni watumishi
wa Wizara ya Maliasili na Utalii wenyewe kuanzia Makao Makuu, Dar es
Salaam hadi ngazi za chini kabisa wilayani na ndani ya hifadhi za taifa.
Mmoja wao amekamatwa akiwa na bunduki tano aina ya rifle.
Operesheni
hiyo imebaini kuwa pamoja na watuhumishi hao, mtandao wa uhalifu
umeimarika hadi ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na Mahakama.
Uvunjaji
wa mtandao huo umeanzia kwa watumishi wengi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii. Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Mohamed Ismail, anayetuhumiwa
kujihusisha na ujangili, sasa amefikishwa mahakamani kujibu mashitaka.
Mohamed Hassan Kidunda ambaye ni Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, naye amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma kama hizo.
Katika
Wilaya ya Serengeti, Omary Lutiginga, ambaye ni Afisa Wanyamapori,
wilayani Mugumu, naye anahojiwa kwa kujihusisha na ujangili.
Mhasibu
wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Jail
Adamson Mwakabenga, amefikishwa mahakamani kwa kukutwa akiwa na pembe
mbili za ndovu.
Afisa
Wanyamapori Wilaya ya Bariadi, Jesca Mathias, naye amefikishwa
mahakamani baada ya kukamatwa akiwa na silaha na risasi, ngozi za chui
(mbili) ngozi ya chatu, na meno ya kiboko. Silaha alizokamatwa nazo ni
bunduki tano za rifle aina ya 458, risasi za shotgun 107, risasi za
rifle 306 (47) na risasi moja ya Sub Mchine Gun (SMG).
Derrick
Kasano Mboneka ambaye ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya
Maswa, anahojiwa kwa kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Msiba
Chiraka ambaye pia ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa,
naye amekamatwa akiwa na bunduki ya kivita aina ya SAR na risasi 13.
Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Michael Andrew, naye anahojiwa akituhumiwa kujihusisha na ujangili.
Mhifadhi
Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa, Yasinta Modest, amekamatwa
akiwa na silaha ya kazini aina ya SAR na risasi 21 nyumbani kwake.
Philimony
Ntandu ambaye ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa
anahojiwa kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kwenye orodha hiyo wapo pia William Lugobi Peter ambaye ni Afisa Wanyamapori, KDU Arusha.
Operesheni Tokomeza imemnasa pia Deonatus Makene ambaye ni Afisa
Wanyamapori Arusha. Anahojiwa kwa tuhuma za kuwasaidia wahalifu wa
tuhuma za ujangili.
Afisa Wanyamapori KDU Arusha, Michael Melakiti anahojiwa kwa tuhuma kama zinazomkabili Makene.
Afisa
Wanyamapori Wilaya ya Serengeti, Cuthbeth Boma, yeye amefikishwa
mahakamani kwa kosa la kupatikana na pembe 10 za ndovu, tembo; meno
manane ya kiboko na mikia sita ya ndovu.
Katika
eneo la Ngorongoro nako Operesheni Tokomeza imeingia. Aliyenaswa ni
Fredrick Flegence ambaye ni Askari Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa
ya Manyara. Anahojiwa kwa tuhuma za kuua wanyama ndani ya Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Askari
Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Manyara, Novatus Mosha, anahojiwa
kwa tuhuma za kuua wanyama ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Makuyuni, Monduli mkoani Arusha,
Bakari Salim (32), naye ni miongoni mwa waliotiwa mbaroni akiwa na kilo
40 za pembe za ndovu.
Pamoja
na hao, bado majangili wengine wanalindwa na viongozi wa Wizara ya
Maliasili na Utalii. Majangili hao ni Raia wa Ugiriki Pano Canavias na
raia wa Afrika Kusini, John-Martin Venter. Huyu alikamatwa mwaka 2011 na
wenzake wawili, lakini aliachiwa huku magari yao yakiwa na wanyamapori
waliouawa. Kwa mujibu wa jarida la The Hunting Report, Venter anaendelea
kuwinda katika vitalu vya moja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Utekelezaji
wa Operesheni Tokomeza ulianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika maeneo
ambayo yamelemewa kwa matukio ya ujangili. Imegawanyika katika Kanda
nne. Inashirikisha JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa (TANAPA), NCAA, na Idara ya Wanyamapori.
Vituko vya maafisa
Kamati
inayoongoza operesheni hii imekutana navituko vya mwaka. Sheria
inawataka askari wanyamapori kurejesha silaha wanazokuwa nazo wakati wa
kazi na kuzisajili katika kitabu maalum, lakini operesheni imebaini kuwa
silaha zote ikiwamo bunduki wanakaa nazo nyumbani kama mali zako kwa
saa 24 hata siku wasizokuwa kazini.
Kilichoisikitisha
kamati inayoendelea na operesheni, imebaini kuwa wengi wa maofisa hao
walioshitakiwa walikuwa na tabia ya kukodisha bunduki za Serikali kwa
majangili ambao walikuwa anatumia bunduki na risasi za serikali kuua
tembe wanaopaswa kuwalinda.
“Kilichosikitisha
wengi wamekutwa na pembe za ndofu kwenye ofisi zao na nyumbani kwao,
ambazo hazikusajiliwa popote wakati sheria iko wazi kuwa wakikamata
pembe za ndogu wanapima uzito na kusajili kwenye kitabu maalum kisha
zinatunzwa,” kilisema chanzo chetu.
Pia
chanzo kingine kilisema kuwa ilikuwa imefikia hatua ambayo maafisa
wanyamapori wakikamata mtuhumiwa ana pembe za ndovu zenye uzito wa kilo
20 au zaidi, wanauza pembe hizo kisha wanatafuta pembe za tembo wadogo
zenye uzito wa kilo saba au chini ya hapo na kuzihifadhi kama ushahidi
wa pembe zilizokamatwa kumbe pembe halisi ziliishauzwa siku nyingine.
Baadhi
ya maofisa wa polisi wasio na biashara ya aina yoyote wamethibitika
kumiliki fedha na majumba makubwa wasiyoweza kuthibitisha iwapo
imetokana na mishahara wanayolipwa.
RCO Arusha atorosha majangili
Uchunguzi unaonyesha kuwa Operesheni hii imewatia mbaroni raia wengi
mno wa ndani na nje ya nchi, lakini mara kadhaa wanaoiendesha
wamekumbana na matukio ya kuingiliwa, ama na watendaji serikalini, au
wanasiasa wenye mamlaka makubwa.
Katika
tukio la Arusha, raia wa kigeni wawili kutoka Saudi Arabia walikamatwa
mwanzoni mwa mwezi huu. Raia hao ni Alhassan Alli Auwayship mwenye hati
ya kusafiria namba IC 886898 na Nader Ali Mbooh mwenye hati namba L
381854.
Walikamatwa
Loliondo baada ya taarifa za kiintelejensia wakiwa na kilo 84 za pembe
za ndovu na silaha mbili. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa
waliachiwa kwa amri ya Mkuu wa Upelekezi (RCO) Mkoa wa Arusha wa Arusha,
Duani Nyanda akishirikiana na msaidizi wake kutoka katika Kituo Kikuu
cha Polisi Arusha Mjini, OCD Ngonyani.
Taarifa
zinaonyesha kuwa watuhumiwa hao walitakiwa kuachiwa kwa sharti kuwa
wangetoa dola 3,000 (Sh milioni 4.8) kwa kamanda huyo wa polisi ili
awaachie watuhumiwa hao. Dola moja ya Marekani ni shilingi zaidi ya
1,600.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI
umebaini kuwa baada ya kuachiwa, hati za kusafiria zilibaki kituoni ila
baada ya muda na kwa maelekezo ya vigogo walirudishiwa na hivyo
kuwafanya watoroke.
Walioshiriki
kuwawekea dhamana ni Salum Islam Salehe, ambaye ni raia mwenye asili ya
Kiarabu. Kwa mjini Arusha, Salehe anajulikana kwa jina maarufu la
“Kichwa”. Inadaiwa kuwa huyo ndiye aliyefanikisha kutoroka kwa
watuhumiwa hao.
Salehe
imebainika kuwa ni wakala wa kupokea wageni kutoka nje ya nchi na
kufanya mipango ya kuwinda. Kazi hiyo ameifanya kwa muda mrefu.
Oktoba
7, mwaka huu Salehe akiwa na wenzake, Shafii Firozi Dalla (ambaye ana
asili ya Kiasia), Gerald Kashiro Joseph ambaye ni Mtanzania, walikamatwa
kwa tuhuma za kujihusisha na uwindaji haramu.
Hata
hivyo, mtuhumiwa Salehe hadi jana taarifa zinaonyesha kuwa alikuwa
hajaandikiwa hati ya mashitaka, jambo ambalo lilionekana wazi kuwa
kulipangwa aachiwe bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Watuhumiwa ni wengi mno
Taarifa kutoka ndani ya Operesheni hiyo zinasema kuwa idadi ya watuhumiwa wanaokamatwa pamoja na zana zao ni kubwa mno.
“Tunakamata
bunduki za kivita ambazo hatujawahi kuziona hapa Tanzania , zina
darubini na hiyo inathibitisha kuwa wana uwezo wa kumlenga na kumuua
tembo akiwa mbali kabisa.
“Ukubwa
wa janga hili la ujangili unawafanya viongozi wetu wanuie kuomba
waongezwe muda ili kuendelea kutokomeza majangili haya, kama hali hii
ingeachwa, nakuhakikisha ndani ya miaka mitano Tanzania isingekuwa na
tembo wala mnyama yoyote porini,” kimesema chanzo chetu.
Habari
ambazo hazijathibitishwa zinasema Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Kikwete
ameamua kuongeza muda wa Operesheni hiyo. Hadi sasa Serikali haijapokea
msaada wa kifedha kutoka nje kufadhili operesheni hii. Fedha zote za
operesheni zinatoka Hazina ya Tanzania .
JAMHURI
lilikuwa la kwanza kuandika kuanza kwa Operesheni Tokomeza katika toleo
lake namba 104. Hata hivyo, viongozi kadhaa wa Wizara ya Maliasili na
Utalii walikanusha jambo ambalo tayari Rais Kikwete alishautangazia
ulimwengu wakati akiwa Marekani.
Baada
ya Operesheni Tokomeza kuzinduliwa, kilichofuata ni kusambazwa kwa
askari katika mapori mbalimbali, wakianza na yale yaliyoandamwa mno na
majangili. Kati ya mapori hayo ni Pori la Akiba la Selous ambalo
linajulikana miongoni mwa majangili kama ‘shamba la bibi.’
Kamati ya Bunge: Tembo wanakwisha
Kamati ya Kudumu ya Bunge imesema ujangili dhidi ya tembo kwa sasa ni janga la kitaifa.
“Ni
ukweli usiofichika kwamba leo hii si tu tembo wanauawa, bali
wanateketezwa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa
Wanyamapori (TAWIRI), taarifa zinazoshabihiana na za utafiti wa
kimataifa zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku,
tembo 850 wanauawa kwa mwezi, na tembo 10,000 wanauawa kila mwaka
(TAWIRI 2011).
“Kutokana
na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu kutokana TAWIRI
zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka
2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka 2012.
“Endapo
kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa mara moja, ni
wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka
saba ijayo,” imeonya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James
Lembeli.
Kamati
hiyo imeongeza kusema, “Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi yetu ambayo
ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo.
Kinachosikitisha ni kwamba Wizara imekuwa na kigugumizi katika kuitikia
kauli ya Rais Jakaya Kikwete iliyoitaka Wizara kuomba msaada kwake kama
tatizo la ujangili limewashinda. Jambo hili linaweza kutafsiriwa kuwa ni
hujuma inayofanywa na baadhi ya watendaji wa Wizara ambao wamepuuza
kauli ya Mheshimiwa Rais.”
Kamati
inapendekeza kufanywa kwa Operesheni kama Operesheni Uhai kwa nchi
nzima kama ilivyofanya miaka ya 1980. Pia imependekeza Sheria ya
Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho kwa kuweka adhabu
kali kwa watu watakaothibitika kuhusika na ujangili, hasa wa tembo.
SOURCE: JAMHURIMEDIA
|